Waliokula fedha maabara kukiona

02Jan 2016
Abdul Mitumba
Nipashe Jumapili
Waliokula fedha maabara kukiona

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imesema itawashughulikia Wakurugenzi wa Halmashauri na watumishi mbalimbali nchini waliofuja fedha za ujenzi wa maabara 10,389 za sekondari za kata nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI,Suleiman Jafo

Mpaka mwezi Novemba mwaka jana, serikali ya awamu ya nne kwa kushirikiana na wanachi ilikamilisha kujenga maabara 5,979 na nyingine 4,410 zilikuwa katika hatua mbalimbali ya ujenzi.
Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo alisema wizara yake itaanzisha zoezi maalum la kukagua miradi hiyo kujiridhisha kama fedha zilitumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema serikali ilitumia mabilioni ya fedha ili kutekeleza agizo wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete la kila shule ya sekondari kuwa na maabara, lakini baadhi ya watumishi walijinufaisha kwa kuongeza gharama ya ujenzi.
Alisema baadhi ya Halmashauri ziliyageuza madarasa kuwa maabara huku gharama halisi zilizotumika zikionyesha kuwa sawa na ujenzi wa jengo jipya.
"Naipongeza serikali ya awamu ya nne kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia ujenzi wa maabara, lakini kuna baadhi ya watendaji wametumia nafasi hiyo kujinufaisha kwa kutumia vibaya fedha za umma, sasa hao serikali hii ya awamu ya tano italala nao mbele," alisema Jafu.
Jafo ambaye ni Mbunge wa Kisarawe, alisema watapita kila shule kufanya ukaguzi kuhakikisha kama maabara zilizozengwa zipo sawa na fedha zilizotumika, na kama wakigundua kuna madudu watawachukulia hatua kali wahusika.
Alisema serikali ya awamu ya tano haina nia ya kuwavunja moyo watendaji wa Halmashauri, bali inataka kuona kila mtu anakuwa na tabia ya uzalendo katika kutekeleza majukumu.
Jafo alisema serikali ya awamu ya tano itaendeleza mazuri ya awamu ya nne kwa kuongeza idadi ya shule, maabara na vifaa vya kusomea na kufundishia.
Aliwataka wafanyakazi wanaosimamia sekta mbalimbali chini ya Tamisemi kutumia mamlaka waliyopewa kwa manufaa ya wananchi na si vinginevyo.
Kauli ya Jafo ni mwendelezo wa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais Magufuli katika kupambana na watu wanaojihusisha na vitendo vya ubadhilifu wa mali za umma.
Katika kutekeleza mapambano hayo, viongozi na watendaji mbalimbali serikalini wamesimamishwa kazi na wengine wamefikishwa mahakamani.
Baadhi ya watendaji wakuu waliosimamishwa ni Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Mohamed Mwinjaka, Kamishna na Mamlaya Mapato (TRA) Rished Bade, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari, Awadh Massawe na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Dk. Edward Hosea.
Wengine ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Diwani Msemo na Mkurugenzi wa Hopaitali ya Taifa ya Muhimbili Dk. Husein Kidanto.
Pia Rais Magufuli alivunja bodi mbalimbali za taasisi za serikali baada ya kubaini hazijafanya kazi ipasavyo.

Habari Kubwa