Shein azika tumaini la mwisho la Maalim Seif

13Jan 2016
Nipashe
Shein azika tumaini la mwisho la Maalim Seif

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amezika tumaini la mwisho la aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kuutangazia umma mbele ya Rais Dk. John Magufuli, kuwa uchaguzi visiwani humo utarudiwa.

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein

Kauli ya Shein imekuja siku moja baada ya juzi Maalim Seif kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kumtaka Rais Magufuli kuingilia mazungumzo yanayoendelea Zanzibar ili muafaka ufikiwe na uchaguzi usirudiwe bali mchakato wa kuhesabu kura ukamilishwe na mshindi kutangazwa.
Hatua hiyo ya Maalim Seif ilionyesha hana imani na viongozi anaoendelea na mazungumzo nao na badala yake, alimuomba Rais Magufuli kuingilia kati ili hatua ya uchaguzi wa marudio isije ikafikiwa kwa kuwa haitaleta amani bali vurugu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Shein alisema uchaguzi uko chini ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakisubiri tume hiyo itangaze tarehe ya marudio.

Dk. Shein ambaye ni Mwenyekiti wa mazungumzo ya kutafuta suluhu yanayoendelea visiwani humu, alitoa kauli hiyo pia mbele ya Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Balozi Seif Idd Ali, ambao pia ni wajumbe wa mazungumzo hayo, huku Maalim Seif akihudhuria peke yake kama kiongozi wa upinzani.

Mbali na viongozi hao, Dk. Shein alitoa pia kauli hiyo mbele ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Hata hivyo, alisema mazungumzo ya kutafuta muafaka yanaendelea na yanashirikisha viongozi sita, wakiwamo waliopo madarakani na wengine wastaafu.

Juzi, Maalim Seif alisema ana imani na Rais Magufuli katika kutatua mgogoro huo kwa kuwa aliwahi kufanya naye mazungumzo na kumueleza kwamba ahakikishe amani na utulivu vinapatikana visiwani Zanzibar.

Kama tafsiri ya Dk. Shein ya kutoa msimamo wa kurudiwa kwa uchaguzi mbele ya Rais Magufuli, inaaminisha kwamba kiongozi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti mtarajiwa wa CCM, anaungana nayo, Maalim Seif atakuwa amebaki na tumaini moja tu.

Tumaini hilo ni vikao vya juu vya CUF kama ambavyo juzi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa endapo Zec itatangaza tarehe ya uchaguzi, itabidi arudi kwenye vikao hivyo ili kupata kauli ya mwisho.

Mbali na kurudiwa kwa uchaguzi, Dk. Shein alisema
mafanikio ya serikali ya awamu saba yametokana na ushirikiano baina ya wananchi na viongozi huku akimtaja Maalim Seif, Makamu wake wa Kwanza wa Rais kuwa ni kati ya viongozi wanaomsaidia na kushirikiana katika kuwahudumia wananchi.

“Suala la utii wa sheria na Katiba ya Zanzibar, halina mjadala ni la kila mmoja wetu, huku tukiyaenzi Mapinduzi haya kwani ndiyo yametufikisha hapa tulipo kwa kuwaenzi waliotuunganisha, hayati Karume na Mwalimu Nyerere, nasi tuendeleze amani, utulivu na mshikamano baina yetu,” alisema Dk. Shein.

Alisema katika serikali yake, uchumi umeendelea kukua ikiwamo pato la taifa kwa asilimia saba huku pato la mtu mmoja mmoja likikua kwa Sh. milioni 1.5 kwa mwaka 2014.

Pamoja na Dk. Shein kuzika matumaini ya uchaguzi, Maalim Seif katika mkutano wake juzi alisema hakuna hoja ya msingi ya kikatiba na kisheria ya uchaguzi kurudiwa na kwamba kurudiwa kwa uchaguzi kunaweza kuleta maafa makubwa kama yale yaliyotokea mwaka 2001 na kuonya wanachama wa CCM kuwa waangalifu.

Mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar uliibuka Oktoba 28, mwaka jana, baada ya Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo kwa madai ya kuwapo kwa dosari nyingi, jambo lililosababisha kukwama kuundwa kwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kinyume cha kifungu cha 90(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Akizungumzia hali ya ustawi wa jamii na kiuchumi katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi, Rais Shein alisema kumekuwapo na mafanikio makubwa katika huduma muhimu za jamii ikiwamo ya maji, afya elimu pamoja na uimarishaji wa barabara za kiwango cha lami katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema ukuaji wa uchumi wa Zanzibar umekua na kufikia asilimia 7.0 kutoka 6.1 mwaka 2015, huku pato la mwananchi wa kawaida likiongezeka kutoka Sh. milioni 1.3 hadi Sh. milioni 1.5 sawa na asilimia 12 tofauti na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya ukuaji kufikia Sh. 884,000 kwa mwaka 2010/2015.

Hata hivyo, alisema mfumko wa bei umendelea kujitokeza Zanzibar na kufikia asilimia 5.7, ndiyo maana serikali imeamua kupunguza ushuru wa bidhaa muhimu zinazoingizwa nchini kuwasaidia wakulima kwa kupata pembejeo kwa bei nafuu visiwani humu.

Dk. Shein alisema serikali imeongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha miezi sita na kwamba mapato ya ndani yalifikia Sh. bilioni 188.4 kutoka Sh. bilioni 172.5 mwaka 2014.

Imeandaliwa na Mwinyi Saddallah, Zanzibar na Christina Mwakangale, Dar

Habari Kubwa