Simba sasa inachapa tu

22Jan 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe
Simba sasa inachapa tu
  • *** Wachezaji watatu walioneshwa kadi nyekundu katika mechi tano za jana wakati Azam ikiing'oa tena Yanga kileleni ...

BAADA ya kuambulia sare katika mechi tatu mfululizo dhidi ya Azam, Toto na Mwadui, Simba sasa inaonekana kurejea kwenye makali yake ya kutembeza vichapo baada ya jana kupata ushindi wake wa tatu mfululizo, ilipoichapa JKT Ruvu mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 33 katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mechi 15, lakini inaendelea kuwa nyuma kwa pointi sita dhidi ya vinara Azam FC na tatu nyuma ya Yanga wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na mechi moja mkononi.
Simba, mabingwa mara 18 wa Tanzania Bara, walipata goli lao la kwanza jana kupitia kwa straika wao Mganda Hamisi Kiiza aliyetupia bao lake la 10 kwa tuta lililotolewa na mwamuzi Martin Saanya katika dakika ya 53 baada ya beki wa JKT Ruvu, Sesil Efrem kumkwatua Danny Lyanga.
Ilikuwa penalti ya kwanza kwa timu hiyo ya Msimbazi msimu huu baada ya mechi 15. Pia hakuna penalti hata moja iliyotolewa dhidi ya timu hiyo tangu kuanza kwa msimu huu Septemba 12.
Dakika 10 baadaye, Lyanga alifunga bao la pili akiuwahi mpira mrefu uliopigwa na kipa Vincent Agban na kumpiga chenga kipa wa JKT Ruvu, Hamisi Seif kabla ya kukwamishwa wavuni kwa shuti mtoto la mguu wa kulia lililoandikisha goli lake la pili msimu huu.
Mchezaji huyo wa zamani wa Coastal Union na FC Lupopo ya DR Congo, alifunga goli lake la kwanza tangu ajiunge na Simba dirisha dogo katika mechi yao ya sare ya 1-1 dhidi ya Toto Africans jijini Mwanza Desemba 19.
Kikosi cha JKT Ruvu kinachonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Ashanti United na Kagera Sugar, Abdallah 'King' Kibadeni, kilionekana kukosa mbinu za kuifunga timu hiyo ya Msimbazi kwani kilipiga shuti moja tu lililolenga lango katika dakika zote 90 za mchezo huo wa kufunga mzunguko wa kwanza kwa timu zote.

NDANDA 4-1 MBEYA CITY
Kama walivyouanza msimu uliopita kwa kifunga Stand United mabao 4-1 nyumbani mjini Shinyanga Agosti 24 mwaka juzi, Ndanda FC walikuwa moto mkali jana baada ya kuipa kipigo kama hicho timu inayonolewa na kocha wao wa zamani Abdul Mingange, Mbeya City.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, mabao ya wenyeji yalifungwa na kinara wa magoli katika timu hiyo, Atupele Green aliyetupia katika dakika ya 11 na 76 pamoja na Omary Mgunda aliyetikisa nyavu dakika za 18 na 28.
Goli pekee la City waliolazimika kubaki 10 uwanjani baada ya beki wa usajili wa dirisha dogo Haruna Shamte kulimwa kadi nyekundu (kadi ya pili ya njano) katika dakika ya 78, lilifungwa na kiungo fundi Joseph Mahundi dakika tatu baada ya saa ya mchezo.
Mbeya City iliingia uwanjani jana bila kiungo wake mzoefu, Haruna Moshi 'Boban' ambaye pia alilimwa kadi nyekundu katika mechi yao ya Jumamosi waliyoshinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC nyumbani mjini Mbeya.

MGAMBO 1-2 AZAM
Bolly Shaibu ambaye alikuwa miongoni mwa wafungaji katika ushindi wao wa 5-1 dhidi ya JKT Ruvu jijini Dar es Salaam Jumamosi, alifunga goli la Mgambo dakika moja baada ya robo saa ya mchezo, lakini beki wa pembeni kulia Shomari Kapombe alifunga mara mbili ndani ya dakika 14 akiitendea haki kazi nzuri ya nahodha John Bocco 'Adebayor' na kuipa Azam FC ushindi wa 12 msimu huu.
Kapombe, beki wa zamani wa Simba, alifunga goli la kwanza la Wanalambalamba katika dakika ya 22 akiuzamisha wavuni mpira uliotemwa na kipa kutokana na shuti kali la mguu wa kulia la Bocco aliyekuwa nje ya boksi.
Mkali huyo wa mabao alizitikisa tena nyavu za maafande hao na kufunga goli la saba kwake msimu huu dakika sita baada ya nusu saa ya mchezo, safari hii akifumua shuti la mguu wa kushoto baada ya kupewa pasi yenye macho ndani ya boksi na Bocco.

STAND 2-1 TOTO
Kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, wenyeji Stand United walifanikiwa kuing'oa Mtibwa Sugar katika nafasi ya nne ya msimamo wa ligi baada ya kupata ushinda wa mabao 2-1 dhidi ya Toto Africans ya Mwanza.
Mabao ya kikosi cha Mfaransa Patrick Liewig yalifungwa na Vitalis Mayanga na Seleman Kassim, maarufu Selembe wakati goli la kufutia machozi la Toto likipachika kwa shuti la faulo ya mguu wa kushoto na Maka Miraj dakika nane kabla ya kipenga cha mwisho cha refa Amaan Simba.
Katika mechi hiyo ya kufunga mzunguko wa kwanza, timu zote zililazimika kubaki na wachezaji 10 uwanjani kipindi cha pili kutokana na nyota wake kulimwa kadi nyekundu na refa huyo kutoka mkoani Kagera.

PRISONS 2-1 COASTAL
Katika mechi nyingine ya jana, Tanzania Prisons iliutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kushinda 2-1 dhidi ya mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union.
Magoli wa Prisons yalifungwa ma Jeremia Juma dakika ya 61 na Mohamed Mkopi dakika nane kabla ya kipenga cha mwisho, wakati wageni walifutwa machozi na Ntenje Juma dakika moja baada ya robo saa ya tatu ya mchezo.

*** Imeandikwa na Juma Mohamed (Mtwara), Somoe Ng'itu na Sanula Athanas (Dar).

Habari Kubwa