`Toeeni taarifa za wahamiaji haramu'

11Jan 2016
Nipashe
`Toeeni taarifa za wahamiaji haramu'

MADEREVA, makondakta na abiria, wametakiwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wanapowatilia shaka watu kuwa ni wahamiaji haramu.

Wito huo ulitolewa na Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro,

alipokuwa akizungumza na Nipashe baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo(UBT) mwishoni mwa wiki.

Kamanda Sirro alisema Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uingizwaji wa silaha, wahamiaji haramu pamoja na uingizwaji wa dawa za kelevya.

“Taarifa tulizonazo ni kuwa hiyo mizigo yote inayoingia jijini hapa, hupitia njia za mabasi na ndiyo maana tumeamua kuja kuzungumza na madereva wa mabasi, makondakta na abiria ili washirikiane nasi kwa kutoa taarifa kwetu pindi wanapowashtukia watu ambao sio raia wa hapa nchini,” alisema Kamanda Sirro.

Hata hivyo, mmoja wa madereva alimueleza Kamishna Sirro kwamba wamekuwa wakisita kutoa taarifa kwa jeshi hilo kwa kuhofia nao watajumuishwa kama wahalifu.

Lakini Kamishna Sirro aliwaeleza kuwa endapo kutakuwa na ubabaishaji wa askari ambao hawana maadili ya kazi pale wanapotoa taarifa hizo, wampelekee yeye kupitia simu yake ya mkononi.

Habari Kubwa