Serikali kutembeza panga vyuo vikuu

13Jan 2016
Nipashe
Serikali kutembeza panga vyuo vikuu

BAADHI ya vyuo vikuu nchini viko hatarini kufutwa baada ya serikali kuamua kuvipitia ili kujiridhisha kama vina sifa stahiki.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, aliliambia gazeti hili kwamba uamuzi huo unakuja baada ya kubaini kwamba licha ya vyuo vingi kuwa na ithibati, bado baadhi havina sifa ya kuwa vyuo vikuu.

Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), takriban vyuo vikuu 60 ithibati na vinahesabika kuwa ni vyuo vikuu kamili.

“Hatutaki vyuo ambavyo vipo vipo tu. Tutavikagua upya kuangalia kama vinakidhi vigezo na hata uhalali wa ithibati vilivyopewa,” alisema Prof. Ndalichako.

Aliongeza kuwa vyuo vitakavyothibitika kuwa havifai vitafungwa bila kusita kwa kuwa serikali haitaki Watanzania wafanyiwe majaribio katika elimu. Alisema ni bora ijulikane wazi kuwa hakuna chuo kikuu kuliko kumpeleka mwanafunzi mahali halafu akatoka mtupu.

“Kuwa na vyuo vingi ambavyo havina sifa, kunachangia kuwa na vijana wengi mtaani ambao hawana ajira, jambo ambalo linawaongezea hasira,” alisema Ndalichako.

Prof. Ndalichako alisema serikali itaangalia pia taratibu zinazotumiwa kutoa ithibati kwa sababu kumekuwa na kilio kikubwa kwa umma, wengi wakilalamika kuwa wanafunzi wanamaliza vyuo vikuu wakiwa hawana na uwezo hafifu.

“Kila mtu analalamika, lakini tumechukua hatua gani? Je, tumekaa chini na kuangalia vigezo na kuona ili mtu awe na chuo anatakiwa kuwa na sifa gani? Anatakiwa awe na watu wa aina gani?.

“haiwezekani mtu mwenye shahada moja amfundishe mwanafunzi wa shahada ya kwanza. Wa kumfundisha huyu anatakiwa angalau awe na shahada ya uzamili, ingawa nayo haitoshi… inatakiwa angalau asilimia 50 ya walimu wa kila chuo kikuu wawe na Ph.D (shahada ya uzamivu),” alisema.

Profesa Ndalichako pia alisema kuna vyuo ambavyo mtu akienda kufundisha hata kwa saa moja tu, anaingizwa kwenye orodha ya walimu waajiriwa.

“Tunaposema walimu, tunamaanisha wale ambao wameajiriwa na chuo. Tunaposema tunaangalia ubora wa elimu, itabidi tuangalie utoaji wa ithibati na kujiridhisha kwamba mambo ambayo tunasema yanatakiwa yawepo ili chuo kiitwe chuo kweli yawepo.

‘Kuna wengine wanafanya chuo kama sehemu ya maonyesho. Siku ile unaenda kukagua unakuta maabara na vitu vingine, kumbe vyote vimeazimwa,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia ubora wa elimu ya juu lazima ziwe na mfumo wa kukagua na kufuatilia mara kwa mara na si kuangalia tu wanafunzi wakiwa vyuoni, bali hata baada ya kumaliza na kwenda kwenye soko la ajira ili kusikia waajiri wanawazungumziaje.

Alisema ili kufikia lengo la Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati, kama ambavyo serikali ya awamu ya tano inatamani, lazima viwango vya elimu viangaliwe upya.

KWA NINI HAKURUDI NECTA?
Nipashe ilipotaka kujua sababu za Profesa Ndalichako kutorudi Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania (Necta) baada ya kumaliza likizo ya mwaka mmoja bila malipo, alisema ni kwa sababu aliamua kujiendeleza kielimu.

“Necta nilikaa miaka tisa, niliona mambo mengi niliyotamani kufanya nimefanya, hivyo nikaona pia kitaaluma watu niliowaacha chuo kikuu (Dar es Salaam) wakiwa walimu wenzangu ni maprofesa. Nikaoana na mimi nijiendeleze kitaaluma,” alisema.

Ili kupata daraja la uprofesa, wanataaluma ambaye amefikia hatua ya mhadhiri mwandamizi, anapaswa kufanya utafiti wa kitaaluma na ushauri elekezi. Utafiti wake huo unatakiwa kuchapishwa kwenye majarida ya kitaaluma kitaifa na kimataifa.

Kutokana na kiu yake hiyo serikali ilimkubalia na baada ya likizo, alirudi chuo kikuu baada ya kuomba na wakamkubalia.

“Nisingerudi hata huu uprofesa nisingeupata. Kwa hiyo kila jambo lina sababu yake na hata nisingeteuliwa (kuwa Waziri) ningejiendeleza kwa sababu sasa hivi mimi ni Associate Profesa (Profesa Mshiriki), lakini nisingeteuliwa kulikuwa na miradi mingine ya utafiti ambayo nimeanza kuitafuta.

“Nilishapata ruzuku kutoka taasisi moja ya Canada na kupata ruzuku ya dola za Marekani 248, 000 (Sh. milioni 530) kwa ajili ya utafiti niliokuwa nifanye Tanzania na Uganda kuangalia walimu wanavyofanya upimaji wwa wanafunzi na humo ndani ningepata machapisho pia,” alisema.

Aliongeza kuwa mwezi wa 12 kuna ruzuku nyingine ambayo ni ya Uingereza, kwenye taasisi iitwayo ESRC aliomba ili afanye utafiti kwenye eneo hilo hilo la upimaji ambalo ndilo eneo lake la kitaaluma.

“Utafiti huu nilikuwa nifanye kwenye shule zilizo kwenye watu wengi ambazo kwa kawaida mahitaji ni meingi kuliko uhalisia. Kwa mfano, uwiano wa mwalimu na wanafunzi haulingani na vitu vingine na nilishapata pauni 697,000 (Sh. bilioni 2.17), kati yake pauni 193,000 (Sh. milioni 599.85) ingekuja kwangu na nyingine kwenye vyuo vya nje ambavyo tungeshirikiana,” alisema.

MASILAHI YA WALIMU
Alisema licha ya kuwa eneo hilo halipo kwenye wizara yake moja kwa moja, ameanza mazungumzo na mwenzake wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambapo pamoja na mambo mengine, wataangalia madeni ya walimu na namna ya kuyalipa.

“Mwalimu hawezi akafundisha kama ana madeni ya hapa na pale. Tutakutana na kuona namna ya kuyakabili ili hata nikikutana na walimu nijue nazungumza na watu wakoje, ingawa nimemwona waziri mwenzangu wa Tamisemi kwenye televisheni akilizungumza na nilifurahi sana,” alisema.

Habari Kubwa