Aliyoyasema Rais Samia kuhusu Sokoine liwe somo kwa viongozi

By Mhariri Mtendaji , Nipashe Jumapili
Published at 04:27 PM Apr 14 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan.

Juzi, taifa liliadhimisha kumbukizi ya miaka 40 tangu aliyekuwa Waziri mkuu, Edward Sokoine alipofariki dunia. Hafla ya kumbukumbu hiyo ambayo Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi, ilifanyika nyumbani kwa kiongozi huyo shujaa, aliyetumikia taifa kwa uaminifu, Monduli Juu mkoani Arusha.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, viongozi waandamizi wa serikali,  dini na wastaafu pamoja na familia ya Sokoine, Rais Samia aliwataka viongozi serikalini kusimamia maagizo wanayopewa bila kutetereka na kuiga uthubutu wa kiongozi huyo. 

Rais Samia alisisitiza kwamba wateule wake hao wanapaswa kutekeleza majukumu yao bila kuyumbishwa na shinikizo kutoka kwa mtu au kikundi cha watu bali wasimame katika misingi na kutenda haki. Alisema somo ambalo Watanzania hususani viongozi wanalipata kutoka kwa Hayati Sokoine ni kuwajibika kama alivyokuwa akifanya kwa kuwa alisimamia misingi ya haki na mienendo na matendo yake yalionyesha mfano bora wa uongozi.

Katika kuiga mfano huo, Rais Samia alisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kusimamia uamuzi unaotolewa na serikali kuhusu jambo lolote na kwamba ukishatolewa (uamuzi), kinachofuata ni utekelezaji tu, hivyo viongozi lazima wafanye hivyo kama ilivyoafikiwa bila kuyumbishwa na ikiwezekana wawe mfano kwa wengine.

Rais Samia aliwakumbusha viongozi na watanzania kwa ujumla kuwa Hayati Sokoine alikuwa mpenda maendeleo kutokana na nyakati tofauti kusisitiza watu kufanya kazi huku akichukia uvivu, uzembe na watu kujilimbikiza mali. Sokoine katika uhai wake alipambana na uhujumu uchumi, biashara za magendo na ulanguzi kiasi cha kuchukiwa na watu waliokuwa wakijihusisha na vitendo hivyo. 

Kutokana na tabia na hulka hiyo, alisema licha ya kwamba ni miaka 40 tangu alipoaga dunia, Sokoine bado anaishi kutokana na matendo yake na ni mfano wa kuigwa katika uongozi. Pia alibainisha kuwa serikali yake inafuata nyayo zake katika kuwaletea maendeleo wananchi kwa kupeleka huduma mbalimbali kama afya, elimu, maji na miundombinu.

Kuna msemo kwamba huchukua miaka mingi, hata karne, kupatikana kwa mtu mwenye haiba, hulka na tabia ya mtu aliyesimama katika nafasi fulani ikiwamo ya uongozi na alikuwa mfano katika jamii husika. Ndivyo ilivyo kwa Sokoine ambaye ni vigumu kupatikana mtu wa aina yake katika matendo na mwenendo kwenye uongozi.

Sokoine alipambana na dhuluma, uzembe, uvivu na umangimeza na aliwataka viongozi kutenda haki pamoja na kusimamia na kutekeleza yale wanayokubaliana. Hakuwa na simile hata kidogo dhidi ya mtu aliyeshindwa kutekeleza majukumu yake. Alikuwa mtu wa kuthubutu na mfuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na serikali. 

Kutokana na tabia yake hiyo, aliwahi kusimama kidete na kumtaka naibu waziri mmoja afukuzwe kwa kushindwa kutekeleza maagizo aliyopewa. Sokoine alimwambia aliyekuwa Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa alikuwa tayari kujiuzulu iwapo naibu Waziri huyo asingefukuzwa. Nyerere alikubaliana naye na hatimaye kumfukuza.

Kwa mfano huo tu, inaonyesha alikuwa mtu wa namna gani katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli mbalimbali hasa maagizo yaliyotolewa kwa viongozi kutoka kwa walio juu yao. Hali hiyo ni tofauti na sasa kwani wako baadhi ya viongozi katika ngazi mbalimbali hawatekelezi majukumu yao na hata kufanya kazi kwa mazoea. 

Hayo yamebainika wakati wa ziara za Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo mbalimbali ambako hukutana na vilio vya wananchi kuhusu kutotatuliwa matatizo yao na viongozi wanaomwakilisha Rais huko. Hatua hiyo imesababisha mara kadhaa Rais kuwatumbua au kufanya utenguzi wa wateule hao. Hiyo ni dalili kwamba watu hao hawatimizi wajibu wao.

Kama alivyosema Rais Samia kwamba uthubutu wa Sokoine linapaswa kuwa darasa kwa viongozi wa sasa kwenye nafasi zao, ni vyema kila mtu akatekeleza wajibu wake kwa kusimamia na kufuatilia masuala mbalimbali kwa lengo la kuipaisha Tanzania katika viwango vya juu kimaendeleo.