Katibu CCM ahadharisha NGO zinazoisemea serikali

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:57 AM May 27 2024
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, David Mramba.
Picha: Julieth Mkireri
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, David Mramba.

KATIBU wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, David Mramba, amesema mashirika yanayoanzishwa kwa ajili ya kuisema serikali na kuhakikisha hayatumiki kama kichaka cha maovu.

Mramba alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki alipokutanisha mashirika yasiyo ya kiserikali yenye mrengo mmoja wa kuisemea CCM na serikali, akisisitiza “wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli”.

Katibu huyo alisema yapo baadhi ya mashirika yamegeuka kichaka cha kuhifadhi uovu. Kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha malengo ya uanzishwaji na kuchafua serikali na chama tawala, jambo ambalo halipendezi kwa jamii.

Mramba pia alisema ni muhimu mashirika hayo kufanya kazi kwa manufaa ya taifa na si kujinufaisha huku akionya wanaojiingiza kwenye migogoro ya wagombea wa nafasi mbalimbali katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

"Fanyeni kazi za taasisi zenu kwa bidii na kuepuka ubadhirifu mkizingatia lengo la kuanzishwa kwake, msiingie kwenye taasisi kufuata uteuzi," alisema Mramba.

Katibu huyo alisema ni muhimu kufuata taratibu za kisheria kwa kusajiliwa ifikapo Juni mwaka huu ili watambulike kwa mujibu wa sheria za nchi na kuheshimu taratibu zilizowekwa.

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Morogoro, Zagina Shanang, alikumbusha wanachama wa chama hicho kuhakikisha katika uchaguzi ujao wanachagua viongozi ambao wana shughuli za kuwaingizia kipato.

Shanang pia alionya mashirika hayo dhidi ya tabia za ubaguzi na kutengeneza makundi ya wagombea huku akisisitiza wanawake kupewa nafasi zaidi za uongozi.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo ulioambatana na mafunzo, Mohamed Mzimba, alimpongeza Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo kwa kukutanisha mashirika hayo na kujadili kwa pamoja mambo ya kukijenga chama na taifa kwa ujumla.