Wafundi wa mitaani wachangamkie kurasimishwa ujuzi wao

22Jan 2016
Nipashe
Wafundi wa mitaani wachangamkie kurasimishwa ujuzi wao

WIKI mbili zilizopita, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ilifungua ukurasa mpya nchini ilipofanya sherehe ya kutoa vyeti kwa wahitimu 67 wa programu ya kurasimisha ufundi, ama ujuzi kwa mafundi waliopata utaalamu huo kupitia mfumo usio rasmi.

Hawa ni wale ambao wakati mwingine huitwa ‘mafundi ya mitaani.’
Mafundi tulionao kila siku, wakiwa wametapakaa karibu katika kila kona za majiji, miji hata kwenye maeneo yetu ya vijijini.
Mafundi ambao wamekuwa na msaada mkubwa kwa watu wa kada zote za maisha na wa vipato vyote, vikubwa, vya kati na vya kawaida ama vya chini.
Nasema wamekuwa ni wa msaada mkubwa kutokana na kutufanyia kazi mbalimbali za ufundi kama zile za ujenzi wa nyumba, matengenezo ya magari yetu yanapoharibika, samani pamoja na huduma zingine kama za vyakula kwenye shughuli za kijamii.
Ziwe za arusi, mahafali, kipaimara,ubatizo vifo na nyingine vya aina hiyo.
Ni mafundi ambao tunawategemea kwa asilimia kubwa, lakini pengine tukiwalipa ujira mdogo ikilinganishwa na iwapo kazi hizo zingefanywa na mafundi ama wataalamu wanaotambulika rasmi.
Wanaotambulika rasmi kwa maana ya kupata mafunzo ya fani husika kupitia mfumo rasmi.
Yaani ule wa kupitia darasani, kwa muda maalumu kama ni wa mwaka ama miaka wakisomea fani husika.
Kama ni ya ufundi magari, uashi ama useremala na kisha kufanya mtihani na hatimaye kutunukiwa cheti.
Lakini mbali na sisi watu wa kawaida kuwatumia mafundi hawa wa mitaani tunapokuwa na shida inayohitaji utaalamu wao, bado hata makampuni makubwa yakiwamo ya ujenzi, makampuni ya magari, mahoteli na mengine pia huwatumia mafundi hawa hawa kwenye miradi yao.
Mfano hai uko kwa makampuni yanayopata zabuni za ujenzi wa majengo na barabara za aina zote.
Sehemu kubwa ya kazi za wazabuni hao hufanywa na mafundi hawa hawa, tunaowaita kuwa wa ‘mitaani.’
Lakini pia bado hata haya makampuni makubwa huwa wanalipa ujira kiduchu, ikilinganishwa na mabilioni ya fedha yanayolipwa kwenye miradi hiyo.
Kimsingi sababu kubwa ya kutothamini utaalamu wa mafundi hao, pamoja na kuwa kazi wanazozifanya zinawaonyesha pasi na shaka kuwa, ni wataalamu waliobobea kwenye maeneo yao, ni ile dhana kuwa, wao ni mafundi wa ‘mitaani.’
Kwamba tunawachukulia ‘poa tu’ na ndiyo sababu ya kuwapa ujira mdogo, kana kwamba utaalamu wao hawakuutolea jasho.
Sasa nimesema hapo juu kuwa, mamlaka ya ufundi imefungua ukurasa mpya baada ya kuja na programu ya kurasimisha ufundi ama utaalamu wa mafundi hawa, na imetoa wahitimu hao 67 wa kwanza wa program hiyo.
Hawa ni wa fani za upishi, ufundi seremala, uashi, magari, vyakula na vinywaji ambao wametambuliwa rasmi.
Hii ni baada ya mafunzo yaliyoendeshwa kwa mara ya kwanza na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma (VETA) cha Dar es salaam.
Katika programu hii, mafundi hao waliopata mafunzo yao nje ya mfumo rasmi, waliweza kupimwa viwango vya ujuzi wao kwa kutumia mitaala ya VETA, kabla ya kupatiwa vyeti vya VETA vya kutambua rasmi ujuzi wao.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA aliyekuwa mgeni rasmi, Geofrey sabuni, VETA ilianzisha programu hiyo baada ya kufanya utafiti wa miaka mitatu kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na iliyokuwa Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana, wakati huo.
Sabuni alisema walifanya utafiti katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro na Mwanza kwa mafundi waliopata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi, ama wa ‘mitaani’ na matokeo kuonyesha uhitaji mkubwa wa kuwa na program ya kurasimisha utaalamu, ufundi, ujuzi na elimu ya wataalamu hao.
Sasa hoja ya mjadala huu inaona kuwa, idadi ya wanafunzi 67 wa kwanza waliohitimu kwenye program hiyo kimsingi ni ndogo sana.
Ni ndogo sana ikilinganishwa na namna mafundi hawa walivyo wengi na walivyotapakaa katika maeneo mbalimbali nchini.
Sasa mjadala unadhani ni wakati muafaka kwao popote pale walipo, kuchangamkia program hii inayolenga kuutambua utalaamu wao rasmi, kwani kwa mujibu wa Sabuni itaendeshwa kwenye kanda tano za VETA, kupitia kwenye vyuo vyao vilivyotapakaa nchi nzima.
Ni asili ya kila binadamu kutaka kutambulika rasmi kwa kile anachokifanya na hivyo ni wakati muafaka kwa mafundi hawa kuitumia fursa hii inayolenga kuwatambua rasmi.
Mjadala unaamini kwamba wakipata vyeti vya VETA, vitawasaidia katika shughuli zao za kila siku, iwe wamejiajiri kwa maana kuwa na fursa hata ya kuomba zabuni mbalimbali kwani vyeti vyao vitawasemea.
Na kama wameajiriwa yumkini sasa watakuwa na fursa ya kulipwa ujira unaoridhisha kulingana na vyeti watakavyopata.
Ni muhimu wakaelewa kuwa, vyeti ni mlango wa kuwafungulia ajira ama kazi zenye staha katika suala zima la kupambana na umaskini.
Hivyo sasa ni shime kwa mafundi hawa wa ‘mitaani’ kuchangamkia fursa hii ili waweze kupata vyeti vya kuurasimisha ujuzi wao kwa kutumia mitaala ya VETA, mamlaka ambao inaheshimika nchini kwenye suala zima la ufundi stadi.

Habari Kubwa