Simba yalipa kisasa, yaituliza Mtibwa

17Jan 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Simba yalipa kisasa, yaituliza Mtibwa
  • ***Ni mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye uwanja wa Taifa. Leo ni zamu ya mabingwa watetezi Yanga dhidi ya Ndanda FC.

SIMBA ilitumia dakika tano tu kutikisha kamba za Mtibwa Sugar na kupata ushindi mgumu wa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, shukrani kwa mshambuliaji Hamis Kiiza aliyekuwa shujaa wa pointi tatu walizopata Wekundu hao wa Msimbazi.

Wachezaji wa Simba

Ushindi huo wa Simba ni wa kwanza tangu Ligi Kuu tangu walipomtimuwa Kocha Dylan Kerr na nafasi yake kuchukuliwa na Jackson Mayanja, ambaye ameanza vizuri kurithi mikoba ya Kerr.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 30 baada ya mechi 14, ikiendelea kubaki nafasi ya tatu kwenye msimamo, huku Mtibwa wakibaki nafasi ya nne wakiwa na pointi 27.
Mechi hiyo ya raundi ya 14 ya Ligi Kuu Tanzania Bara ilizikutanisha timu hizo kwa mara ya pili ndani ya mwezi huu, kwani Januari 10 Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya kikosi cha Mecky Mexime na kukatisha ndoto za Wanamsimbazi kutwaa taji la nne la michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalika katikati ya wiki hii mjini Zanzibar.
Iliwachukua Simba dakika tano tu tangu kuanza kwa kipindi cha kwanza kufunga bao kupitia Kiiza aliyeusukumia nyavuni mpira kwa kichwa akimalizia krosi iliyopigwa na Mohamed Tshabalala.
Lilikuwa ba la tisa kwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Simba kutoka Uganda tangu ajiunge na wavaa jezi hao nyekundu na nyeupe akitoka Jangwani, hivyo kumfikia mshambuliaji wa Elius Maguli.
Katika mchezo huo uliojaa kila aina ya ushindani, Simba wakifumua mashuti matatu yaliyolenga lango dhidi ya moja kwa Mtibwa, huku kila upande ukipata kona tano.
Vijana wa Mtibwa wangeweza kupata bao kupitia kwa Shiza Kichuya aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, lakini akapiga shuti 'cha mtoto' na kuishia mikononi mwa kipa Agban Vincent.
Simba ilipoteza nafasi nyingine ya kufunga kupitia kwa Kiiza baada ya Mganda huyo kupiga shuti juu na kupoteza kazi nzuri iliyofanywa na Peter Mwalyanzi.
Beki wa pembeni wa Mtibwa, Issa Rashid 'Baba ubaya' nusura aitungue Simba na kufanya matokeo kuwa 1-1 kama siyo shuti lake kugonga 'paa' na mpira kurudi uwanjani kabla ya kuokolewa na Juuko Murshid.
Walikuwa Simba tena waliopoteza nafasi ya kufunga baada ya shuti la Kiiza kukosa shabaha na kutoka pembeni ya lango la Mtibwa kufuatia pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto.
Katika matokeo mengine, Majimaji ya Songea na Coastal Union ya Tanga, zilimaliza dakika 90 na kufungana bao 1-1, huku Mgambo JKT ikifanya sherehe ya mabao baada ya kuinyonyoa JKT Ruvu mabao 5-1, Stand United wakiichapa Kagera Sugar bao 1-0
Ligi hiyo inaendelea tena leo kwenye Uwanja wa Taifa kwa mabingwa watetezi Yanga kucheza na Ndanda FC.
Yanga wako nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma Azam FC yenye pointi 35, ambayo ilitarajia kucheza mechi jana usiku dhidi ya African Sports.
kati
Vikosi vilikuwa: Simba: Vincent Agban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Hassan Isihaka , Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Ibrąhim Ajib/ Danny Lyanga (64) na Peter Mwalyanzi/ Said Ndemla (dk 31).

Mtibwa Sjgar: Said Mohammed, aally Shomary, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Salim Mbonde, Henry Joseph, Shabani Nditi, Shiza Kichuya, Mjzamil Yassin, Hussein Javu /Jaffar Salum ( dk 50), Ibrahim Rajab ' Jeba' na Mohammed Ibrahim/ Vincent Barnabas ( dk 64).

Habari Kubwa