TFF isake dawa kukomesha udhalilishaji viwanjani

23Jan 2016
Mhariri
Nipashe
TFF isake dawa kukomesha udhalilishaji viwanjani

VITENDO vya udhalilishaji vimeendelea kufanyika kwenye viwanja vya soka nchini licha ya mamlaka za soka kuvikemea sanjari na kutunga kanuni mpya kuvidhibiti.

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyoketi kisiwani Unguja, Zanzibar Juni 20 mwakamwaka jana ilipitiusha kanuni mpya Na. 37(24) kinachopendekeza adhabu ya kifungo kisichozidi miaka miwili na faini isiyozidi milioni tatu kwa wadhalilishaji.

Nipashe tunafahamu kuwa kanuni hiyo mpya ilitungwa baada ya mmoja wa wachezaji wa klabu ya Yanga kumdhalilisha kwa kumkumbatia na kumpiga mabusu uwanjani askari polisi mwanamke aliyekuwa na sare za Jeshi la Polisi baada ya nyota huyo kuifungia timu yake katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Costal Union jijini Tanga Februari 4 mwaka jana.

Licha ya kanuni hiyo kupitishwa na kuanza kutimika rasmi msimu huu, vitendo vya udhalilishaji viwanjani, hasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara vimeendelea.

Mwishoni mwa Oktoba mwaka jana, kamati ya uendeshaji wa ligi hiyo ilimfungia kwa miaka miwili na faini ya Sh. milioni 2 Juma Said, maarufu Nyoso, kutokana na kufanya kitendo cha udhalilisha dhidi ya Nahodha wa Azam FC, John Bocco.

Nahodha huyo wa City alipenyeza kidole katikati ya miguu ya mshambuliaji huyo wa Wanalambalamba wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ambayo mabingwa wapya wa Kombe la Kagame walishinda 2-1 dhidi ya timu hiyo ya Halmashauri ya jiji la Mbeya.

Katika kile kinachoonekana kanuni hiyo ya TFF haitishi, udhalilishaji wa aina hiyo ulijitokeza tena Jumatano wakati wa mechi ya ligi hiyo kati ya Simba na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ilishuhudiwa Nashon Naftar wa JKT Ruvu alimdhalilisha kwa kupenyeza kidole katikati ya miguu ya Hassan Ramdhani, maarufu Kessy, wakati wa mechi hiyo iliyomalizika kwa mabingwa mara 18 wa Tanzania Bara kushinda 2-0.

Tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, Nipashe hatuungi mkono vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha taratibu na Sheria 17 za Soka za Soka.

Tunaamini kuwa kujirudia kwa vitendo hivyo kwenye viwanja vya soka nchini ni ishara kwamba kanuni za TFF hazina mashiko kwa maana zimeshindwa kukomesha tatizo hilo.

Bocco na Kessy ndiyo walioonekana hadharani wakitendwa kwa kadhia hiyo, lakini kuna wachezaji wengi waliojitokeza hadharani na kueleza namna walivyowahi kukumbwa na changamoto hiyo.

Tunaamini wapo wachezaji wengi ambao wamefanyiwa vitendo hivyo, lakini hawajulikana kutokana na kutokujitokeza kwao na kuweka wazi na matukio hayo kutonaswa na kamera za waandishi wa habari kama ilivyotokea kwa Elias Maguli wa Stand United, Bocco na Kessy.

Ni rai yetu kwa mamlaka ya juu kisoka nchini, yaani TFF kusaka dawa ya kukomesha kadhia hiyo inayokiuka misingi ya maadili na ubinadamu.

Habari Kubwa