Samatta, Cannavaro wote wanajenga nyumba moja

18Jan 2016
Nipashe
Samatta, Cannavaro wote wanajenga nyumba moja

TANGU Kocha Mkuu wa timu ya taifa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alipomteua mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wa ndani Mbwana Samatta kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa kumekuwa na mijadala mbalimbali imeibuka.

TANGU Kocha Mkuu wa timu ya taifa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alipomteua mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wa ndani Mbwana Samatta kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa kumekuwa na mijadala mbalimbali imeibuka.
Mijadala kama hii ni kawaida sana, hasa kwenye mitandao ya kijamii na hata makala kwenye magazeti mbalimbali.
Kila mmoja ana uhuru wa kutoa maoni yake na jinsi mtazamo wake unavyomtaka kuwa.
Lakini kwa jinsi hali inavyokwenda naona tunaanza kubomoa badala ya kujenga.
Wapo wanaoliona suala ya Mkwasa kumwondoa Nadir Haroub 'Cannavaro' kwenye unahodha kama ni kosa kubwa linalostahili adhabu.
Kuna wanaoamini kuwa Samatta bado hakuwa na uwezo wa kuwa nahodha mbele ya Cannavaro.
Baadhi wanasema pamoja na uchezaji bora wake, lakini kwa umri wake bado angeendelea kuwa mchezaji wa kawaida na siyo muda muafaka kwake kuuvaa unahodha.
Wengine wanasema kuwa Mkwasa ni kama amemdhalilisha beki huyo bora kabisa nchini kwa kutompa taarifa ya kumwondoa kwenye unahodha ya badala yake angempa taarifa kwanza.
Hawa wapo tofauti kidogo. Wanaona Samatta anafaa, ila Cannavaro hakuvuliwa kiungwana.
Ni kweli kabisa, inawezekana Mkwasa amekosea kwa hilo, lakini sidhani kama iwe kigezo cha kumsakama na eti kumlazimisha amuombe radhi beki huyo.
Baadhi wanakwenda mbali zaidi na kusema kuwa kitendo hicho kimemkera sana Cannavaro kiasi cha kufikia kuandika barua ya kustaafu kuichezea Taifa Stars baada ya kuitumikia kwa miaka 10.
Hata hivyo, kwa uungwana kabisa na ukweli toka ndani ya moyo wake, Cannavaro mwenyewe anasema kuwa sababu kuu ni lawama lukuki alizorushiwa kwamba amekwisha na alichangia Taifa Stars kufungwa mabao 7-0 na Algeria ikiwa ugenini.
Ya pili, ndiyo anagusia ya kuvuliwa unahodha na kupewa Mbwana Ally Samatta mara tu baada ya kutwaa tuzo ya mwanasoka bora Afrika kwa wanasoka wanaocheza ndani ya Afrika.
Akasema kuwa hapingi yeye kuvuliwa unahodha, wala halazimishwi kubakiwa nao, lakini utaratibu uliotumika haturidhika nao.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, kocha mkuu ndiye ana mamlaka ya kuteua nahodha ya timu wakati wowote na katika mazingira yoyote yale ambayo anaona yanafaa.
Inawezekana kabisa Mkwasa amefanya kosa kwa kutomtaarifu kwanza mhusika, lakini pamoja na hayo haiondoi ukweli kuwa yeye ndiye anayeamua.
Na kwa Watanzania ninavyowajua hata kama angempa taarifa na Cannavaro mwenyewe akaafiki bila kinyongo, bado wangeendelea kuhoji ni kwa nini amenyang'anywa na kupewa Samatta kama wengine wanavyodai kuwa bado hastahili.
Mimi nadhani suala ya unahodha kwenye timu ya taifa lisikuzwe sana na kuonekana kuwa ndiyo kuchaguliwa au kuondolewa kwao kutasababisha timu ishinde au ifungwe.
Kuna mengi ya kujadili kwa ajili ya soka na timu ya taifa ambayo inakabiliwa na michuano ya AFCON, nini cha kufanya ili kushinda mechi zijazo ni si nani anastahili kuwa nahodha na kwa wakati gani.
Hii itakuwa ni sawa na wale waliokuwa wanazozana nani atafagia banda la kuku wakati bado hawajanunuliwa.
Jinsi ninavyowasikia mashabiki wa soka, na ninavyowasoma kwenye mitandao, suala hili limeenda mbali zaidi na kuhusisha hata ushabiki wa klabu kongwe za Simba na Yanga. Hii ni hatari.
Huko nyuma tumeona athari za aina hiyo, kiasi cha baadhi ya mashabiki wa klabu moja kususa kuishangilia Taifa Stars.
Tukiendelea na mjadala huu na kuufanya kuwa ni jambo la ajabu na halijawahi kutokea popote pale duniani, kwanza kabisa tutaiweka Stars kwenye wakati mgumu.
Lakini pia hata Samatta mwenyewe hatoufurahia unahodha kwa sababu wapo wataoona amepewa kwa njia za 'panya' kwa hiyo.
Vilevile, kutokana na mjadala kukuzwa bila sababu za msingi sana, anaweza hata kuukataa ili kulinda heshima yake, na hii si tu kwamba itakuwa haipendezi, lakini inaweza kuwa athari kwa timu yenye ya taifa.
Unahodha kwenye timu yoyote ni kitu kinachokuja na kupita, inawezekana kabisa akaja kocha mwingine kwenye kikosi kicho na kutoa Samatta.
Nadhani sasa huu ni wakati wa Watanzania wote kuungana kwa pamoja kuiunga mkono timu ya taifa Taifa Stars kwenye michuano ambayo imebaki ya AFCON ili ifanye vizuri, kuliko kujadili nani anafaa kuwa nahodha na nani hafai.
Tukumbuke kuwa wote tunajenga nyumba moja tu, iweje tuanze kugombea fito?