Wababe URA watua Zanzibar

02Jan 2016
David Kisanga
Nipashe Jumapili
Wababe URA watua Zanzibar

TIMU ya soka ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) imetua salama Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza leo kwenye Uwanja wa Amaan visiwani humo.

TIMU ya soka ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA)

Timu hiyo ya Ligi Kuu ya Uganda imesafiri zaidi ya Km 1200 kwa basi baada ya kuondoka jijini Kampala Jumatano asubuhi ikipitia Mutukula.
Kwa mujibu wa daktari wa timu hiyo, Edward Kulubya, wachezaji wao wote wako salama na wako tayari kwa ajili ya mechi za mshindano hayo yanayofanyika mara moja kwa mwaka.
"Tulisafiri salama kutoka Kampala na tuko tayari kwa mashindano. Tulifika hapa (Zanzibar) jana (juzi) Ijumaa," alisema.
URA FC itaanza kusaka taji lake la kwanza la michuano hiyo kwa kuikabili JKU FC ya Zanzibar kesho 10:15pm kwenye Uwanja wa Amman.
Wakusanya mapato hao wamewaacha baadhi ya nyota wao muhimu wakiwamo mastraika matata Robert Sentongo na Frank Kalanda pamoja na beki Richard Jjuuko ambaye yuko kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda (Cranes) kinachojiandaa kwa michuano ya CHAN.
Kiungo Derrick Tekkwo alikuwa Kampala juzi, lakini alitarajiwa kuungana na timu Zanzibar jana jioni. URA itaikabili Simba Januari 5 saa 2:15 usiku katika mechi ya pili ya Kundi A kabla ya kufunga hatua ya makundi kwa kuikabili Jamhuri FC Januari 8 saa 10:15 jioni.

Habari Kubwa