Sumaye: Nimeshtushwa kutembelewa na Magufuli

12Jan 2016
Nipashe
Sumaye: Nimeshtushwa kutembelewa na Magufuli

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amemmshukuru Rais Dk. John Magufuli, kwa kumtembelea na kumjulia hali katika Hospitali ya Taasisi ya Jakaya Kikwete, alipolazwa kwa matibabu.

Rais Magufuli akizungumza na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye

Akizungumza baada ya kutembelewa na Rais, Sumaye alisema alishtushwa na kitendo hicho kwa kuwa hakuwa na taarifa ya ujio wake na wala hakutarajia.

“Nimeshukuru sana Rais kuja kunitembelea, ni jambo kubwa sikutegemea, na ndiyo maana nilikuwa kama nimeshtuka kwa sababu sikutegemea na sikupata taarifa yoyote, nilikuwa natoka tu ndani naona watu wengi wanaingia, nikajiuliza watu gani hawa? Mara namuona Rais,” alisema na kuongeza:

“Nimemshukuru sana Rais Magufuli kwa upendo wake, inaonyesha anajali sana watu wake. Kama mnavyoona, kwa kweli ninaendelea vizuri na ninapata matibabu mazuri, wananihudumia vizuri na sasa hali yangu ni nzuri na ni matumaini yangu kwamba baada ya muda mfupi nitatoka hapa hospitalini.”

Sumaye alilazwa katika taasisi hiyo siku nne zilizopita kwa matibabu ya moyo na madaktari wanaomtibu walimhakikishia Rais kwamba Waziri Mkuu huyo mstaafu alikuwa anaendelea vizuri ikilinganishwa na alipofikishwa hapo.

Pamoja na kumpa pole, Rais Dk. Magufuli pia alimuombea apone haraka ili aendelee na majukumu yake ya kila siku.

Habari Kubwa