Yanga hii haponi mtu

22Jan 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Yanga hii haponi mtu
  • *** Tambwe alipiga 'hat-trick' yake ya pili msimu huu, timu hiyo ya Jangwani ilipopata ushindi mnono na kuing'oa Azam kileleni baada ya saa 24.

HAPONI mtu! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana kikosi cha Yanga kuonyesha kwamba kimepania kutetea ubingwa wake kilipoichapa timu kibonde ya Majimaji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kupata ushindi mkubwa zaidi msimu huu.

Ushindi huo mnono uliifanya timu ya mabingwa hao mara 25 wa Bara ifikishe pointi 39 baada ya mechi 15, ikiing'oa Azam kileleni kutokana na tofauti ya magoli baada ya timu hiyo Chamazi kurejea kileleni juzi iliposhinda 2-1 ugenini dhidi ya Mgambo.
Kiungo Mzimbabwe Thaban Kamusoko ndiye aliyefungua karamu ya mabao ya Jangwani dakika nne tu baada ya kipenga cha kwanza akifumua shuti kali la mguu wa kulia nje ya boksi. Lilikuwa goli la tano kwa nyota huyo ambaye ni miongoni mwa wachezaji watatu wa Yanga waliokosa penalti msimu huu.
Mzimbabwe mwingine, Donald Ngoma alifunga goli lake la tisa msimu huu na la pili kwa Yanga jana baada ya kupewa pasi murua ndani ya boksi na Kamusoko dakika ya pili baada ya mapumziko.
Dakika tatu kabla ya saa ya mchezo, kinara wa mabao, Amissi Tambwe alitupia la tatu kwa shuti kali akiitendea haki kazi nzuri ya Ngoma.
Mrundi huyo alirejea tena kambani katika dakika ya 72 akiifungia timu yake bao la nne, safari hii akijitwisha kichwa mpira wa krosi kutoka winga Deus Kaseke ambaye pia alitoa pasi ya mwisho ya goli la Kamusoko.
Straika huyo wa zamani wa Simba na Vital'O ya kwao Burundi, alijihakikishia kuondoka na mpira baada ya kupiga 'hat-trick' yake ya pili msimu huu alipomchambua kwa shuti la mguu wa kulia ndani ya boksi Kipa Bora wa msimu wa 2012/13, David Burhan dakika sita kabla ya kipenga cha mwisho cha refa Jimmy Fanuel.
Tambwe ambaye anaongoza safu ya wafumani nyavu hatari akiwa na magoli 13, alipiga 'hat-trck' yake ya kwanza msimu huu waliposhinda 4-0 dhidi ya Stand United na kuungana na Kiiza na Ibrahim Ajibu ambao kila mmoja ana 'hat-trick' moja.

MWADUI 2-1 KAGERA
Baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Mbeya City mjini Mbeya Jumamosi, kikosi cha Jamhuri Kihwelo 'Julio' kilizinduka na kushinda 2-1 nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, shukrani kwa mabao ya Jerryson Tegete dakika ya 22 (goli lake la tano msimu huu) na Fabian Gwanse dakika ya 52 wakati wageni walifutwa machozi na Babu Ally aliyefumua shuti kali la mguu wa kulia ndani ya boksi dakika chache kabla ya mechi hiyo kumalizika.

A/SPORTS 0-0 MTIBWA
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, baada ya kuishika Azam FC kwa sare ya 1-1 Dar es Salaam Jumamosi usiku, African Sports walipata pointi moja nyingine baada ya kutofungana na mabingwa wa 1999 na 2000, Mtibwa Sugar.

Habari Kubwa