Yanga nayo imuombe radhi Niyonzima

24Jan 2016
Adam Fungamwango
Lete Raha
Yanga nayo imuombe radhi Niyonzima

ZILIANDIKWA makala nyingi za kuipongeza Yanga kwa hatua ilizochukua kwa mchezaji wake, Haruna Niyonzima.

Haruna Niyonzima

Ilidai kuvunja mkataba na mchezaji huyo baada ya kuchelewa kurejea kwenye kikosi cha timu hiyo alipopewa ruhusa kwenda kuitumikia timu yake ya taifa ya Rwanda kwenye michuano ya Chalenji iliyomalizika mwishoni mwa mwaka jana nchini Ethiopia.
Kwanza ilimsimamisha kwa muda usiojulikana.
Utetezi wake wa kuja nchini akiwa na plasta ngumu (P.O.P) akidai aliumia haukusaidia.
Wiki kadhaa baadaye uongozi wa Yanga uliita waandishi wa habari na kutangaza rasmi kuvunja mkataba wa kiungo mahiri.
Licha ya kutangaza kuvunja mkataba ilimtaka Niyonzima alipe kiasi cha dola 71,000 ambazo ni karibu Sh. Milioni 150 za Kitanzania.
Ikaenda mbali zaidi na kuzipigwa mkwara timu zinazomtaka kuwa ni lazima kwanza zilipe hizo pesa ndiyo ziweze kumchukua.
Kikubwa zaidi uongozi wa Yanga ulisema kuwa Niyonzima ni mkosefu mzoefu na mara kwa mara amekuwa na tabia ya kuchelewa kurudi kila anapoitwa kwenye timu ya taifa au anaporejea kwao. Hili kwa Niyonzima linaeleweka.
Tukaandika makala ya kuupongeza uongozi huo kwani adhabu kama hiyo itakuwa fundisho kwa wachezaji wengine na pia italinda nidhamu.
Binafsi nilindika makala ya kupongeza uongozi kwa sababu ya kuamua kiume kwani pamoja na umahiri wake wote akiwa uwanjani, na licha ya kuwa ni mchezaji anayeongoza kwa kupendwa kwenye klabu hiyo, lakini wakaamua kuvunja naye mkataba.
Nikasema ni jambo la kuigwa na klabu nyingine katika kurudisha nidhamu ya wachezaji ambao kwa sasa wengi wao wameonekana kuwapanda vichwani viongozi kwa sababu ya udhaifu wa kuchukua hatua.
Lakini wasiwasi wangu ukawa kwenye kipengele cha kuzitahadharisha timu zitakazomchukua kuwa ni lazima kwanza ziilipe Yanga mamilioni ya shilingi.
Nikasema maana ya kuvunja mkataba ni kwamba pande zote mbili zipo huru, na hata kama kuna madai basi wanabaki kuwa madai huwezi kumzuia mchezaji asiende popote.
Kipengele hicho kilinipa wasiwasi kama ni kweli Yanga imedhamiria na hili ililotamka au inatuchezea sinema?
Hofu yangu haikuwa ya bure, tayari uongozi wa Yanga umekuja tena mbele ya kamera za waandishi wa habari, safari hii ikiwa na mchezaji tuliyeaminishwa kuwa ni mtovu wa nidhamu aliyekubuhu, akiomba radhi na kutaka kurudishwa kundini.
Uongozi wa Yanga nao sasa umeonekana kugeuka na kuachana na maneno makali yaliyokuwa yakisemwa juu ya mchezaji huyo, na sasa amesamehewa na kutaka kurudishwa kundini.
Mimi sipingi viongozi wa Yanga kumsamehe Niyonzima kwa sababu, anayekosa ni binadamu na anayesamehe pia ni binadamu, ila ninachoshangaa ni jinsi viongozi wa klabu hiyo walivyomnanga mchezaji huyo awali na kuwaaminisha wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa hafai, msaliti na anaweza kupandikiza mbegu mbaya ya utovu wa nidhamu ndani ya kikosi.
Kwa nini viongozi wa Yanga wasingemsikiliza wakati uleule aliporejea na (P.O.P) kutoka Rwanda na baadaye kumtaka aombe radhi?
Kama wangekaa naye na kusikiliza utetezi wake wakati ule, nadhani mkutano ule na waandishi wa habari uliotumika kuvunja mkataba na Niyonzima ungekuwa ni wa yeye kuomba radhi na kusamehewa kama ulivyofanyika huu wa pili.
Najuliza, kulikuwa na sababu gani ya kutomsikiliza wakati ule na kufanya maamuzi, lakini baadaye ndiyo wakaamua kumsikiliza na kumfanyia mkutano wa kuomba msamaha? Walikurupuka? Au kuna nguvu nyuma ya pazia ambayo imeamuru Niyonzima arejeshwe?
Kutokana na hili lililotokea, uongozi wa Yanga unaweza kutoaminika tena na wanachama na mashabiki wao wanapotoa matamko yao.
Lakini pia viongozi wa Yanga wanatengeneza matabaka, huku baadhi ya wachezaji nao wanaweza kufanya kama mwenzao na kama wakiadhibiwa wanaweza kuhoji mbona Niyonzima alisamehewa?
Najua kuwa Niyonzima aliikosea klabu ya Yanga na ameomba radhi, lakini kwa hili pia uongozi wa Yanga pia umekosea na inabidi umuombe radhi mchezaji huyo, wanachama na mashabiki wake.

Habari Kubwa