Yanga yaanika 'madudu' ya Tiboroha

25Jan 2016
Nipashe
Yanga yaanika 'madudu' ya Tiboroha

Siku moja tu baada ya Jonas Tiboroha kutangaza kujiuzulu kwenye nafasi ya Katibu Mkuu wa Yanga, uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani umeibuka na kudai msomi huyo alifanya 'madudu'.

Jonas Tiboroha.

Tiboroha mwenye PhD katika Michezo, alitangaza kuachia ngazi juzi kwa madai ya kubanwa na majukumu ya mwajiri wake, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa klabu hiyo haijaridhishwa na utendaji wa Tiboroha na uongozi ulimtaka aachie ngazi kabla hawajafikia uamuzi wa kumfukuza.

Sanga alidai kuwa moja ya mambo ambayo hayakufanyiwa kazi kwa weledi ni sakata la kiungo wa timu wa kimataifa Mrwanda Haruna Niyonzima.

Sanga alidai kuwa Tiboroha alionekana kulitetea Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapokuja suala la maslahi ya klabu hiyo.

"Tiboroha alificha ukweli kwa Kamati ya Nidhamu ya klabu juu ya barua za ruhusa na taarifa mbalimbali za mchezaji huyo alizokuwa akizituma klabuni hapo wakati akiwa kwa Rwanda," alisema Sanga.

Aliongeza kuwa Yanga imekamata barua na nakala mbalimbali zinazonyesha katibu huyo alikuwa na mpango wa kutaka kumpeleka nchini Uturuki mshambuliaji wa timu hiyo, Donald Ngoma kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini humo.

Sanga alidai kuwa uongozi wa klabu hiyo ulipata taarifa kutoka kwa mtaalam huyo wa michezo akiutaarifu kuwa alikuwa na matatizo ya kifamilia, lakini akasafiri kwenda Ghana kuhudhuria kongamano la FIFA huku Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ikiwa haina taarifa.

"Pia aliiazima klabu ya BDF ya Botswana kiasi cha Dola za Marekani 5,000 bila ya uongozi wa Yanga kuhusishwa na mpaka sasa fedha hizo hazijarudishwa, mbaya zaidi anatengeneza maneno kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano (Isaac) Chanji anafanyia mizengwe aondolewe," aliongeza.

Tiboroha jana hakupatikana kueleza juu ya tuhuma hizo zilizoelezwa na viongozi wa juu wa klabu hiyo.

Katika hatua nyingine, Yanga inatarajia kutangaza siku ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo baada ya kumpata mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uchaguzi ndani ya wiki moja.

Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alitangaza kujiuzulu kutokana na kubanwa na mambo ya kifamilia.

Habari Kubwa