Vita ya madaraka ya Bunge yakolea

25Jan 2016
Nipashe
Vita ya madaraka ya Bunge yakolea

KASI iliyoonyeshwa na Bunge lililopita katika kuisimamia Serikali kiasi cha kumlazimu Rais Jakaya Kikwete, kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri zaidi ya mara nne, inatajwa kuwa chanzo cha kuibuka kwa vita inayoonekana wazi ya kutaka kudhibiti mhimili huo muhimu wa dola.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa walisema mkanganyiko ulioibuka kuhusiana na uteuzi wa kamati mbalimbali za chombo hicho ni ishara ya wazi kwamba kuna vita ya kutaka kudhibiti utendaji wa chombo hicho, ambayo mshiriki wake mkuu ni serikali ya awamu ya tano.
Wakieleza zaidi, baadhi ya wachambuzi hao wamedai kuwa mwenendo wa Bunge la 11, kuanzia mchakato wake wa kumpata Naibu Spika na hadi sasa katika uteuzi wa wajumbe wa kamati za Bunge, unaashiria kuwa serikali imepania kupunguza makali ya chombo hicho ambacho katika miaka kumi iliyopita kimejitahidi kwa kiasi kikubwa kutekeleza wajibu wake wa kuisimiamia serikali kiasi cha kuibua masuala kadhaa yaliyotikisa baraza la mawaziri, mfano ukiwa ni kashfa za Richmond, uchotwaji wa Sh. bilioni 133 za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu (BoT), Operesheni Tokomeza na pia uchotwaji wa mabilioni ya fedha kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa pia BoT.
Mwishoni mwa wiki, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alitangaza wajumbe wanaounda kamati mbalimbali za chombo hicho huku mjadala ukiibuka kuhusiana na uamuzi wa kutowarejesha baadhi ya wabunge walioitikisa serikali kutokana na kuibua kwao mambo kadhaa kupitia kamati walizokuwamo. Wabunge wengi waliokuwa maaarufu wamejikuta wakikosa nafasi katika kamati mbalimbali walizokuwapo awali ikiwamo nyeti ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), na kisha wengi wao kuwekwa katika Kamati ya Huduma za Jamii.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ni miongoni mwa wabunge machachari waliojikuta wakiwekwa katika Kamati ya Huduma za Jamii, wengine wakiwa ni Peter Serukamba ambaye awali alikuwa katika Kamati ya Miundombinu na Tundu Lissu aliyeng’ara wakati alipokuwa katika Kamati ya Katiba na Sheria na sasa kuwekwa pia katika kamati hiyo ya Huduma za Jamii.
Mmoja wa wachambuzi hao alidai kuna uwezekano Bunge la sasa linaelekea kuwa kibogoyo kwani zipo ishara kwa serikali kuingiza ushawishi wake.
“Kama utakumbuka, mchakato wa kumpata Naibu Spika ulizua maneno kwa sababu licha ya Dk. Tulia (Ackson) kuwa na sifa zote, bado kuna ukweli kuwa hakuwahi kuwa mbunge hapo kabla. Hivyo, kama siyo Rais kumteua kuwa Mbunge na muda mfupi baadaye kuchukua fomu za kugombea unaibu spika, maana yake, isingetarajiwa kwa mtu asiyewahi kuwa mbunge leo hii kuwa mtu wa pili kwa madaraka bungeni. Hii ni dalili kwamba kulikuwa na uungwaji mkono wa serikali. Na hili la uteuzi wa wajumbe wa kamati ni dalili nyingine kwamba tunakoelekea Bunge litakuwa kibogoyo. Tuombee isiwe hivyo,” aliongeza mchambuzi huyo ambaye ni mhadhiri mwandamizi.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema uteuzi wa wajumbe wa kamati za Bunge ni wa kushangaza kwa kuwa wabunge machachari wamepelekwa kwenye kamati ambazo hazisimamii wizara nyeti.
Alisema serikali ya Dk. John Magufuli, imejitambulisha kwa ufuatiliaji wa karibu wa utendaji wa serikali na kuhoji mambo mbalimbali, lakini inashangaza kuwa hapo hapo, wabunge ambao wanafahamika kwa ufuatiliaji mzuri wa mambo wamewekwa kando ya kamati nyeti kama PAC.
“Tunapata shaka…tulitarajia tuwe na wenyeviti wa kamati wenye kuibua mambo, yeye (Rais) pekee hawezi kufika kila mahali, anahitaji wabunge wafuatiliaji,” alisema, akiongeza kuwa uteuzi wa kamati za Bunge la 11 umefanyika kama vile hakuna chama cha upinzani chenye nguvu bungeni na kutoa taswira kuwa bado kuna bunge la mfumo wa chama kimoja kwa kutafuta namna ya kuwafunga midomo wabunge machachari waliowezesha kuibuliwa kwa maovu mengi kupitia kamati walizokuwapo awali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Sikika, Irenei Kiria, alisema udhaifu upo kwa wenyeviti wa baadhi ya kamati na jambo hilo ni hatari kwa uimara wa Bunge.
“Ukishakuwa na kamati yenye mwenyekiti hafifu, ni wazi kuwa watashindwa kuhoji Wizara husika. Hii itafanya tuwe na Bunge lisiloweza kuiwajibisha serikali bali kuwa na Bunge la kuisaidia serikali,”alisema.
Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Iringa, Essau Ntabindi, alisema kwa mtazamo wake, uteuzi wa wajumbe katika kamati za bunge unaweza kuelezwa kuwa wa njia mbili, moja ikiwa ni kisiasa na pili ikawa ni uteuzi wa kawaida.
Alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli inaonyesha imedhamiria kuleta maendelea nchini, hivyo kuwaweka baadhi ya wabunge ambao huibua hoja nzito bungeni kwenye kamati ya huduma za jamii kunaweza kukawa na sababu ya kuimarisha sekta hizo.
Kwa mfano, alisema kuwaweka Zitto Kabwe na Serukamba katika kamati ya huduma za jamii pia kunaweza kukasaidia kuboresha sekta hizo, ikiwamo sekta ya afya na elimu na hilo ni jambo jema.
Aidha, alisema njia ya pili, ni kuwapo kwa mbinu ya serikali kulipoza bunge ili isiingie katika mtikisiko wa kisiasa kama ilivyotokea katika awamu ya serikali ya nne.

SARAKASI KAMATI ZA BUNGE
Awali, habari ambazo Nipashe ilizipata, zilieleza kwamba baadhi ya wabunge ambao walikuwa machachari kwa kuibua mambo mengi mazito katika Bunge la 10 na makada waliowahi kutikisa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa hoja mbalimbali, walijikuta wakiondoshwa kwenye kamati walizokuwa wamepangiwa awali kutokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya vigogo.
Ilidaiwa kuwa baadhi ya wabunge waliohamishwa kwenye kamati walizokuwa wamepangiwa awali siku moja ama saa chache kabla ya majina yao kutangazwa ni pamoja na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, ambaye awali alipangwa katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na baadaye kupelekwa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Taarifa zilidai kuwa Zitto alipangwa pia kwenye kamati ya PAC, lakini baadaye akapelekwa Ardhi, Maliasili na Utalii, kisha akahamishiwa tena Kamati ya Bajeti kabla ya kufikishwa kwenye Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii.
Ilielezwa zaidi kuwa Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, awali alipangwa kwenye kamati ya Uwekezaji na Mitaji kabla ya kupelekwa kwenye Huduma za Maendeleo ya Jamii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kasikazini, Serukamba, awali alipangwa kwenye kamati ya Viwanda na Biashara kabla ya kujikuta pia kwenye kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii.
Kadhalika, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, awali alipangiwa katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kabla baadaye kujikuta kwenye Kamati ya Bajeti.
Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana, Spika wa Bunge Job Ndugai, alikanusha madai ya kuwapo kwa shinikizo kutoka kokote bali, kilichotokea ni kutekeleza uamuzi wa Bunge kuhakikisha kuwa wabunge wa zamani hawapangwi katika kamati walizowahi kuzitumikia awali.
Alisema katika Bunge la sasa, asilimia 80 ni wapya huku asilimia 20 wakiwa wa zamani na kwamba hivi sasa, wabunge wote wa zamani wako kwenye kamati nyingine na siyo walizokuwapo awali.
"Isifike mahali kamati fulani ikaonekana ni ya mtu fulani peke yake, kwa hiyo hakuna aliyerudi kamati ya zamani," alisema Ndugai.

KASHFA ZILIZOTIKISA BUNGE
Kashfa ya mkataba tata wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond iliibuliwa bungeni mwaka 2006 na kuvunja baraza lote la mawaziri baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kulazimika kujiuzulu baada ya kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.
Mwaka 2008, Bunge liliibua kashfa ya EPA iliyoitikisa vilivyo serikali. Baadaye, mabadiliko ndani ya Baraza la Mawaziri yalimuweka nje aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Maghji huku Gavana wa BoT, Daudi Balali (sasa marehemu) akifutwa kazi.
Mei 2012, wakati ilipotolewa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kujadiliwa bungeni, ulitokea mtikisiko mkubwa uliowang’oa mawaziri sita na manaibu wawili.
Makali ya Bunge yaliichachafya tena Serikali ya Rais Kikwete, Desemba 2013 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza Ujangili. Baraza la Mawaziri lilitikiswa na mawaziri kadhaa waling’olewa.
Novemba 2014, ripoti ya PAC bungeni baada ya kuchambua ile ya CAG, iliyochunguza miamala ya Akanti ya Tegeta Escrow ilisababisha mtikisiko mkubwa na mawaziri kufutwa kazi, ambao ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Habari Kubwa