Tembo Warriors yasaka nafasi kombe la Dunia

By Saada Akida , Nipashe
Published at 07:16 AM May 25 2024
Timu ya Taifa ya Mpira wa miguu ya watu wenye Ulemavu jioni ya Mei 23, 2024 wakiingia Uwanja wa Petrosport kujiandaa na mechi ya wapinzani wao Ghana kufuzu nusu fainali ya michuano ya Afrika 'AAFCON' inaliyoanza Mei 18, 2024 nchini Misri.
Picha: Mtandaoni
Timu ya Taifa ya Mpira wa miguu ya watu wenye Ulemavu jioni ya Mei 23, 2024 wakiingia Uwanja wa Petrosport kujiandaa na mechi ya wapinzani wao Ghana kufuzu nusu fainali ya michuano ya Afrika 'AAFCON' inaliyoanza Mei 18, 2024 nchini Misri.

BAADA ya kufungwa na Ghana katika hatua ya robo fainali ya Afrika (AAFCON), Kocha Mkuu wa Tembo Warriors, Salvatory Edward ameweka wazi kubadilisha malengo ya mashindano hayo na sasa anatafuta nafasi kwa ajili ya kucheza kombe la Dunia 2026.

Tembo Warriors walifungwa 4-1 na Ghana katika mchezo wa hatua ya robo fainali uliopigwa uwanja wa PetroSport, nchini Misri.

Tanzania leo inashuka dimbani tena dhidi ya mabingwa Angola kuendelea kuisaka nafasi adhimu ya kushiriki Kombe la dunia 2026 kuiwakilisha Tanzania na Afrika katika nafasi saba, zinazoenda kuiwakilisha kombe la Dunia.

Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Salvatory alisema mechi ya Ghana ilikuwa ya ushindani mkubwa, wachezaji walipambana lakini haikuwa bahati kwao.

Alisema licha ya kufungwa kwenye hatua ya robo fainali lakini bado wapo katika mashindano na wanajiandaa kwa mechi zijazo kutafuta nafasi ya kwenda kucheza kombe la Dunia.

“Malengo yetu yamebadilika baada ya kuhitaji kombe la Afrika, sasa tunahitaji kujipanga vizuri katika mechi zetu, mashindano magumu na tunapambana na matumaini yetu kuwa sehemu ya timu saba ambazo tutaenda kuiwakilisha nchi katika kombe la Dunia, 2026,” alisema Salvatory.

Nahodha  wa Tembo Warriors, Shadrack Hebron alisema wamepoteza mechi ya robo fainali na wana sahau matokeo hayo na kuweka nguvu zao kwenye mechi zijazo kutafuta nafasi ya kombe la Dunia.

“Bado hatujakata tamaa, tumepoteza mechi ya robo fainali lakini bado hatujaondolewa kwenye mashindano, sasa tunapambana kutafuta nafasi ya kufuzu na kwenda kucheza kombe la Dunia mwakani,” alisema Shadrack.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dk. Suleiman Serera amewataka wachezaji na benchi la ufundi (Tembo Worriors) kuyachukulia matokeo waliyopata katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Ghana.

"Tukiendelea kulia na kusikitika wala haitaturudishia kitu, tunachotakiwa kujua mwana michezo  yeyote anayekuja kwenye mashindano anakuja kwa ajili ya kushinda, hakuna anayekuja kwa ajili ya kupoteza,"alisema

Aliwataka kutokuwa na simanzi bali  waende  kuboresha nafasi wanazozipata na  kutumia katika  mechi zingine, mechi za Afrika kipimo sahihi na kupambana kutafuta nafasi ya kufuzu kombe la Dunia.

Brigedia Generali Ismail Shajack Ismail mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Misri amewataka wachezaji na benchi la ufundi kwenda kujipanga vilivyo kupambania timu saba zitakazoshiriki Kombe la Dunia.