Kenya kupeleka kikosi cha polisi Haiti kwa usaidizi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:45 AM May 20 2024
Machafuko yatokanayo na makundi ya wahalifu nchini Haiti.
Picha: Guerinault Louis/Anadolu/picture alliance
Machafuko yatokanayo na makundi ya wahalifu nchini Haiti.

SERIKALI ya Kenya imesema kikosi chake cha polisi kitapelekwa nchini Haiti lengo likiwa ni kuongoza ujumbe wa kimataifa wa kusaidia kupambana na magenge ya wahalifu.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Kenya, Korir Sing´Oei, wakati akizungumza na waandishi habari muda mfupi kabla ya Rais William Ruto kuanza safari ya kwenda Marekani kwa ajili ya kufanya mkutano na Rais Joe Biden mnamo Mei 23, 2024.

Julai mwaka jana Kenya iliahidi kupeleka kikosi cha askari 1,000 nchini Haiti kulisaidia taifa hilo la kanda ya Karibia kurejesha utulivu baada ya kuandamwa na kiwingu cha ghasia za makundi ya wahalifu.

Hata hivyo mpango huo wa Kenya umekumbwa na misukosuko kufuatia kufunguliwa kesi kadhaa za kuupinga. Hapo kabla mahakama moja nchini humo ilisema mpango huo ni kinyume na katiba na kwamba haupaswi kutekelezwa hadi pale Kenya na Haiti zitakapofikia mkataba wa pamoja wa usalama.

Serikali iliharakisha kupatikana mkataba huo uliosainiwa mnamo Machi Mosi, mwaka huu.