TFF, ZFA waboreshe viwango vya marefa

11Jan 2016
Editor
Nipashe
TFF, ZFA waboreshe viwango vya marefa

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi iliingia hatua ya nusu-fainali jana, mabingwa watetezi Simba wakiwakabili mabingwa wa 2010, Mtibwa Sugar wakati Yanga wanaosaka taji la pili wakichuana na URA ya Uganda.

Ingawa idadi ya timu shiriki imepungua kutoka 13 mwaka jana hadi nane, michuano hiyo mwaka huu imekuwa na msisimko na ushindani mkubwa.
Imeshuhudiwa timu ndogo ya Jamhuri ya Pemba ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya mabingwa mara tatu na wa kihistoria, Simba huku mabingwa mara mbili wa michuano hiyo wakishindwa kutinga hatua ya nusu-fainali kwa mara pili mfululizo wakifungwa 2-1 dhidi ya Mafunzo FC ya Ligi Kuu ya Zanzibar.
Hata hivyo, wakati michuano hiyo ambayo lengo lake ni kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 ikiwa sehemu ya burudani kwa wakazi wa Zanzibar na Watanzania wengine wanaoifuatilia kupitia runinga, kumekuwa na udhaifu katika uchezeshaji wa baadhi ya waamuzi.
Hadi sasa kwa mfano, tayari refa msaidizi mwenye beji ya uamuzi inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Dalila Jaffar ameondolewa kwenye orodha ya marefa wa michuano hiyo baada ya kukataa goli halali la mchezaji 'kinda' Shiza Kichuya (19) wa Mtibwa Sugar walipocheza dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Amaan Januari 3.
Mbali na refa huyo, wapo waamuzi wengine walioshindwa kuzitafsiri vyema Sheria 17 za Soka katika mechi za michuano hiyo mwaka huu.
Katika mechi ya Kundi B ya Azam FC dhidi ya Yanga, kwa mfano, ilishuhudiwa wachezaji wakipigana na kutemeana mate, lakini wakaishia kuonywa kwa kadi za njano, kinyume cha Sheria Na. 12 ya Soka (Rafu na Tabia Mbaya).
Nipashe tunatambua jitihada za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) katika kuzalisha waamuzi wengi wa soka nchini, lakini tunaona kuna haja mamlaka hizo za soka nchini kutilia mkazo kwenye ubora na si wingi wa marefa.
Tunatambua kwamba mamlaka hizi za soka nchini zimekuwa zikisisitiaza katika kuwasihi marefa wazingatie utoaji wa uamuzi ya haki, lakini baadhi wameendelea kufanya kinyume chake, wakionekana wazi kuzipendelea baadhi ya timu kwa maslahi wanayoyajua wenyewe na kuziathiri timu zisizo na ushawishi wa aina yoyote kwao.
Ni dhahiri kwamba marefa wa aina hii, wenye kuchezesha kwa upendeleo dhidi ya baadhi ya timu, wanaishushia heshima michuano ya soka nchini kwa sababu kupitia wao, mara nyingi matokeo ya mechi huwa hayaendani na kiwango cha soka kinachoonyeshwa uwanjani.
Kwa kukumbushia juu ya madhara ya kuwa na uchezeshaji usio wa haki, ni kwamba uchezeshaji usio wa haki uwanjani hushusha kiwango cha soka kwa Taifa lolote lile, Tanzania ikiwamo.
Kuendelea kuboronga kwa baadhi ya waamuzi, kama ambavyo imeonekana kwenye baadhi ya mechi za Kombe la Mapinduzi mwaka huu na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kutaendelea kuitafuna Tanzania katika michuano ya kimataifa.
Jambo jema na la kupongeza, ni uamuzi wa ZFA kuchukua hatua za haraka kwa kuwafungia marefa wanaoboronga katika mechi husika. Tunashauri TFF nao waiige utaratibu huo kwa manufaa ya soka na maendeleo ya Tanzania.
Ni matarajio yetu kuwa TFF na ZFA zitaendelea kusaka dawa ya kuboresha viwango vya marefa wa soka nchini kwa manufaa ya mchezo wenyewe, Ligi Kuu na Taifa kwa ujumla.

Habari Kubwa