Simba yasubiri kukata mtu Moro

23Jan 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Simba yasubiri kukata mtu Moro
  • Mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara, leo wanaanza rasmi kusaka tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

SIMBA imeshinda mechi zote mbili zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu tangu imtimue kocha mkuu Dylan Kerr na leo imepanga 'kuikata' Burkina Faso katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

kocha wa Simba Jackson Mayanja.

Michuano hiyo ni ya mtoano na mshindi baada ya mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam, atasonga mbele kusaka timu bingwa ambayo itaiwakilisha Tanzania Bara kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

Jackson Mayanja, kocha wa muda wa Simba, alisema kikosi chake kimo mjini Morogoro tangu jana mchana kwa kasi moja tu ya kushinda na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Mayanja alisema ametinga mkoani humo akiwa na nyota wake wote wa kikosi cha kwanza na kuwataja majeruhi waliobaki jijini kuwa ni Raphael Kiongera, Brian Majegwa na Mohammed Fakhi.

“Ninajua mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu timu ndogo huwa zinajiandaa kukamia klabu kubwa, ninalitambua hilo, ninahitaji kushinda mechi hiyo ya tatu tangu nijiunge na Simba na ya kwanza kwangu kuiongoza timu hii tukicheza ugenini,” alisema.

Mganda huyo aliongeza kuwa kila mechi kwake ni fainali na kwa kutambua hilo, amewaandaa wachezaji wake kuhakikisha wanashinda mechi ya leo.

Mechi nyingine zinazotarajiwa kuchezwa leo katika mashindano hayo yaliyorejeshwa tena nchini ni kati ya ndugu wa wawili wa jiji la Mwanza, Pamba na Toto Africans kwenye Uwanja wa Kirumba wakati
Ndanda FC itawakaribisha Mshikamno kwenye Uwanja wa Nagwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Bara Yanga kuchuana na Friends Rangers ya Magomeni kwenye Uwanja Taifa huku Njombe Mji wakiwakabili Prisons wakati Stand United watavaana na Mwadui mkoani Shinyanga.

Habari Kubwa