Viongozi wetu na hatma ya Wizara ya Afya

06Jan 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe
Viongozi wetu na hatma ya Wizara ya Afya

KWA muda mrefu sasa sekta ya afya imekuwa miongoni mwa maeneo yasiyopewa kipaumbele kwa vitendo, licha ya umuhimu wake kwa mfumo, maisha na shughuli tofauti za binadamu.

Dk Khamis Kigwangala

Ingawa kuna sera, sheria za nchi, mikataba na itifaki za kikanda na kimataifa kuhusu afya bora, hapa nchini umuhimu wake kwa watu haupo katika kiwango cha kuridhisha.

Mathalan, unapofika wakati wa kampeni za kuwapata viongozi wa umma, sekta ya afya haiibui mijadala ya kutosha kama ilivyo kwa maeneo mengine ya maendeleo.

Badala yake wanaohitaji uongozi wa umma wamekuwa wakiahidi kufanikisha nia za kuwapo hali bora katika maeneo tofauti ya afya, mwisho wa siku inaendelea kuwa ‘taabu juu ya taabu’.

Ndio maana kwa miongo mingi sasa, huduma za afya nchini zimekuwa duni na mbovu kiasi cha kusababisha hasara kwa uchumi wa taifa na maisha ya watu.

Ongezeko la magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika, kushindwa kutekelezwa kwa sehemu za sera na sheria zinazohusiana na afya yamekuwa mambo ya kawaida yasiyopatiwa suluhu kutokana na utendaji kazi kwa mazoea. Uzembe juu ya uzembe!

Ingawa hali ipo hivyo, mipango na mikakati ya serikali katika kuiboresha sekta ya afya imewasilishwa mara kadhaa kwenye mikusanyiko tofauti, baadhi yake ikitekelezwa na mingine kutelekezwa.

Lakini hata ile inayotekelezwa kwa ufanisi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee (kwa sasa) inaongoza kwa ukiritimba wa utoaji taarifa na hivyo kuinyima jamii pana haki ya kutambua ukweli huo.

Kwamba katikati ya uzembe, rushwa na aina nyingine za ufisadi zilizoighubika sekta hiyo, bado kuna mafanikio japo kwa uchache yaliyokuwapo, lakini ‘yakafichwa’ ili yasijulikane kwa umma.

Hapo ndipo inapoibuliwa hisia kuhusu udhaifu wa idara na kitengo kinachohusiana na masuala ya habari na mawasiliano na mahusiano ya umma katika wizara hiyo.

Kwa bahati mbaya miongoni mwa wahusika katika utoaji habari, mawasiliano na mahusiano wizarani hapo, wamekuwapo kwa zaidi ya muongo mmoja hivyo kuendeleza ukiritimba unaopaswa kuwekwa kwenye orodha ya ‘majipu’ yanayostahili kutumbuliwa kwa ukali na haraka.

Lakini sasa mwanga wa matumaini ya kuondokana na uduni na ubovu wa huduma za afya zinazosimamiwa na wizara hiyo, umeanza kuonekana.

Hatua kama zinazochukuliwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamis Kigwangallah na ‘bosi’ wake, Ummy Mwalimu zinapaswa kuungwa mkono.

Hatua hizo ni pamoja na udhibiti wa huduma ‘feki’ kama za tiba asilia na tiba mbadala zinazochangia kuathiri afya za watu, ingawa waathirika wanaaminishwa kuwa zinafaa kwa uponyaji.

Hata hivyo huduma hizo zikapata nguvu na kuwafikia watu wengi kutokana na kudumaa kwa zanahati, vituo vya afya na hospitali za umma.

Kwa hiyo Dk Kigwangalla anapojitoa ‘kuzimfunga kengele’ tiba mbadala na zile za asilia ili zisiwe chanzo cha kuchagiza kasi ya kuathiri afya za watu, anapaswa kupongezwa, kuungwa mkono na kushauriwa kwa nia njema.

Hali hiyo itasaidia kupata suluhu yenye maslahi mapana kwa umma, kwamba hata kama huduma stahiki za tiba mbadala na asilia zitatolewa, isiwe katika kuathiri afya za watu.

Hali ilivyo sasa tiba mbadala na zile asilia zinawahusisha ‘matapeli’ wa ndani na wale wa kutoka nchi za Asia hususan Korea Kaskazini, India na China.

Wanatumia mwanya wa ukosefu wa huduma bora za afya nchini kuingiza na kusambaza ‘madudu’ wanayoyaita tiba mbadala.

Wasiokuwa na kimbilio la kupata huduma bora wanazoziamini zinazotolewa ‘kiutapeli’.

Inawezekana wakajitokeza watu wenye hadhi ya juu kitaaluma ama vinginevyo, wakataka kukidhi matakwa ya nia zao na kuunga mkono ‘utapeli’ unaofanywa katika sekta ya afya. Haipaswi kuwa hivyo.

Imani hiyo inawafanya watu wengi ‘kuliwa’ fedha zao, tena ambazo wangezitumia kwa watoa huduma wa kuaminika na wakapata tiba husika.

Ukiacha hali hiyo iliyochochewa na kushindwa kuwajibika kwa viongozi wenye dhamana kwa awamu zilizopita, bado utendaji kazi duni serikalini ukaendelea kuchangia uwapo wa huduma duni.

Mathalan inapotokea wahitaji kwa `miaka nenda miaka rudi’ wakafika wizarani kupata huduma, lakini wahusika katika idara ama vitengo mahususi wakawa hawajafika kutokana na sababu kama foleni, itapaswa kuvumiliwa?

Ndio maana bado ninauona umuhimu na maana ya tukio la Dk. Kigwangalla kufunga mageti ya wizara hiyo hivi karibuni.

Tukio ambalo kwa taarifa za uhakika, sasa wafanyakazi wanaingia wizarani hapo kabla ya muda wa mwisho unaotambuliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zao.

Na hiyo haihusishi kuingia kazini tu, bali kutumia muda mwingi kuwahudumia wahitaji na hivyo, hatua kwa hatua, kuzifuta nyayo za uzembe na utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea uliozoeleka.

Kwa hakika, mwenendo wa wizara hiyo iliyo mhimili mkuu katika uboreshaji wa afya za watu na mazingira, unaridhisha ingawa wahusika hawapaswi kubweteka.

Hivyo ni wajibu wa jamii kuziunga mkono, lakini pia kukosoa katika nia ya uboreshaji ili mwisho wa siku, viongozi wetu waweze kuliongoza taifa katika kuwa na hatma yenye uwapo wa huduma bora za afya nchini.