Simbachawene aagiza kuhojiwa Mkurugenzi Dodoma

23Jan 2016
Nipashe
Simbachawene aagiza kuhojiwa Mkurugenzi Dodoma

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa, George Simbachawene amemuagiza Kaimu katibu mkuu Tamisemi, Bernadi Makali kumuweka kwenye kiti moto Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa, George Simbachawene.

Simbachawene ametaka Mkurugenzi Mtendaji huyo ahojiwe juu ya barua iliyoandikwa na Ofisa Elimu Msingi kwenda katika shule mbalimbali,
ikiwataka wazazi kuchangia michango ya elimu kinyume na waraka wa serikali.
Waziri huyo alitoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara ya kushitukiza kwenye Shule ya Msingi Dodoma Makulu, ambayo wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo juzi waliitishwa kikao na kamati ya shule hiyo wakitakiwa kuchangia vitu mbalimbali.

Wazazi hao walitakiwa kuchangia fedha ya mlinzi, umeme na maji, vitu ambavyo tayari fedha zake zimeshatolewa na serikali katika mwezi huu wa Januari.

Waziri huyo aliitembelea shule hiyo ili kujiridhisha na kuona namna fedha za elimu bure zinavyotumika. Akiwa shuleni hapo, Waziri Simbachawene alikutana na mwalimu mkuu Janeth Justine na kumuhoji juu ya matumizi ya fedha hizo na namna ambavyo ameanza kuzitumia kama waraka wa serikali unavyoelekeza.

Mwalimu mkuu huyo alisema kuwa jumla ya fedha walizopokea ni Sh. 1,052,000 kwa wanafunzi 1400 kuanzia darasa la awali wanaosoma shuleni hapo.

“Fedha zote hizi mmeshazipokea na zingine bado hata hamjazigusa lakini leo wazazi wanalalamika mnataka wachangie hela za mlinzi, umeme, maji wakati serikali hivyo vyote imeshavilipia,” alisema Simbachawene.

Akitolea ufafanuzi, mwalimu huyo alisema yeye aliletewa mwongozo pamoja na barua inayoonyesha kuwa anaweza kuchangisha michango mbalimbali kwa wazazi kupitia barua hiyo. “Mimi waraka nimeusoma vizuri lakini kuna barua ililetwa, ilitoka kwa Ofisa Elimu wa Manispaa kwa shule za msingi ikitoa maelekezo kuwa tunaweza kuendelea kuchangisha michango,” alisema mwalimu Justine.

“Ndipo jana tukawaita wazazi na kuwaeleza lakini walikataa na kusema hawako tayari kuchangia. “Mimi sikuhusika na kikao hicho. Ni Diwani ndiye aliyekuwa akisimamia pamoja na kamati ya shule.”

Baada ya maelezo hayo Waziri alitoa maagizo kwa mwalimu kuacha kuchangisha mchango wowote na pia kumwagiza Kaimu Katibu Mkuu wa Tamisemi kumwita mkurugenzi pamoja na ofisa elimu aliyeandika barua hiyo.

“Serikali hii imeamua kutoa elimu bure lakini sasa hawa watumishi wetu ambao wanakwenda kinyume na maagizo ya serikali wanatupa lawama kwa wananchi wetu,” alisema Simbachawene. “Waitwe na wahojiwe na baadaye nitatoa maamuzi kwa kile walichofanya.” Awali akitolea ufafanuzi wa fedha hizo za elimu bure kwa waandishi wa habari, Waziri alisema kuwa kiasi kilichotolewa ni cha mwezi mmoja hivyo walimu wanatakiwa kuzitumia kama muongozo unavyoelekeza.

“Malipo haya yataendelea kulipwa kila mwezi na fedha hizi zisitumike vibaya katika kulipa madeni ya nyuma, bali zitumike katika vipaumbele vya shule na kutatua changamoto nyeti za kielimu na walimu wakuu wasiingilie utaratibu huo.”

Habari Kubwa