Simba, Azam kukinukisha leo

20Jan 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Simba, Azam kukinukisha leo
  • *** Ligi hiyo iliyoanzishwa 1965, leo inaingia katika raundi ya 15 ikihitimisha mzunguko wa kwanza msimu huu.

KOCHA mkuu wa muda, Jackson Mayanja leo jioni atasaka ushindi wake wa pili katika mechi yake ya pili wakati Simba itakapoikabili JKT Ruvu iliyopoteza 5-1 nyumbani dhidi ya Mgambo Shooting mwishoni mwa wiki.

Wachezaji wa Azam FC

Mechi hiyo ya raundi ya 15 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni sawa na mechi nyingine nne za leo kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ulioanza Septemba 12.
Baada ya kutoka sare katika mechi tatu mfululizo dhidi ya Azam FC, Toto Africans na Mwadui FC, Simba imeshinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Ndanda na Mtibwa na kurejesha matumaini ya kukata kiu ya taji la Ligi Kuu waliyonayo kwa msimu wa nne sasa.
Rekodi mbaya za JKT Ruvu iliyofunga mabao 16 na kufungwa 25 msimu huu huku ikiambulia pointi nne katika mechi tatu zilizopita dhidi ya Coastal Union, Ndanda na Mgambo zinaibeba Simba kufanya vizuri leo.
Kikosi cha JKT Ruvu kinachonolewa na nyota wa zamani wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni, kitaingia kwenye Uwanja wa Taifa kikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara katika mechi zote mbili za VPL msimu uliopita.
Ushindi katika mechi ya leo utaifanya Simba ambayo imefunga magoli 21 na kuruhusu tisa katika mechi 14 zilizopita na kukaa kwenye nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi, iwe na pointi tatu nyuma ya vinara Yanga ambao hata hivyo, kesho wataikaribisha Majimaji iliyoambulia pointi moja katika mechi tano zilizopita.
Lakini, Wanamsimbazi wanapaswa kuwaombea njaa Azam FC, ambao jioni watakuwa na kibarua kigumu kupata ushindi au sare dhidi ya Mgambo jijini Tanga ili kuing'oa Yanga kileleni na kulinda rekodi yao ya kutopoteza mechi katika mzunguko wa kwanza.
Kikosi cha Muingereza Stewart Hall kinachoendelea kukosa huduma beki wa kati Aggrey Morris kutokana na majeraha ya goti, kitaingia uwanjani leo kikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya kwanza kwenye uwanja wake wa nyumbani na ya tatu msimu huu kiliposhikwa 1-1 dhidi ya African Sports Jumamosi usiku.
Hata hivyo, Wanalambalamba wataingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri kuliko timu nyingine yoyote kwa kushinda mechi zote za mikoani. Wamechukua pointi 12 ugenini hadi sasa kwa kuzichapa Stand United (2-0) na Mwadui (1-0) zote Shinyanga, kabla ya kuzinyuka Ndanda (1-0) mkoani Mtwara na Majimaji (2-1) mjini Songea.
Ndanda ambayo ilipoteza 1-0 dhidi ya Yanga Jumapili, itawakabili Mbeya City ambao watakosa huduma ya kiungo mzoefu Haruna Moshi 'Boban' aliyetolewa kwa kadi ya pili ya njano wakati wa mechi yao ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui FC mjini Mbeya Jumamosi.
Kikitoka na ushindi wa 1-0 ugenini jijini Mwanza dhidi ya Toto Africans Jumamosi, kikosi cha Salum Mayanga cha Tanzania Prisons kitasaka pointi tatu nyingine leo kitakaposhuka kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kuchuana na mabingwa wa 1988 wa ligi hiyo, Coastal Union.
Uhondo wa VPL pia utakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga pale kikosi cha Mfaransa Patrick Liewig kilichoshinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi, kitakapowakaribisha 'Wanakishamapanda', Toto Africans.

Habari Kubwa