Watendaji waliotoa vibali vya ujenzi sehemu zisizoruhusiwa waadhibiwe

06Jan 2016
Editor
Nipashe
Watendaji waliotoa vibali vya ujenzi sehemu zisizoruhusiwa waadhibiwe

Serikali jana ilianza kubomoa nyumba ambazo zimejengwa katika sehemu zisizoruhusiwa katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Operesheni hii inatazamiwa kuhusisha nyumba zipatazo 15,000 katika jiji hilo. Hii ni awamu ya pili baada ya ile ya kwanza iliyofanyika Desemba, mwaka jana lakini ikasimama ili kuwapa watu muda wa kuhama. Hata hivyo, operesheni hiyo imesimamishwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutokana na shauri lililofunguliwa mahakamani hapo na baadhi ya waathirika.

Operesheni hii inasimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC). Nyumba mbalimbali vikiwamo vitega uchumi zimewekewa alama ya X kuashiria zinatakiwa kubomolewa. Nyumba 15,000 ni idadi kubwa, ina maana kutakuwa na waathirika wengi wa ubomoaji huo. Tunaelewa nia njema ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanaheshimu sheria za nchi yanapokuja masuala ya ujenzi. Hata hivyo, pamoja na hatua hiyo ya serikali lakini bado kuna mambo mengi ya msingi yanapaswa kushughulikiwa wakati operesheni hii ikiendelea. Ni ukweli kabisa kuwa nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na tatizo kubwa la mipango miji. Mathalani, jiji la Dar es Salaam limeshindwa kuwa na mpangilio ulio bora kutokana na ujenzi holela.

Hata mji wa Dodoma, ambao katika siku za usoni unatakiwa kuwa mji mkuu wa nchi yetu, lakini nao umekuwa ukikabiliwa na tatizo la ujenzi holela. Ukifuatilia historia utagundua kuwa ramani ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa mji mkuu ilikuwa ya mfano wa kuigwa. Nchi kama Nigeria ambayo ilihamisha makao yake makuu kutoka jiji la Lagos kwenda Abuja ilileta wataalamu kuja kujifunza Tanzania. Ni jambo la kushangaza kuona Tanzania imeshindwa kutekeleza azma yake ya kujenga makao makuu katika mji wa Dodoma pamoja na mpango huo kuwapo kwa miaka mingi.

Pia cha kushangaza ni kuwa miundombinu ya miji yetu iko kwenye hali mbaya kutokana na baadhi ya watendaji kutokuwa waaminifu. Wakati serikali ikiendelea na ubomoaji nyumba tulitegemea kuona pia ikiwawajibisha watendaji waliohusika na kutoa vibali kwa watu kujenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Watendaji waliohusika na dhambi hii wanapaswa kuchukuliwa hatua kali kutokana na adha ambayo wanaisababisha katika jamii. Mathalani, kuna vitega uchumi vinavyohusisha kampuni kubwa, hii kwa kiasi kikubwa itaathiri Tanzania katika medani ya kiuchumi ya kimataifa.

Moja ya matatizo makubwa inayokabiliwa nchi yetu ni tatizo la ajira, ambapo serikali imekuwa ikihamasisha uwekezaji vitega uchumi ili kuongeza nafasi za kazi. Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa baadhi ya wawekezaji wamejikuta wakitapeliwa na maofisa wa ardhi waliowapa vibali huku wakifahamu ujenzi umefanyika katika maeneo yasiyoruhusiwa. Kitendo hiki kitaichafua taswira ya nchi yetu katika medani ya kimataifa na kufanya watu waamini kuwa Tanzania sio sehemu salama ya kufanya uwekezaji.

Ili haki itendeke ni lazima serikali ichukue hatua kali dhidi ya watendaji wote waliohusika na kutoa vibali kwa watu kujenga katika maeneo yasiyoruhusiwa. Ukweli unabaki kuwa kuna wananchi walio wengi wanaathirika na operesheni hii kutokana na makosa yaliyofanywa na watendaji wa serikali wasiokuwa waadilifu. Hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta nidhamu lakini pia haki itakuwa imetendeka. Pia serikali lazima iboreshe mfumo wake wa utoaji wa ardhi ili kumaliza tatizo hili la ujenzi holela. Aidha, ili kuendana na kipindi hiki cha sayansi na tekinolojia, ni bora serikali ikaanzisha mfumo wa kidijitali ili kuondoa tatizo hili. Pia serikali iendeleze mpango wake wa kupima maeneo nchi nzima ili kuepusha wananchi kuingia kwenye matatizo ya kununua maeneo yasiyoruhusiwa kujengwa.

Habari Kubwa