Wataka Mwinyi, Mkapa, JK wapunguziwe mishahara

17Jan 2016
Nipashe Jumapili
Wataka Mwinyi, Mkapa, JK wapunguziwe mishahara

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), limesifu kasi ya Rais John Magufuli ya kutumbua majipu, lakini limemwomba ageukie mishahara ya marais wastaafu na kuipunguza hadi nusu ikiwa ni mwendelezo wa hatua zake za kubana matumizi ya fedha za umma.

RAIS MSTAAFU WA AWAMU YA TATU, BENJAMIN MKAPA

Aidha, shirikisho hilo limemtaka Rais Magufuli ajielekeze pia kwenye halmashauri za majiji na miji nchini ambako limesema fedha za miradi ya maendeleo zimegeuzwa hazina mwenyewe.
Rai hizo zilitolewa na Rais wa TUCTA, Gratian Mukoba katika mazungumzo maalumu na Nipashe, kuhusu masuala mbalimbali ya wafanyakazi na mambo ambayo wanatarajia kutoka kwa Rais Magufuli.
Mukoba alisema mishahara wanayolipwa sasa marais wastaafu, Alhaji Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete ni mikubwa wakati walishamaliza utumishi wa umma.
“Rais mstaafu anapata asilimia 80 ya mshahara anaolipwa rais aliye madarakani, sisi TUCTA tunaona huo nao ni ufisadi na tunamuomba Magufuli aipunguze ifike angalau nusu ya mshahara wa Rais aliyeko madarakani,” alisema Mukoba ambaye pia ni rais wa Chama cha Walimu (CWT).
Hakuna taarifa rasmi kuhusu mshahara wa Rais, hata hivyo.
Alisema Rais Magufuli pia anapaswa kupunguza mafao makubwa wanayopata viongozi wa kisiasa kama wabunge, ambayo waliyaweka wenyewe wakiangalia maslahi yao binafsi watakapostaafu lakini yamekuwa mzigo mzito kwa walipa kodi.
Kiinua mgongo cha wabunge baada ya miaka mitano tu ya utumishi ni Sh. milioni 250.
Mukoba alisema hatua anazochukua Rais Magufuli kwa sasa ni kama utekelezaji wa ushauri wa TUCTA ambao wamekuwa wakiutoa miaka mingi iliyopita, ikiwemo kupunguza safari za nje na misafara isiyo na tija.
Alisema shirikisho hilo liliishauri serikali ya wamu ya nne kupunguza idadi ya wajumbe wanaosafiri na viongozi kama Rais nchi za nje ili kuokoa fedha za walipa kodi, lakini iliziba masikio.
“Kasi ya Rais wetu ni nzuri hasa anapobana matumizi ili kufanya vitu vya maana," alisema. "Inatupa moyo kwamba tunakoelekea ni kuzuri zaidi.
"Ila hatujajua kama kasi hiyo itaendelea hivyo hivyo au itafika wakati itapungua.
"Magufuli amethibitisha kwamba tunaweza kubana matumizi na kufanya mambo ya maana hilo halina ubishi.”
Katika kubana matumizi huko, Rais Magufuli aliamuru Sh. bilioni nne zilizokuwa zimetengwa na Hazina kwa matumizi ya sherehe za siku moja ya maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika, zitumike kupanua km nne za barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam.
Aidha, punde baada ya kuzindua Bunge la 11 mjini Dodoma Novemba mwaka jana, Rais Magufuli aliamuru Sh. milioni 230 kati ya fedha zilizokuwa zimetengwa kwa sherehe hiyo, zikanunue vitanda na mashuka kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amepiga marufuku safari holela za nje ya nchi kwa watumishi wa serikali.
Akihutubia katika ufunguzi wa Bunge, Rais Magufuli alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2013 na nusu ya 2014/2015 pekee, safari za vigogo nje ya nchi ziligharimu Sh. bilioni 356.3 fedha ambazo zingeweza kujenga barabara yenye urefu wa Kilomita 400 au kutimiza miradi mbalimbali ya jamii.
Alisema tiketi za ndege pekee ziligharimu Sh. bilioni 183.160, mafunzo ya nje ya nchi Sh. bilioni 68.612 na posho za kujikimu Sh. bilioni 104.552.
Mukoba alisifu hatua ya Rais Magufuli kufuta safari nyingi za nje ya nchi alizozielezea kuwa hazikuwa na manufaa kwa nchi na hatua yake ya kupunguza msusuru wa wajumbe waliokuwa wakisafiri na viongozi ughaibuni.
“Mfano msururu wa viongozi wanakwenda Dubai kwenye mafunzo badala ya kuita wataalamu wawili kutoka huko waje wawafundishe mkiwa hapa hapa ili kubana matumizi," alisema Mukoba.
"Kwa kweli haya anayofanya Magufuli yametukosha na tunaona anafikiri sawa sawa na sisi maana ndiyo maono yetu ya muda mrefu.”
Aidha, alisema ni matarajio ya wafanyakazi kwamba Rais Magufuli atapunguza kodi ya mishahara ya wafanyakazi hadi kufikia chini ya asilimia 10 kama ambavyo alikuwa akiahidi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu uliomwingiza madarakani Oktoba mwaka jana.
Mukoba alisema mfumuko wa bei na kodi kwenye mishahara umekuwa mzigo mkubwa kwa wafanyakazi, hivyo kupunguzwa kwa kodi kunaweza kuwasababishia unafuu wa maisha wafanyakazi wa sekta mbalimbali.
Kuhusu majipu ya kwenye Halmashauri na Manispaa, Mukoba alisema ingawa Rais Magufuli amekuwa na kasi nzuri katika kuwashughulikia wakwepa kodi na watendaji wasiowajibika, majipu ambayo hayajatumbuliwa bado ni mengi hasa kwenye halmashauri na manispaa nchini.
“Majipu ambayo Rais ameyatumbua ni sehemu ndogo tu, bado kuna majipu mengi sana ya kutumbua hasa kwenye halmashauri ambako fedha za walimu zimekuwa zikitafunwa mchana kweupe, huku nako akija ataona mambo ya ovyo ovyo yanayofanywa na viongozi,” alisema Mukoba.
“Mfano Manispaa ya Kinondoni inakusanya Sh. bilioni 40 kwa mwaka na madai ya walimu ni Sh. milioni 500 tu lakini utashangaa kuona mwaka unaisha lakini hela ya kulipa madai mbalimbali ya walimu hawaitengi.
"Ndo maana nasema bado kuna majipu mengi sana huku chini... akimaliza juu ashuke ajionee uozo uliopo huku.”
Mukoba alisema wakurugenzi wengi wa manispaa na halmashauri wameshindwa hata kuwapandisha madaraja walimu tangu mwaka 2013, hali ambayo imewafanya waishi kwa masikitiko na kupunguza ari ya kazi.
Alisema malimbikizo ya madai mbalimbali ya walimu nchini yamefikia zaidi ya Sh. bilioni 67 hivyo alimuomba Rais Magufuli kuwashinikiza wahusika walipe madeni yote ya walimu kama hatua ya kuwafuta jasho na kurejesha ari ya kazi.
“Aliahidi kwamba atakuwa rafiki wa wafanyakazi na sisi tunasubiri tuone namna atakavyowajali,” alisema Mukoba ambaye kwa miaka mingi amekuwa akikwaruzana na serikali kuhusu malimbikizo ya malipo ya walimu.

Habari Kubwa