Yanga haikamatiki

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 06:27 PM Feb 18 2024
Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya (kushoto), pamoja na straika wa timu hiyo, Clement Mzize wakishangilia katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jana. Yanga ilishinda mabao 3-0.
PICHA: YANGA SC
Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya (kushoto), pamoja na straika wa timu hiyo, Clement Mzize wakishangilia katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jana. Yanga ilishinda mabao 3-0.

MABAO ya viungo, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua, yaliiwezesha Yanga kuondoka na ushindi wa mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jana.


Kiungo mkabaji, Mudathir alifunga mabao mawili katika mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili na sasa amefikisha mabao sita msimu huu huku goli lingine la kiungo mshambuliaji, Pacome, raia wa Ivory Coast, pia likimfanya kufikisha idadi kama hiyo.

Matokeo hayo yanawafanya mabingwa hao watetezi, Yanga kuendelea kujiimarisha kileleni katika msimamo wa ligi wakifikisha pointi 43 na kuiacha KMC ikiwa nafasi ya tano na pointi 12 kibindoni.

Beki wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage, alitoa pasi mbili za mwisho za mabao hayo na kumfanya awe na 'asisti' nne katika ligi mpaka sasa.

Yanga ilitimiza msemo unaosema biashara asubuhi, ilipoandika bao la kwanza katika sekunde ya 54 kupitia Mudathir ambaye kwa siku za karibuni amekuwa kama 'moto'.

Baada ya kuona wanaanzia mpira nyuma na kupasiana kwa karibu bila tahadhari na wakati mwingine kumrudishia kipa, Maseke, nyota wa Yanga waliwazingira KMC na Clement Mzize, alifanikiwa kuupokonya akiwa karibu na lango, mpira akampelekea mfungaji ambaye alipiga shuti kali lililowababatiza mabeki, ukamrudia Stephane Aziz Ki, ambaye naye alijaribu, lakini kipa aliupangua, ukaenda kuangukia tena kwa kiungo huo kabla ya kuupachika wavuni kiulaini.

Baada ya bao hilo la 'asubuhi' wachezaji wa KMC walionekana kuchanganyikiwa na kufanya makosa mengi katika eneo lao la hatari na kama wachezaji wa Yanga wangekuwa makini wangemaliza kipindi cha kwanza wakiwa na mabao zaidi ya matano yale waliyofunga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Agosti 23, mwaka jana.

Mzize peke yake alikosa mabao ya wazi, dakika ya tisa alipobaki yeye na kipa, lakini akapiga shuti dhaifu lililoishia mikononi kwa Maseke, dakika ya 11, akiwa yeye na Maxi Nzengeli, wakikabiliana na kipa wa KMC, lakini mpira ukaenda nje, dakika ya 26, akiwa yeye na nyavu, akapiga nje, na dakika ya 34 akiwa pia jirani ya lango tupu akapiga pembeni.

Kwa upande wake, Pacome, alikosa bao dakika ya 14, shuti lake likidakwa na Maseke.

KMC ilifanya mashambulizi yake dakika ya 10, wakati Awesu Awesu, alipotandika shuti kali lililowababatiza mabeki wa Yanga, kabla ya kudakwa na kipa, Djigui Diarra, aliyekuwa langoni kwa mara ya kwanza baada ya kurejea kutoka katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), akiitumikia Mali.

Dakika ya 27, Fred Tangalu, akiwa nje ya eneo la hatari alipiga shuti kali lililotoka sentimeta chache langoni kwa Yanga, huku Diarra akiwa amechelewa kufika eneo la tukio.

Kipindi cha pili, KMC ilimtoa kipa wake, Maseke ambaye alionekana hayupo vizuri, akigombana na mabeki wake na nafasi yake ikachukuliwa na Denis Richard, lakini haikuwa dawa.

Mudathir alipachika bao la pili dakika ya 53, alipoutokea mpira wa krosi iliyopigwa na Kibabage, wakati mabeki wa KMC wakiusubiri kuokoa, mfungaji alitoka nyuma yao na kuukwamisha wavuni kirahisi tu.

Dakika sita baadaye, Pacome alisawazisha makosa yake kwa kuiandikia Yanga bao la tatu, akiunganisha krosi ya Kibabage kutoka wingi ya kushoto.

Ni kama KMC walizinduka baada ya mabao hayo matatu kwa sababu walianza kumiliki mpira, hasa Awesu ambaye alionekana yuko katika kiwango cha hali ya juu.

Straika mpya wa Yanga, Joseph Guede, aliyesajiliwa hivi dirisha dogo la usajili, alikosa mabao mawili ya wazi, moja akigongesha mwamba alipopiga kichwa mpira uliotoka kwa Musonda.