Somo la Samatta kama baba angemsubiri Messi kwenye ngazi

13Jan 2016
Lete Raha
Somo la Samatta kama baba angemsubiri Messi kwenye ngazi

LIONEL Messi juzi usiku alishinda tuzo yake ya tano ya Mwanasoka Bora wa Dunia.

Kwa kuwa ni mara ya tano, inawezekana kwamba ameshaizoea mno na si kitu kigeni tena kwake kuweza kuwa 'dili' kubwa sana kwenye klabu yake ya Barcelona, ama nchini mwao Argentina.
Lakini bado nyota huyo hawezi kupata mapokezi ambayo hayajapangwa kama ilivyotokea kwa Mtanzania Mbwana Samatta aliporejea akitokea kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani ya bara hili.
Alirejea saa usiku wa manane ili kuwahi ndege ya 'bure' ya Caf na wazazi wake walikaa kwenye ngazi za nje ya uwanja wa ndege wakiumwa na mbu kumsubiri kijana wao ambaye kwa juhudi zake binafsi ameliletea taifa heshima.
Pengine Samatta ameipata tuzo hiyo katika kipindi kigumu kwa nchi ambayo chini rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, kuna vita kubwa inafanyika ya kuziba mianya ya mafisadi waliokuwa wakiyavuta nyuma maendeleo ya taifa.
Ilikuwa ni kipindi kibaya kwa Samatta kuitwaa tuzo hiyo sasa wakati ambao kusafiri kwa kiongozi ni lazima ruhusa itoke juu kabisa kwa Katibu Mkuu Kiongozi au kwa Rais mwenyewe.
Kwa mazingira hayo, ilikuwa ni jambo lisilotarajiwa kwa Samatta kupelekewa ndege ya rais imfuate kutokea Nigeria ilikofanyika hafla ya tuzo hizo kama ilivyotokea kwa mshindi wa tuzo kuu ya Mwanasoka Bora wa Afrika, Pierre-Americ Aubameyang wa Gabon.
Samatta ameshinda tuzo ya Afrika kwa juhudi zake binafsi, sawa. Hakupata mapokezi mazuri, sawa. Lakini haitakuwa sawa kama serikali itakaa kimya bila kumfanyia Samatta jambo kubwa kwa manufaa yake na vizazi vijavyo na kutengeneza mazingira ya kuwatoa kina Samatta wengine.
Kuwatengeneza kina Samatta wengine ni pamoja na kuhakikisha maeneo ya wazi yaliyovamiwa na mafisadi yanarudishwa kuwa kama zamani.
Serikali inatia mkono wake katika kusaidia kuboresha maeneo ya wazi ili yawe viwanja kwa ajili ya kuwapa vijana wadogo fursa ya kujihusisha na michezo.
Pia Serikali ihakikishe inashusha kodi ya kuingiza vifaa vya michezo ili kuwawezesha wazazi wa vijana kuwa na uwezo wa kuwanunulia watoto wao 'njumu' na jezi ili wasicheze mpira pekupeku.
Siku za nyuma kidogo katika maeneo ya miji mikubwa kama ya Dar es Salaam, vijana baada ya kunyang'anywa maeneo yao ya wazi, kutokana na kupenda michezo walithubutu kucheza soka japo kwenye barabara za pembeni ya mji kwa kusubiri gari moja lipite na mechi iendelee. Lakini jambo hilo la hatari haliwezekani tena sasa kutokana na wingi wa magari. Ni lazima michezo ifanyike kwenye maeneo rasmi, kwa sababu michezo ni sekta rasmi inayowapa utajiri mkubwa vijana duniani.
Kukosa mapokezi kwa Samatta ni uthibitisho kuwa bado michezo haipewi umuhimu unaostahili, na yanayofanyika mbele za kamera ni kwa ajili ya kujikosha tu kutokana na presha za wananchi katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Ni kwa sababu wenzetu wanajua michezo ni gemu ya mabilioni ya pesa, ndiyo maana hutasikia baba yake Messi anaisubiri tuzo ya mwanaye kwa kung'atwa na mbu kwenye ngazi za uwanja wa ndege.