Serikali ya Rais Magufuli na tishio la kuangamiza upinzani

20Jan 2016
Richard Makore
Nipashe
Serikali ya Rais Magufuli na tishio la kuangamiza upinzani
  • Ni magezi makubwa ambayo hakuna mtu aliyethubutu kuyadharau na wote waliokihama CCM walijiunga moja kwa moja na upinzani hususan Chadema

MWAKA jana Watanzania walishuhudia mageuzi makubwa katika siasa za Tanzania ikiwamo viongozi waandamizi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakihama chama na kujiunga na upinzani.

rais john magufuli

Ni mageuzi makubwa ambayo hakuna mtu aliyethubutu kuyadharau na wote waliokihama CCM walijiunga moja kwa moja na upinzani hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Hatua hiyo ya viongozi waandamizi kujiunga na upinzani ilitoa upinzani mkubwa na kugeuza upepo wa kampeni ambazo miaka ya nyuma zilikuwa zimezoeleka hapa nchini.
Licha ya viongozi wa kitaifa wa vyama vya Chadema na Cuf, kujitenga na upinzani dakika za mwisho, lakini hatua hiyo haikuathiri kampeni kama wengi walivyokuwa wamedhani itakuwa.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na aliyekuwa mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba waliviacha vyama vyao dakika za mwisho kabla ya kampeni kuanza mwezi Agosti mwaka jana.
Hata hivyo, Mawaziri Wakuu wastaafu wa serikali wa serikali ya awamu ya tatu na awamu ya nne, Fredrerick Sumaye na Edward Lowassa walibadili mtazamo huo na kufufua matumaini mamkubwa ya kupatikana ushindi.
Miongoni mwa viongozi waandamizi waliokuwa katika serikali ya awamu ya nne ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Dk. Goodluck Ole Medeye anazungumzia hali ya siasa ilivyo hapa nchi kwa sasa.
Dk. Medeye anasema serikali ya awamu ya tano imeanza vibaya kwa kuweka nguvu nyingi katika kujaribu kukandamiza upinzani.
Katika historia ya Tanzania, Dk. Medeye anasema baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi, upinzani ulikandamizwa katia awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa.
Awamu ya tatu vyama vingi vya siasa hapa nchini, anasema vyama vya siasa vilipitia katika kipindi kigumu ikilinganishwa na awamu ya nne ya Rais Kikwete ambaye alitoa fursa za vyama vya upinzani kufanya shughuli zao za kisiasa bila bughudha.
Mwanzo wa serikali hii ya Dk. Magufuli ni mbaya kwa sababu amepiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa na kwamba hatua hiyo ni ukandamizaji wa demokrasia ya kweli hapa nchini.
Anatoa mfano kuwa baada ya kampeni kumalizika na uchaguzi kufanyika, Chadema pamoja na vyama vilivyokuwa chini ya Ukawa vilitaka kwenda kuwashukuru Watanzania kwa kuwapa kura zaidi ya milioni sita.
Hata hivyo, mwanasiasa huyo anasema kitendo cha serikali ya Dk. Magufuli kupiga marufuku siyo tu kinakandamiza demokrasia, lakini pia kinawadharau Watanzania ambao wana haki ya kushiriki katika shughuli za siasa hapa nchini.
Kuzuia vyama vya siasa kufanya shughuli zao za kisiasa ikiwamo miutano ya hadhara ni ukikwaji wa Katiba ambayo, Rais Magufuli aliapa kuilinda.

MTAZAMO WAKE KWA MARAIS WALIOPITA
Dk. Medeye ambaye alikuwa Naibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika uongozi wa Rais Kikwete anasema umefika wakati kwa marais wastaafu kukaa pembeni badala ya kuendelea kung’ang’ania kutoa maelekezo kwa serikali iliyopo madarakani.
Anasema kwa bahati mbaya marais hao bado wana nguvu ndani ya CCM, kwa hiyo maelekezo yao yanapokelewa na kufanyiwa kazi hatua ambayo inakandamiza demokraisa hapa nchini pamoja na upande wa Zanzibar.
Akilinganisha awamu zote za uongozi, Dk. Medeye anasema, Rais Kikwete alikuwa mwanademokrasia lakini Mkapa alikuwa tofauti na alitamani kuona upinzani unakufa na kutoweka hapa nchini.

MPANGO WA ELIMU BURE HAPA NCHINI
Kuhusu mpango wa elimu bure hapa nchini kuanzia Chekechea hadi kidato cha nne, Dk. Medeye anasema hiyo haikuwa Ilani ya CCM katika uchaguzi uliopita mwaka jana.

Sera ya elimu bure ya mwaka 2014 ilipitishwa na serikali ya awamu nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na ikazinduliwa na yeye mwenyewe kabla hajatoka madarani na utekelezaji wake ulikuwa umepangwa uanze mwaka huu.

Anasema mtu yoyote ambaye angeingia madarakani asingekuwa na namna yoyote ya kubadili sera hiyo, na kwamba Rais Magufuli siyo wazo lake bali amekuta mipango yote ipo tayari.
Hata hivyo, anasema licha ya serikali kutangaza elimu bure, lakini utekelezaji wake bado ni mgumu kwa kuwa shule nyingi bado zinadai michango hususani zile za bweni hadi kufikia Sh. 280,000 kwa mwanafunzi mmoja kwa mwaka.
Mwanasiasa huyo anasema, Chadema ilichokuwa inataka kufanya kama ingeingia madarakani ilikuwa ni kuboresha sera hiyo badala ya elimu bure kuishia kidato cha nne isogee hadi Chuo Kikuu.
HARAKATI ZA KUGOMBEA USPIKA WA BUNGE
Mwanasiasa huyo ambaye amefanya shughuli mbalimbali ndani na nje ya nchi, anasema aligombea Uspika mwaka jana katika Bunge la 11 ili kuboresha chombo hicho na kukifanya kiwe cha kisasa.
Kwa mfano anasema wabunge hawana ofisi za kukutana na wageni wao wanapokuwa bungeni mjini Dodoma, badala yake wakipata wakitembelewa na mtu wanakutana naye katika mgahawa.

Anasema angebahatika kuwa Spika angeweka ofisi za kila mkoa ndani ya ofisi za Bunge mjini Dodoma ambayo ingetumiwa na wabunge wanaotoka mkoa husika kwa ajili ya kukutana na wageni wao badala ya kuwapeleka katika mgahawa ili kuzungumza nao.

Maboresho mengine ambayo angefanya bungeni ni kila Mbunfe anakuwa na vifaa vya kisasa zikiwamo simu za Ipad kwa ajili ya kufuatilia shughuli mbalimbali za Bunge badala ya kugawiwa makaratasi ambayo alisema ni gharama kuyaandaa.

Maeneo mengine ambayo angehakikisha yanapewa msukumo ni kuweka kanuni za kuwabana wabunge ili wahudhurie vikao kwa kuwa imefika mahali mambo nyeti zikiwezo sheria yanapitishwa na watu 30.

Dk. Medeye anasema wasaidizi wa Mbunge angehakikisha wanaajiriwa na ofisi ya Bunge ili kuleta ufanisi kwa shughuli anazotakiwa kuzifanya kwa niaba ya mwakilishi huyo.

LEO AKIKUTANA NA RAIS MAGUFULI ATAMUELEZA NINI

Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Arumeru Magharibi kwa miaka mitano kati ya 2010 hadi 2015, anasema leo hii akikutana na Rais Magufuli atamwambia ajifunze kupokea ushauri na kuuchuja na kuchukua yale mazuri na kuacha mabaya.
Anasema akikutana naye pia angemshauri kuunda wizara ya Habari na Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi, Mazingira, Maafa na Uokoaji, Utumishi, Kazi na Ajira, badala ilivyo kwa sasa.

USHAURI KWA CHAMA CHAKE CHA CHADEMA
Anasema kazi pekee iliyobaki kwa Chadema ni kukijenga chama kuelekea uchaguzi wa 2020 kuanzia ngazi ya kaya, shina, tawi, kata, jimbo hadi taifa.

Anasema changamoto kubwa inayokikabili chama hicho ni namna ya kuhakikisha kinajisimika kuanzia ngazi ya chini mijini na vijijini na kwamba hilo likifanyika uchaguzi ujao kitapata mafanikio makubwa zaidi.
MALENGO YAKE YA BAADAYE KISIASA
Anasema amestaafu ubunge katika jimbo lake na kuamua kuwachia vijana na kwamba sasa anajipanga kugombea Ubunge wa Afrika Masharika mwaka ujao.

Anasema anao uwezo na uzoefu wa kutosha katika masuala ya kimataifa na kwamba Tanzania ikimuamini na kumpa nafasi hiyo ataiwakilisha vizuri katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo alisema ina changamoto nyingi.

Anasema bado ana imani na wabunge wote wakiwamo wa CCM ambao ndiyo wapiga kura katika nafasi atakayogombea mwakani na kwamba watafanya hivyo kwa kuongozwa na Mungu.

ANAKUMBUKA NINI KAMPENI ZA MWAKA JANA
Kikubwa anachokumbuka ni namna yeye, viongozi wenzake wa Chadema na aliyekuwa mgombea urais chini ya Ukawa, Edward Lowassa walivyokuwa wakipokelewa na umati mkubwa wa wananchi.

“Kila tulipofika katika eneo la mkutano wa kampeni, shida yetu tulikuwa tunafikiria umati huu mkubwa tutapataje eneo la kuwatosha wote wakae na kutusikiliza na walikuwa wanakuja bila kulipwa fedha kama ilivyokuwa ikifanyika kwa CCM,’’ anasema
Anasema kampeni zilifanyika kwa amani na hawajawahi kupata tatizo lolote na walipata fursa ya kunadi Ilani ya Ukawa na wananchi wakaielewa vizuri.
Akizungumzia mipango ya serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli, Dk. Medeye anasema kero za Watanzania hazijaguswa hata kidogo.

Badala yake anasema serikali ya awamu ya tano imeanza kwa kuleta maafa ya ya kubomoa nyumba za wananchi wanaoishi mabondeni bila ya kuwaandalia mazingira salama ya kwenda kuishi.
Anasema serikali makini na inayojali wananchi wake inapaswa kuweka mipango ya kuwapatia wananchi hao makazi kabla ya kuanza kubomoa nyumba zao.

MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU 2015

Ili kuhakikisha Chadema kinapata matokeo sahihi na kuyalinda , kiliunda kikosi maalum kwa ajili ya kupokelea matokeo kutoka vituoni.

Anasema siku chache bada ya kufanyika uchaguzi huo, jeshi la polisi lilivamia kituo chao cha kupokelea matokeo kutoka vituo mbalimbali kwenye majimbo.
Anasema wakati kituo hicho kinavamiwa mgombea urais wa Ukawa, alikuwa anaoongoza kwa asilimia 72 na kwamba chama hicho kilikuwa na uhakika wa kushinda uchaguzi huo.

Dk. Medeye anakiri kwamba kama kituo kile kingeachwa kifanye kazi yake vizuri wangepata mapema matokeo halisi ya urais ambayo yalikuwa yanaonyesha, Lowassa alikuwa katika nafasi nzuri ya kuibuka mshindi.

SERIKALI YA MAGUFULI KUBANA MATUMIZI
Kuhusu utaratibu wa sasa wa serikali ya Rais Magufuli kudhibiti mianya ya rushwa, kuongeza mapato na kubana matumizi, Dk. Medeye anasema, serikali hii ingeacha bajeti iliyokuwa imepitishwa 2015/2016 iende kama ilivyokuwa imepangwa.

Anasema Rais Magufuli angetakiwa kuanza mipango yake kwa kutumia bajeti yake ya 2016/2017 ambayo itapitishwa mwaka huu.

Akizungumzia semina kwa Mawaziri na watendaji mbalimbali walioteuliwa hivi karibuni, Dk. Maedeye anasema walipaswa kupewa semina kwa kuwa baadhi yao hawajawahi kuwa serikalini.

Kitendo cha kuzuia semina kwa madai ya kubana matumizi kutawafanya Mawaziri washindwe kujua majukumu yao wanayopaswa kufanya ili kulisogeza taifa mbele.

SIJUTII KUHAMA CCM NA KUJIUNGA NA CHADEMA
Kada huyo wa CCM tangu enzi za chama cha Tanu, kabla ya kukitosa CCM mwaka jana anasema, hajawahi kujua kujiunga na Chadema na anajiona yupo huru kufanya mambo yake.
Anasema anaamini Rais Kikwete alikiongoza CCM vizuri na hakutoka huko kutokana na ugomvi na mtu yoyote na anamshukuru kiongozi huyo kwa kuwa mwanademokrasia.
“Sehemu aliyoharibu mwishoni mwa uongozi wake, ni pale alipokuwa amepanga mgombea wake wa urais, badala ya kuacha kazi hiyo ifanywe na vikao vya CCM,’’ anasema

Dk. Medeye anasema hakuna alichopoteza kwa kuhama CCM na kwamba bado anao moyo wa kulitumia taifa, lakini kwa ngazi ya kikanda siyo jimboni.
Mwanasia huyu ni msomi kwa ngazi ya Udaktari wa Falsafa (Phd) aliyoipata nchini Marekani na amewahi kuongoza taasisi mbalimbali za kimataifa.

Habari Kubwa