Wanasiasa wa Zanzibar watangulize maslahi ya taifa na si itikadi za vyama

13Jan 2016
Editor
Nipashe
Wanasiasa wa Zanzibar watangulize maslahi ya taifa na si itikadi za vyama

WAKATI wananchi wa Zanzibar wakiwa wameadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi jana, hali ya kisiasa si shwari kutokana na kauli zilizotolewa na wanasiasa wa huko katika kipindi cha sikukuu.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, katika hotuba yake wakati wa kilele cha maadhimisho hayo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, alisisitiza msimamo wa chama chake wa kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu, ambao ulifutwa baada ya kufanyika oktoba 25, mwka jana.
Dk. Shein aligombea nafasi ya urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo, ambao ulitangazwa kufutwa matokeo yake na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Kauli ya Dk. Shein imekuja siku moja baada ya mgombea kiti cha urais cha Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, kutoa msimamo wa chama chake wa kutaka kuhalalishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25.
Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, alikutana na waandishi wa habari na kusisitiza msimamo wa chama chake wa kupinga kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Mambo yanayotokea Zanzibar ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kwamba yanaibua maswali kwa nini kila ikitokea uchaguzi visiwani humo kunakuwa na hali ya wasiwasi kiusalama.
Wapenda amani walitarajia kuwa katika kipindi hiki cha sherehe za amani kingetumika kupata ufumbuzi wa tatizo la Zanzibar. Lakini kinachoonekana sasa ni kuwa viongozi wa Zanzibar wametanguliza itikadi za vyama vyao badala ya maslahi mapana ya visiwa hivyo.
Kauli za Dk. Shein na Maalim Seif zimetolewa wakati ambao kumekuwa na jitihada za kusaka ufumbuzi la tatizo hilo lakini tofauti na matarajio ya wengi, zinatoa wasiwasi kama ufumbuzi wa tatizo hilo utakapatikana kwa haraka.
Hii si mara ya kwanza kwa hali hiyo kutokea. Hali ya sintofahamu imekuwa ikitokea tangu uchaguzi wa chini ya mfumo wa vyama vingi ulipoanza kufanyika mwaka 1995.
Pamoja na jitihada nyingi za ndani ya nje ya nchi, bado inaonekana wanasiasa wa Zanzibar wameshindwa kuweka misingi ya kuhakikisha watu wa Zanzibar wanachagua viongozi wao kwa amani na utulivu.
Inasikitisha kuona kuwa kila linapotokea suala la uchaguzi Zanzibar, joto la kisiasa hupanda kiasi cha kutishia amani.
Mvutano zaidi huhusisha vyama vya CCM na CUF, ambavyo viongozi wake wamekuwa wakivutana kiasi cha kusababisha sintofahamu miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Hata hivyo, tatizo kubwa la uchaguzi wa Zanzibar limekuwa linasababishwa zaidi na ucheleweshaji wa kutangaza matokeo yake.
Ilitegemewa kuwa kutokana na Zanzibar kuongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa miaka mitano bila shaka ingesaidia kupunguza mivutano lakini hali imekuwa tete.
Ni jambo la kushangaza kuwa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia historia ya kisiasa kujaribu kupandikiza chuki na mgawanyiko miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Mathalan, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakikumbushia siasa za vyama vya zamani vya ASP, ZNP na ZPPP, ambavyo vilikuwa uhasama na mvutano mkubwa katika miaka ya 1950 na 1960 na kuleta mambo hayo katika kipindi hiki.
Hivi kweli ni busara kweli kwa kizazi hiki kuleta siasa za miaka ya 1950 katika Uchaguzi Mkuu unaofanyika mwaka 2015?
Tunatoa mwito kuwepo kwa busara miongoni mwa viongozi wa ZEC, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na viongozi wa CCM na CUF kwa kuweka maslahi ya taifa mbele.
Pia viongozi wa CCM na CUF wanapaswa kuchunga kauli zao ili kutochochea chuki za kisiasa na kuacha demokrasia kuchukua mkondo wake.