Tangazo la Jecha laweka mguu sawa majeshi Z'bar

25Jan 2016
Nipashe
Tangazo la Jecha laweka mguu sawa majeshi Z'bar

TANGAZO la Mwenyekiti ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, la tarehe ya marudio ya uchaguzi, limeliweka Jeshi la Polisi na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi (SMZ) `mguu sawa' kwa kuimarisha ulinzi mkali visiwani humu.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Mhe Jecha Salum Jecha.

Chanzo cha kuimarishwa kwa ulinzi huo kumetokana na watu wasiofahamika kusambaza vipeperushi vyenye ujumbe wa uvunjifu wa amani katika maeneo tofauti ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam, alithibitisha kusambazwa kwa vipeperushi na polisi imeanza kuwasaka watu hao.

Alisema vipeperushi vya uchochezi vilianza kuonekana mitaani muda mfupi baada ya Zec kutangaza tarehe ya kurudiwa Uchaguzi Mkuu Machi 20, mwaka huu.

Hata hivyo, Kamanda Mkadam alisema kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha moja kwa moja vipeperushi hivyo kuwa vina malengo ya kisiasa kutokana na ujumbe wake na kuwataka wananchi kutoa taarifa za kuwafichua watu hao.

“Tutahakikisha Zanzibar inakuwa shwari katika kipindi chote hasa wakati huu wananchi wanasubiri uchaguzi wa marudio kufanyika Machi 20, mwaka huu,” alisema Kamanda Mkadam.

Aidha, alisema kuwa kumekuwapo na viashiria vya uvunjifu wa amani Zanzibar na kuwataka wananchi na wafuasi wa vyama vya siasa na viongozi wao, kuhubiri amani na kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa.

“Jeshi la polisi halitamvumilia wala kumuonea huruma mtu yeyote atakayebainika kuvuruga amani ya nchi,” alisisitiza Kamanda Mkadam.

Aidha, alisema ni kweli polisi walitumia mabomu ya vishindo juzi kuwatawanya wananchi waliokuwa wamekusanyika katika mtaa wa Kundemba kinyume cha sheria.

Alisema kuwa katika mkusanyiko huo, mtu mmoja alikamatwa na baada ya kumpekua alikutwa akiwa na dawa za kulevya.

“Jeshi lililazimika kufyatua bomu ili kuwatawanya vijana waliokuwa katika eneo hilo na kurahisisha kumkamata kijana aliyekuwa na dawa za kulevya,” alisema.

Askari wa doria wakiwa katika magari ya Jeshi la Polisi waliochanganyikana na wa Vikosi vya SMZ, wamekuwa wakifanya doria katika mitaa mbalimbali ya kuingia na kutoka Manispaa ya Mji wa Zanzibar kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa marudio.

Habari Kubwa