Wachezaji Bongo sasa mmemsoma Samatta

11Jan 2016
Nipashe
Wachezaji Bongo sasa mmemsoma Samatta

TANZANIA imepata heshima kubwa duniani baada ya mchezaji wake Mbwana Samatta kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka ndani.

Ilikuwa ni furaha kubwa wa Watanzania wote na Ukanda mzima wa Afrika Mashariki baada ya kutangazwa kuwa ndiye mshindi wa tuzo hiyo.
Itabaki kuwa siku ya kukumbukwa na Mbwana Ally Samatta katika maisha yake yote, familia yake na Watanzania kwa ujumla akitoka kwenye nchi ambayo si moja kati ya vigogo barani Afrika.
Alikuwa akipambana na wachezaji wengine wawili; Robert Kidiaba Muteba, Mkongomani anayeichezea TP Mazembe na Baghdad Bounedjah raia wa Algeria anayekipiga kwenye klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Mbali na kutwaa tuzo hiyo, amefanikiwa kuchaguliwa kwenye kikosi kinachounda wachezaji bora barani Afrika.
Kwa hili lililotokea ni somo kubwa kwa wachezaji wote wa Kitanzania kuwa hakuna kisichowezekana ili mradi tu iwekwe nia, uvumilivu, kujinyima, nidhamu na bidii.
Samatta ametoka kwenye kitongoji cha Mbagala ambacho wanaishi watu wengi wenye kipato cha hali ya kawaida, lakini kutokana na kuwa na vitu nilivyovieleza hapo juu, amepasua anga na sasa anakula matunda ya kile alichokikusudia.
Na kama tulivyomsikia, mwenyewe anasema hajaridhika na mafanikio hayo kwani anataka sasa awe mmoja wa wachezaji watakaotingisha Ulaya.
Samatta amekuwa kama kioo sasa kwa wachezaji wote wa Tanzania wanaocheza soka nchini kuwa mafanikio hayaji kama mvua au kuridhika mapema.
Kote alikopitia Samatta, alikutana na wachezaji ambao walikuwa na vipaji vikubwa kuliko yeye, lakini kwa sasa ama hawako tena kwenye medani ya soka au viwango vyao viko chini.
Tanzania ni moja ya nchi ambayo imebarikiwa kwa kuwa na wachezaji wenye vipaji vya soka, lakini kwa bahati mbaya sasa vinaishia njiani kwa sababu mbalimbali, ikiwemo wenyewe kutojitambua.
Kuwa na kipaji pekee hamfanyi mchezaji awe mzuri na kudumu katika soka. Ila mchezaji yeyote anayeheshimu kipaji chake na kukilea, kukiendeleza kama Samatta ndiye anayefanikiwa.
Pamoja na wachezaji wengi wa Kitanzania kuwa na vipaji, lakini wengi wao ni wavivu wa mazoezi.
Wengine wanashinda, kulala baa na kufanya vitendo ambavyo haviendani na maadili ya soka.
Wapo wachezaji ambao wanadhani ili waendelee kuwa wachezaji wazuri au mastaa, lazima wawe washirikina au waende kwa waganga 'wakajitengeneze'.
Lakini Samatta ameonyesha kuwa hayo yote hayana ukweli, kwani aliingia Simba akiwa mchezaji kinda na aliwakuta mastaa wakubwa kina Mussa Hassan Mgosi, lakini kwa juhudi zake aliweza kupata namba, akacheza kwa nusu msimu tu na kununuliwa na TP Mazembe.
Pia hapa nchini kuna wachezaji wazuri tu, lakini badala ya kucheza soka na kuonyesha vipaji vyao ili wasonge mbele wao kazi yao ni kuchukua pesa toka upande wa pili wa wapinzani wao ili wacheze chini ya kiwango.
Wachezaji hawa inabidi sasa wajifunze kitu kuwa kitendo cha kuuza mechi kinawafanya waonekana kuwa hawana viwango vya kucheza soka, badala yake wachezaji wa upande wa pili ndiyo wanaonekana kuwa mastaa.
Hii si hatari kwa maendeleo ya soka nchini, bali hata kwa wao wenyewe kwa sababu huwezi ukafika mafanikio kama ya Samatta kwa kuuza mechi.
Yeyote anaweza kuwa na uwezo mkubwa kisoka mara mbili kuliko hata Samatta, lakini kutokana na tabia hiyo hakuna atakayetambua kipaji cha mchezaji kwa sababu hakionyeshi uwanjani kwa sababu ya tamaa ya pesa za muda mfupi tu.
Sasa wachezaji wetu waamke wajue kuwa soka kwa sasa ni utajiri mkubwa mkubwa.
Mwanasoka wa kizazi hiki anaweza kuwa tajiri mkubwa na kumiliki hisa mbalimbali kwenye makampuni ndani na nje ya nchi au yenye mwenyewe kuyaanzisha.

Habari Kubwa