Utoaji wa Leseni za Biashara ya Petroli

15Jan 2016
Nipashe
Utoaji wa Leseni za Biashara ya Petroli

KATIKA makala zetu za nyuma tuliwahi kuzitambulisha sheria kadhaa, pamoja na mamlaka ambazo kwa namna moja ama nyingine zinahusika kwa ukaribu zaidi na sekta ya nishati hapa nchini. Hususan, tukazibainisha sheria anuwai kuhusiana na jambo hili.

Waziri wa Sheria na Katiba, Dk.Harrison Mwakyembe

Baadhi ya Sheria hizo ni pamoja ni Sheria namba 27 ya mwaka 1980 ambayo ndiyo inahusika na masuala ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta ndani ya ardhi ya nchi yetu.
Zaidi ya hapo tukaitaja pia Sheria za Umeme ya mwaka 2008, inayohusika na masuala ya nishati vijijini, pamoja na Sheria ya Petroli ya mwaka 2008. Katika uelimishanaji huu tukazungumzia pia majukumu ya mamlaka, Wakala na Mashirika ya Serikali yaliyopewa jukumu la kuzisimamia Sheria hizi.
Tunazungumzia hapa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), (Mamlaka ya Udhibiti wa Bidhaa za Nishati na Maji nchini (EWURA) na kadhalika wa kadhalika.
Leo tena si vibaya kama tutalirejea eneo hili lakini kwa dhima moja tu sasa: Kuitazama Sheria inayohusika na Utoaji pamoja na uendeshaji wa Leseni za Biashara ya bidhaa za Petroli.
Kama tulivyowahi kubainisha huko nyuma, Sheria inayohusika na bidhaa za Petroli inaitwa Sheria ya Petroli ya mwaka 2008 na sheria hii ilitungwa kwa jina la kimombo kama The Petroleum Act, 2008. Hii hutajwa kama Sheria namba 4 ya mwaka 2008 na waweza kurejea chapisho muhimu la Prof.Ibrahim Juma (sasa Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania) ili kupata historia, Kanuni, athari kwa sheria nyinginezo pamoja na mambo mengine mengi kuhusiana na Sheria hii pamoja na Sheria nyinginezo takribani zote za Tanzania (na hasa zile zinazotumika bara pamoja na masuala ya Muungano). Chapisho hilo linaitwa Index to the Laws of Tanzania Mainland.
Msimamizi mahsusi wa Sheria hii ya Petroli ni EWURA na ipo Sheria maalum kabisa iliyoiunda Mamlaka hii na sheria hiyo si hii tunayoizungumzia hapa sasa. EWURA ni kifupi cha maneno ‘Energy and Water Utilities Regulatory Authority’(Mamlaka ya Udhibiti wa Bidhaa za Nishati na Maji).
Sheria hii ni ndefu na inazungumzia mambo mengi kwa hivyo basi tuliangalie eneo moja tu, lakini lililo muhimu sana, ndani ya Sheria hii: Leseni za Uendeshaji wa Biashara ya Bidhaa za Petroli.
Sura ya III (vifungu vya 7 hadi 12) ndivyo hasa vinavyozungumzia kwa undani taratibu kuhusiana na utoaji, uendeshaji, usimamishwaji na hata usitishwaji (termination) ama upokwaji kwa maana ya kunyang’anywa (revocation) wa Leseni za Uendeshaji wa Biashara ya Bidhaa za Petroli.
Vifungu 19-23 vilivyo ndani ya Sura ya V navyo vinahusika kwa ukaribu pia na mada hii kwa vile vinatoa wajibu wa kisheria (legal obligations) anaopaswa kuwa nao mmiliki yeyote wa leseni ya Petroli aliyepewa na EWURA kupitia Sheria hii ya mwaka 2008.
Vifungu vingine takribani vyote vinahusika lakini si dhumuni la makala hii kuvizungumizia leo kutokana na uhaba wa nafasi na pia ufinyu wa muda. Tuviangalie kwa ukaribu zaidi vifungu vya 7-12 kuhusiana na utoaji, uendeshaji na upokonyaji wa leseni za petroli.
Kifungu cha 7 cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2008 kinatangaza uharamu wa kisheria wa mtu, kampuni ama taasisi yeyote kujiingiza katika shughuli za biashara ya bidhaa ya Petroli pasipo kwanza kufuata vigezo vinavyokidhi matakwa kwa mujibu wa Sheria hii, na hasa lile kufanya biashara hiyo bila leseni iliyotolewa na mamlaka husika kwa mujibu wa vifungu vya sheria hii (ya mwaka 2008).
Inatakiwa basi, kupitia katika kifungu cha 8 cha Sheria hii, kwa mtu yeyote anayetaka kujihusisha na shughuli moja ama zaidi katika mlolongo wa utoaji huduma (Supply chain) za biashara ya petroli, kuwasilisha kwanza ombi la uendeshaji wa shughuli hizi kwa kulipeleka ombi hilo kwa Mamlaka husika. Taratibu za kujaza na kuwasilisha maombi, kuyafanyia tathmini na hatimaye kuyapitisha, pamoja na aina ya nyaraka zinazopaswa kuambatanishwa na mwombaji mbele ya mamlaka itoayo leseni hizi, zimo katika kanuni za utoaji wa leseni za biashara ya Petroli ambazo zilitungwa na mamlaka husika kwa idhini ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Sheria hii.
Inatia moyo kuona kwamba Sheria hii imenuia kuondoa upendeleo, ubaguzi, urasimu na ukiritimba ili kuleta ufanisi zaidi na pia ili kuheshimu masharti yaliyomo ndani ya Katiba yetu ya mwaka 1977 pamoja na mikataba ya kibiashara ya kimatiafa,kwa kutamka wazi kupitia kifungu 8(3) kwamba katika mchakato wote wa kuomba, kufanya tathmini na hatimaye kutoa (ama kutotoa) leseni za kuendeshea biashara ya bidhaa za petroli, kila muombaji atapaswa kupewa haki ya usawa na kutoonewa kwa misingi ya kibaguzi au vigezo vingine vyenye kutoa kipaumbele visivyo na tija.
Katika kuhakikisha hili linatekelezeka ki-uhalisia wake, kifungu hiki kidogo kinaenda mbali zaidi kwa kusema kwamba mamlaka husika za leseni za Petroli hazitapaswa kuweka sharti au masharti ama vikwazo vingine ambavyo Sheria yenyewe ya Bunge haikuviidhinisha kuwepo.
Hata hivyo, Sheria ya Petroli inaweka sharti moja ambalo ni muhimu na lenye manufaa. Kifungu cha 8 (4) kinatamka kuwa kabla ya kutolewa kwa leseni yoyote inayoruhusu biashara ya petrol muombaji atapaswa kuthibitisha kwamba ameyazingatia masharti kuhusiana na utunzaji wa mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
Ndiyo kusema kwamba atapaswa basi kupata hati safi kutoka Mamlaka ya Udhibiti na Utunzaji wa Mazingira, NEMC. Kwa kawaida moja ya matakwa muhimu yaliyo katika Sheria ya Mazingira ni lile linaloshurutisha kufanyika kwanza kwa Tathmini ya Athari za Kimazingira kwa mradi wowote ambao unapaswa kufanyiwa tathmini chini ya Sheria hiyo.Tathmini hii muhimu sana hujulikana kama EIA, ikiwa ni kifupi cha maneno ya kimombo ‘Environmental Impact Assessment’.
Mwisho, kabla ya kufanya uamuzi wa ama kuidhinisha utoaji wa leseni au kuyakaa maombi, Sheria kupitia kufungu cha 9 inataja vigezo takribani tisa (9) hivi ambavyo Mamlaka ya utoaji leseni itapaswa kuvizingatia. Vigezo hivyo ni pamoja na : (1) mchango wa biashara husika katika kusaidia kukabiliana na mahitaji ya wateja wa bidhaa za petrol.
Pia kukabiliana na mapungufu ya bidhaa hizi nchini kwa sasa na siku za usoni; (2) iwapo biashara husika inaendana na Mkakati wa Taifa wa Nishati; (3) Mchango wa biashara inayokusudiwa katika kuchochea ushindani wa kibiashara kwa bidhaa za Petroli nchini; (4) Athari za Kijamii na pia Kimazingira za Biashara/mradi unaoombewa leseni; (5) Uwezo wa Muombaji Leseni kukidhi vigezo vya kisheria, kitaalam, kiuchumi na kifedha katika uendeshaji wa leseni anayoitaka;
Pia (6) Gharama za shughuli inayotakiwa kufanywa na atahri zake katika bei ya bidhaa za Petroli nchini; (7) Maoni ama pingamizi zozote kutoka kwa wananchi na wadau kuhusiana mradi/biashara inayopaswa kufanywa na muombaji leseni; na pia (8) athari nyingine chanya ama hasi katika maslahi ya umma.
Kama Mamlaka itaridhika kwamba muombaji amemudu vigezo vyote na kwa kuzingatia mambo mengine yaliyo ndani ya Sheria, basi leseni yaweza kutolewa, ikiwa na masharti kwa anayepewa, iwapo itakuwa lazima (Rejea kifungu 9(1))
Itokeapo kwamba, muombaji hakukidhi vigezo basi kifungu kidogo 9(3) kinaidhinisha Mamlaka husika kukataa kuidhinisha kutolewa leseni hiyo, lakini iwapo hili linafanyika basi mamlaka husika itapaswa kuziweka sababu hizi katika maandishi kwa muombaji ambaye leseni haijatolewa kwake.

Habari Kubwa