Siri ya wasichana waliong’ara kitaifa mtihani darasa la nne

26Jan 2016
Nipashe
Siri ya wasichana waliong’ara kitaifa mtihani darasa la nne

HISTORIA yaonyesha kuwa kwa miaka mingi nchini katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania ukiwamo mkoa wa Kagera, kumekuwa na dhana kuwa watoto wa kike hawastahili kupewa elimu sawa na watoto wa kiume na kwamba dhamana pekee inayowastahili ni kuolewa na kuwa mama wa nyumbani.

Hata hivyo,kwa kadri wasichana wanavyopewa fursa na kufanya vizuri katika mitihani hiyo, taratibu dhana hiyo potofu imekuwa ikibadilika.
Kufuatia matokeo ya mtihani huo, wanafunzi watatu wasichana katika kumi bora kitaifa, wametoka shule iitwayo Kaizirege Boarding Nursery, Primary, Secondary and High School.ya mkoani Kagera

Wanafunzi wanasemaje?

Ayam Babiha (12) ni miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa katika mtihani wa darasa la nne,uliofanyika mwaka jana.
Anasema hakutarajia kupata ushindi wa kiasi hicho, ingawa alijitahidi kusoma kwa bidii ili apate matokeo mazuri.
Ayam ni mzaliwa wa eneo la Nshamba wilayani Muleba mkoani Kagera, anasema kuwa alipokuwa anaenda likizo, baba yake alimsisitiza na kumhakikishia kuwa, endapo atafanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la nne, atampa zawadi ambayo hata hivyo hakumfichulia.

“Ahadi ya baba yangu kwamba atanipa zawadi nzuri ambayo alisema itakuwa ‘surprise’ niliongeza bidii ili kuhakikisha kuwa nafanya vizuri...hakika nimefurahi sana wakati mwalimu mkuu wa shule aliponiita na kunipa taarifa hizi,” anasema.
Ayam ni mtoto wa mwisho katika familia yao yenye watoto watano.
Anasema kuwa anapenda zaidi masomo ya Sayansi, Hisabati, Kiingereza na Kiswahili, hivyo walimu wanapofundisha anayaelewa vizuri zaidi.
“Nikimaliza masomo yangu nataka kuwa daktari ili nishirikiane na wengine wanaofanya kazi hiyo kuokoa maisha ya watu. Lengo langu ni kufanya kazi kwa uadilifu na mafanikio makubwa kama Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Nyerere,” anasema.
Mwanafunzi mwingine aliyeingia kumi bora kitaifa ni Beatrice Novertus (11)amezaliwa Kayanga, wilayani Karagwe mkoani humo.
Anasema kuwa amejisikia mwenye furaha kubwa kwa kushinda vizuri mtihani huo.
Ushindi huo, anasema aliutarajia kwa sababu amekuwa akisoma kwa bidii ili kuhakikisha kuwa anafanya vizuri na ndivyo ilivyotokea.
Beatrice anapenda sana masomo ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi, ambayo aliyafanyia maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza mtihani huo.
Anawataka wanafunzi wenzake wasipoteze muda wa kusoma kwa kufanya masuala mengine yatakayosababisha kuwashusha kitaaluma na kuvuruga safari yao ya kielimu.
“Nyumbani tumezaliwa watoto wa nne. Mimi ni mtoto wa kwanza na natamani kuwa daktari. Inabidi nisome kwa bidii kuhakikisha kuwa nafanya vizuri zaidi. Siko tayari kupoteza hata dakika moja.Nitakapofanikiwa nitawasidia wazazi na wadogo zangu,” anasema.
Anawashauri wanafunzi wenzake watumie hata muda wa likizo kujisomea madaftari na vitabu ili kuongeza maarifa, yatakayowawezesha kufanya vizuri katika mitihani yao.
Mwanafunzi mwingine Ashura Seif (11) ni mzaliwa wa Nkwenda,Karagwe, anasema alifurahi sana baada ya kupata taarifa ya ushindi kwa sababu, alisoma kwa bidii lakini hakutarajia kushinda kwa kiwango hicho.
“Siku ya mtihani nilisoma maswali kwa uangalifu na kuyajibu yote kulingana na nilivyoelewa. Hata lile nililohisi kuwa nina mashaka na jibu lake sikuliacha nilijibu. Nimeshangaa sana kufahamishwa kuwa, mimi ni miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa… kumbe ukisoma kwa bidii hakuna kinachoshindikana,” anasema.
Ashura ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto wa nne wa familia yao, anasema anapenda sana masomo ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi.Kama ilivyo kwa wenzake.
“Nawashauri wasichana wasiogope kusoma masomo ya sayansi sio magumu sana endapo watasoma kwa bidii. Pia wazazi waongeze msukumo wa kuwasomesha watoto wa kike,” anasema.
Eulogius Katiti ni meneja mkuu wa shule ya Kaizirege iliyoko katika manispaa ya Bukoba, anasema, ingawa walifahamu wamewaandaa vizuri wanafunzi wao, waliyapokea matokeo hayo kwa furaha hasa ikizingatiwa kuwa sasa hivi elimu ni ushindani mkubwa.
“Tunapoingia kwenye mfumo huu mpya, ambao darasa la nne nao wanaingizwa katika utaratibu wa kutoa matokeo kitaifa, lazima ufurahi sana kuingia katika kumi bora. Ushindani ni mkubwa tofauti na tulivyozoea ushindani wa kiwilaya,” anasema Katiti.
Anasema kuwa katika matokeo hayo ya darasa la nne, waliofanya mtihani katika shule hiyo ni 87 wakiwamo wa wasichana 47 na wa kiume 40. Wanafunzi watano kati ya hao ndiyo wamepata daraja “B” na waliosalia wote 82 walipata daraja “A”.
Meneja huyo anasema, wameweza kufikia hatua hiyo kutokana na jitihada mbalimbali ikiwamo kuhakikisha wanakuwapo walimu wa kutosha, vitendea kazi vya kisasa na shule zao zote ni za bweni.
“Kuna utaratibu wa mashindano ya kitaaluma. Tunashindanisha madarasa kwa madarasa, mikondo kwa mikondo na wanafunzi wanaofanya vizuri tunawapa zawadi. Kwa hiyo, wanaokosa zawadi huwa wanajitahidi kusoma, ili awamu inayofuata nao wafanye vizuri na kupata zawadi,” anasema.
Anasema wanajitahidi madarasa yao kuwa na watoto wachache ili iwe rahisi kwa walimu kuwafikia, na kuwa kadirio la juu kila darasa halipaswi kuzidi watoto 35.

.
“Nalishukuru sana Baraza la Mitihani Tanzania kubadilisha utoaji wa matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la nne na kuyaweka kitaifa tofauti na zamani. Hii itatuwezesha kuona shule nyingine zinafanyaje maana tulikuwa tumefungiwa katika wilaya,” anasema.
Akizungumia jamii kutoona umuhimu wa kuwasomesha watoto wa kike, anasema jambo hilo lilikuwapo tangu zamani, lakini shule yao sasa inajaribu kupambana nalo.
“Tunahamasisha watoto wa kike wasome kwa bidii ili waweze kuwa na ushindani dhidi ya watoto wa kiume kitaaluma. Mfano katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2014, kati ya wanafunzi kumi bora kitaifa, tulipata mwanafunzi mmoja tena wa kike,” anasema.

Anasema matokeo hayo yanadhihirisha kuwa shule hiyo inawaandaa vizuri watoto wa kike, ili nao washindane na watoto wa kiume kushika nafasi za juu kitaifa kama watoto wa kiume, na kuwa wanaiomba jamii kuunga mkono jitihada hizo kwa kuwapeleka shule kwa wingi watoto wa kike.
Kuhusu serikali kutoa ada elekezi anasema walikwishapokea mwongozo kutoka serikalini na kusisitiza kuwa, watu hawakuyaelewa vizuri maelekezo ya serikali ndiyo maana yakawapo malalamiko.

“Serikali haikuwa na maana kwamba lazima watozwe kile kiwango ambacho kimependekezwa.Serikali imesema ikiwa shule inatoza zaidi ya kiasi kinachoelekezwa, wahusika wanapaswa kuiandikia kuwa wanatoza kiasi fulani kwa sababu ya vitu vya ziada vilivyoko katika shule husika,” anasema.

Shule ya msingi Kaizirege yenye wanafunzi 500, katika matokeo hayo ya mtihani wa darasa la nne uliofanyika mwaka 2015, imekuwa ya kwanza kiwilaya, ya pili kimkoa na ya tisa kitaifa.
Baraza la Mitihani la Tanzania limeanza kuendesha upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) kuanzia mwaka 2015.Upimaji huu ulifanyika tarehe 25 na 26 Novemba, 2015, uliendeshwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu zote za uendeshaji wa upimaji wa kitaifa.
Lengo la Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) ni kutoa tathmini endelevu ya mwanafunzi inayoweza kubaini umahiri wa juu wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Mitihani la Taifa, wanafunzi 1,037,305 walisajiriwa kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne(SFNA).
Takwimu za matokeo ya upimaji huu zinaonesha kuwa jumla ya wanafunzi 869,057 kati ya wanafunzi 977,886 sawa na asilimia 88.87 waliofanya upimaji huu wameweza kupata alama zenye madaraja ya ufaulu wa A,B,C na D.Wanafunzi
108,829 sawa na asilimia 11.13 wamepata alama za daraja E lenye ufaulu usioridhisha.

Habari Kubwa