Zanzibar hali tete

12Jan 2016
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Zanzibar hali tete
  • Hoja 10 za Maalim kupinga uchaguzi wa marudio

HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar, inazidi kuwa tete baada ya aliyekuwa mgombea uras kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, jana kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mazungumzo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupinga kurudiwa kwa uchaguzi.

Katibu Mkuu wa CUF. Maalim Seif Shariff Hamad

Aidha, Maalim Seif ameonyesha kutokuwa na imani na mazungumzo ya kutafuta mwafaka yanayoendelea visiwani humo.

Badala yake, amemtaka Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati mzozo huo akisema kurudiwa kwa uchaguzi si suluhisho la mgogoro huo bali kutachochea zaidi vurugu.

Alisema anaamini kwamba Dk. Magufuli atafanya hivyo na siyo kusubiri kutumia wadhifa wake kama Amiri Jeshi Mkuu kutuma askari Zanzibar kutafuta amani pindi iatakapovunjika.

Akionyesha kutokuwa na imani na mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina yake na Rais Ali Mohammed Shein na Marais wastaafu, Maalim Seif alisema kwa wiki mbili sasa amekuwa Ikulu Zanzibar akiandika barua kukumbushia kuandikwa kwa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vinane vilivyokwisha fanyika mpaka sasa bila mafanikio.

Maalim Seif aliyetumia saa 1:30 kuzungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, alisema hakuna hoja wala msingi wa kikatiba na kisheria ya uchaguzi kurudiwa.

Alisema kiini cha mzozo wa kikatiba na kisheria visiwani Zanzibar, uliotokana na kufutwa, changamoto zake na namna ya kuutatua.

Maalim Seif alisema kurudiwa kwa uchaguzi kunaweza kuleta maafa makubwa kama yale yaliyotokea mwaka 2001, na kuwaonya wanachama wa CCM kuwa waangalifu.

Mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar uliibuka Oktoba 28, mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo kwa madai ya kuwapo kwa dosari nyingi.

Tangu kufutwa kwa uchaguzi huo ni taribani siku 72 sasa huku Rais Dk. Shein, akiendelea kuiongoza Zanzibar, lakini CUF inadai kutoitambua serikali iliyopo madarakani.

Maalim Seif alisema hoja ya kurudiwa uchaguzi haina uhalali, wala msingi na ni chachu ya kuiweka nchi katika utawala usiokuwa halali na kusababisha fadhaa kubwa kwa wananchi.

“Hatuoni msingi wowote wa kurudia uchaguzi. Kama CCM wanang’ang’ania urudiwe, wafanye uchaguzi hata mara 100 lakini haitashinda kama uchaguzi utakuwa wa haki,” alisema Maalim Seif.

Alisema kurudiwa kwa uchaguzi kunaweza kuzaa fujo na vurugu katika nchi na kupeleka mzozo mkubwa zaidi wa kikatiba na kisheria.

KINACHOJIRI VIKAO VYA KAMATI
Maalim Seif alisema katika vikao vinavyoendelea hivi sasa ambavyo vimefikia vinane, bado Rais Dk. Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wanang’ang’ania kurudia uchaguzi huku wakimtetea kwa nguvu Mwenyekiti wa Zec, Jecha.

Alisema na yeye amekuwa akisisitiza haja ya kuheshimu matakwa ya kikatiba na kisheria na maamuzi ya wananchi wa Zanzibar yaliyofanywa Oktoba 25, mwaka jana.

Alieleza kuwa kutokana na kutofikiwa kwa muafaka pamoja, walikubaliana kuandaa taarifa ya pamoja ambayo ilielezwa kwamba ingeandaliwa na Katibu wa vikao ambaye ni Rais Dk. Shein, lakini hadi sasa ni zaidi ya wiki mbili zimepita hakuna kikao chochote kilichoitishwa.

Alisema ameandika barua kuhimiza kufanyika kwa kikao cha kupokea taarifa hiyo na kuipitisha, lakini bado Rais Dk. Shein amesema wanahitaji muda.

Alisema wakati mazungumzo ya kupata muafaka yakiendelea, CCM wanapita katika kambi za Jeshi wakiwalaumu askari kwa uamuzi wa kuipigia kura CUF.

Alisema wanachama hao wa CCM pia wanawatishia askari wakisema serikali ikiingia madarakani rasmi wataadhibiwa.

KWA NINI UCHAGUZI USIRUDIE
Maalim Seif alieleza kuwa hoja ya kurudiwa kwa uchaguzi haina msingi na haiwezekani kutekelezwa.

Alisema mbali na matokeo ya uchaguzi ya Urais Zanzibar ambayo yanaonyesha wazi kuwa CCM ilishindwa, vile vile hata matokeo ya Urais wa Muungano kwa upande wa Zanzibar, yalionyesha hivyo hivyo.

Alisema hatua ya Mwenyekiti wa Zec, Jecha kufuta uchaguzi haikuwa halali na ina kasoro nyingi kikatiba na kisheria.

"Kurejea uchaguzi ni sawa na kuhalalisha kitendo batili alichofanya Jecha," alisema.

Maalim Seif alisema kurejea uchaguzi bila kupata ufumbuzi juu ya uhalali wa uamuzi wa Mwenyekiti wa Zec, ni sawa na kuhalalisha kitendo hicho na kutoa ruhusa kuwa huko mbele anaweza kurudia tena.

Alisema matamko ya waangalizi wa uchaguzi na namna tuhuma za kasoro za uchaguzi zilivyoibuliwa na Mwenyekiti wa Zec, haziwezi kuwashawishi wapigakura kulikuwa na kasoro katika uchaguzi.

Maalim Seif alisema kurejea uchaguzi ni sawa na kuihukumu Zec yote kuwa ina makosa wakati makosa yalitendwa na mtu mmoja.

UCHAGUZI UKIRUDIWA WATAFANYA NINI
Maalim Seif alisema kuwa suala hilo siyo la kisera hivyo hataliamua peke yake bali kutaitishwa vikao na kufanya maamuzi na kisha kutoa tamko la kichama.

ALICHOZUNGUMZA NA MAGUFULI
Alisema kuwa bado ana imani na Rais Dk. Magufuli katika kutatua mgogoro huo kwa kuwa aliwahi kufanya naye mazungumzo na kumweleza kuwa ahakikishe amani na utulivu vinapatikana visiwani Zanzibar.

Alisema alichoelezwa na Rais Magufuli ndicho alichoelezwa na Rais Dk. Shein kuhakikisha mgogoro unapatiwa ufumbuzi haraka.

NAMNA YA KUTATUA MGOGORO
Maalim Seif alisema ili kulinda misingi ya Katiba ya Zanzibar chini ya kifungu cha 119(1) na (10) na kujenga uhalali na heshima ya Zec, ni lazima Mwenyekiti wa Zec, Jecha ajiuzulu au kusimamishwa kazi.

Alisema pia Zec chini ya Makamu Mwenyekiti na Makamishna waliobaki, wamalize kutangaza matokeo ya urais kwa majimbo tisa ambayo yalishahakikiwa na kumalizia kuhakiki matokeo ya urais kwa majimbo 14 yaliyobaki na kutangaza matokeo.

Lingine ni Rais Dk. Magufuli aongoze juhudi za kutatua mgogoro huo awe Mwenyekiti wa kamati.

Alisema pia uongozi wa vyama vya CUF na CCM ufanye mazungumzo ya haraka ya kukamilisha taratibu za kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar chini ya mshindi wa uchaguzi wa Urais wa Zanzaibar.

Alisema mambo yoyote yanayohitaji kurekebishwa katika mfumo wa uchaguzi ili kuondoa kasoro zilizopo kwa nia ya kuimarisha mfumo huo kwa chaguzi zozote na baadaye, ni vyema yakawekewa muda maalum wa kujadiliwa na kupata muafaka.

KWA NINI ANAMUAMINI MAGUFULI
Maalim Seif alisema anamwamini Rais Magufuli kwa kuwa mazungumzo aliyowahi kufanya naye Ikulu jijini Dar es Salaam alionyesha wazi alikuwa anataka mzozo umalizike kwa haraka na kila upande uridhike.

Alisema Rais Magufuli ni mtu ambaye anapenda amani na hayuko tayari kutumia majeshi kuweka amani sawa.

Alisema hata akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atafanya kazi wa Rais Dk. Magufuli kwa ukaribu zaidi.

Alisema Katiba ya Zanzibar na Muungano zinatambua uwapo wa serikali mbili na kila serikali ina mamlaka na sheria zake.

Alisema katiba hizo zote mbili hazijaeleza kuwa serikali zote mbili zitaundwa na chama kimoja, hivyo Rais Magufuli atafanya kazi kwa Katiba ya Muungano na yeye atafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

“Nitaendelea kushirikiana na Serikali ya Muungano, hatutakuwa na Serikali ya Zanzibar kamili bali itakuwapo serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Maalim Seif.

KUITWA MSALITI
Maalim Seif alisema anajiamini na akichukua maamuzi huwa anayetekeleza mara moja, alisema hana hoja ya kuficha mambo bali anaongozwa na maslahi ya nchi kwa Wazanzibar wote.

“Kama kuna maneno yanayosemwa kuwa mimi ninawasaliti CUF ni uzushi, sijawahi kukubalina na CCM katika vikao vinavyoendelea, kama mnabisha mtaona mwisho wake,” alisisitiza Maalim Seif.

MATOKEO YA UCHAGUZI WALIYONAYO
Maalim Seif alieleza kuwa katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, CUF walijiandaa kikamilifu kwa kuweka mawakala kila kituo pamoja na kupata nakala ya matokeo katika vituo vyote vya Unguja na Pemba.

Alidai kuwa kwa matokeo ya Muungano, mgombea wa CCM, Dk. Magufuli alipata kura 194,317(46.5%) huku Edward Lowassa akipata kura 211,033(50.50%) na idadi ya wapigakura walikuwa 417,882.

Alidai kuwa kwa matokeo ya Urais Zanzibar, Dk. Shein alipata kura 182,011 (46.28%) na Maalim Seif kura 207,847 (52.84%).

YEYE NI NANI KWA SASA
Maalim Sef alieleza kuwa kwa sasa yeye siyo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kwa kuwa muda wa kuongoza nafasi hiyo ulimalizika tangu Novemba 10, mwaka jana.

Alisema toka siku hiyo, alishatoa maelezo kutopangiwa kazi yoyote ya kiserikali.

Alisema kwa sasa anatumia magari ya serikali na ulinzi wa serikali kwa sababu anadhani akijiondoa moja kwa moja serikali atawaachia mwanya viongozi wa CCM kufanya uchakachuaji mkubwa na kuwafanya wafuasi wa CUF kupata shida.

KAULI YA SERIKALI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Abood, alisema utaratibu uliopo ni kuwa uchaguzi wowote ukifutwa lazima urudiwe na hakuna njia ya mkato mbali na hiyo.
Alisema Zec ndiyo waliofuta matokeo ya uchaguzi na ndiyo wenye jukumu la kutangaza lini utarudiwa.

Alisema Zec ina mamlaka kikatiba na haiwezi kuingiliwa na mtu yoyote na kwamba hakuna muujiza mwingine unaoweza kutokea kupata viongozi licha ya kurudiwa.

“Mimi nitaheshimu uamuzi wa Tume na ninachojua uchaguzi lazima utarudiwa, hivyo tunaisubiri Zec itangaze siku na tarehe ya kurudiwa uchaguzi,” alisisitiza Abood.

Kuhusu serikali kuwapa vitisho askari, Abood alisema suala hilo halina ukweli kwa kuwa haki ya kupiga kura ni ya kila mtu, na jambo hilo ni siri, hivyo serikali haiwezi kujua nani kaipigia kura CUF na nani kaipigia CCM.

CCM YAMJIBU
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema Maalim Seif anapaswa aeleze kama ana mpango wa siri wa kuchafua amani visiwani Zanzibar.

Alisema hakuna mtu yeyote anayetaka kuivunja amani ya Zanzibar bali CCM walichokisema kwa wanachama wake ni kujiandaa na uchaguzi mpya baada ya kauli ya Zec kutolewa kuwa matokeo yamefutwa.

Alisema ugomvi baina yake (Maalim Seif) na Zec, asiuhamishie CCM.

Kuhusu CCM kushindwa hata mara 100 endapo uchaguzi utarudiwa, Vuai alihoji: Kwa nini Maalim Seif anakataa kurudia kama anajua atashinda hata mara 100?."

Habari Kubwa