Tathmini ya waathirika wa bomoa bomoa ifanyike kwa umakini

19Jan 2016
Nipashe
Tathmini ya waathirika wa bomoa bomoa ifanyike kwa umakini

Wakazi walioishi katika Bonde la mto Msimbazi eneo la Mkwajuni,Kinondon Desemba 17,mwaka jana, walibomolewa nyumba zao ikiwa ni mwendelezo wa bomoabomoa unaoendelea mkoani Dar es Salaam.

Wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo walipaaza sauti zao juu wakilalamikia kuvunjiwa nyumba zao, kwa kile walichodai kuwa hawakupewa taarifa yeyote mapema inayowataka kuhama eneo hilo na mamlaka husika kabla ya utekelezaji wa mpango kubomoa makazi yao.
Kwa mtazamo wangu, pamoja na kasoro kubwa, kama mpango huo ungeratibiwa vizuri malalamiko yanayotolewa sasa na waathirika wa mpango huo katika eneo la Mkwajuni yasingekuwapo.
Kinachotakiwa sio kunyooshena kidole ni kurekebisha kasoro ,ili mambo yaende sawa.
Waziri wa Mazingira na Muungano, January Makamba hivi karibuni alitembelea eneo hilo na kuzungumza na baadhi ya wananchi walioathirika.
Makamba aliwaambia waathirika hao kuwa serikali ni sikivu kwa watu wake, hasa baada ya kutokea malalamiko ya ubomoaji wa makazi na aliwataka wananchi kupitia serikali yao ya mtaa kujiorodhesha ili hatua za utoaji msaada zifuatwe.
Kauli hiyo, imenishtua kidogo kutokana na kukosa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa mitaa, yawezekana wakanyonga haki za waathirika .Pia naogopa suala hilo lisichukuliwe kwa misingi ya itikadi za kisiasa kutokana na ukweli kuwa waathirika wengi watashindwa kunufaika na misaada hiyo.
Kwa mtazamo wangu ni kwamba,hakuna sababu za msingi kubagua waathirika kwa kigezo cha hatimiliki au leseni ya makazi.Serikali inapaswa kufanya tathmini ya wenye nyumba walioathirika na mipango ya bomoa bomoa.
Mwenye hati miliki au leseni za makazi, alijenga nyumba kwa gharama ileile ambayo mtu asiye na vielelezo ametumia lakini alikuwa akimiliki nyumba katika eneo hilo
Nathubutu kusema kuwa, serikali isibague waathirika wa bomoa bomoa kwani wajibu wa serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wake wanajengewa mazingira ya amani na usalama ili kuwafanya wanapiga hatua za maendeleo
Wakati Waziri Makamba ametembelea eneo hilo la Mkwajuni aliahidi hatua za dharura kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi ambao wazazi wao wameathiriwa na bomoa bomoa wanaendelea na masomo bila usumbufu wowote.
Kufuatia kauli hiyo yawezekana itakuwa vigumu kuwabagua wanafunzi hao kutokana na ukweli kuwa wanahitaji wanafunzi kuhakikishiwa kuwa wanapata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Kama azma ya serikali ni kuendelea na mpango wa ubomoaji ifanye uhakiki ili kubaini wananchi wenye hati miliki, leseni za makazi na wasiokuwa na nyaraka hizo ili kila mmoja kwa namna yake anashughulikiwa.
Pamoja na tathmini hiyo kufanyika, itabidi serikali izingatie kuwa wakati ule upatikanaji wa nyaraka hizo ulikuwa mgumu enzi hizo kutokana na mazingira kuwa magumu kwa baadhi ya watendaji.
Ili sheria ifuate mkondo wake, mabadiliko ya makusudi lazima yafanyike kwa kuzingatia haki za binadamu, waathirika hao waliishi pamoja hivuo masuala yao yashughulikiwe kwa pamoja.
Pamoja na hatua ya Serikali kufanya usafi katika eneo la Mkwajuni lililobomolewa kwa kuondoa kifusi ili shughuli za jamii zianze kutekelezwa ikiwemo kujenga eneo la burudani.
Waathirika hao wanapaswa kuandaliwa utaratibu mzuri ili kuendeleza maisha yao na siyo kuwaacha wakiendelea kuhangaika na watoto wao.
Sote tunafahamu kuwa bonde la mto Msimbazi limetangazwa kuwa hatarishi kuanzia kipindi cha serikali ya mkoloni mwaka 1949 na kukumbushiwa tena mwaka 1979.
Mwaka 2011 baada ya watu 49 kufariki kwa mafuriko katika mto Msimbazi, ulikuwa uthibitisho kuwa, eneo hilo kweli ni hatarishi kwa watu na serikali haiwezi kukaa kimya na kushuhudia watu wakiendelea kupoteza maisha.
Hatua za makusudi zinapaswa kuchukukuliwa kama Waziri Makamba alivyosema kuwa, Benki ya Dunia imetoa Sh Bilioni 100 kwa ajili ya kusafisha mto Msimbazi, ili kuepusha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaojitokeza kila mara.