Majina matatu yatawala kiti cha Mwenezi wa CCM

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:42 PM Apr 02 2024
John Mongela, Amos Makalla na Lengai Ole Sabaya.
PICHA: MAKTABA
John Mongela, Amos Makalla na Lengai Ole Sabaya.

LEO ni miaka mitatu na siku 14 tangu Rais Samia Suluhu aingie madarakani. Uteuzi na utenguzi wake wa viongozi umekuwa unatikisa serikalini na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndani ya uongozi wake, kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi ndani ya CCM, huku nafasi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo ikiguswa karibu kila yanapofanyika.

Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, makada watatu wa chama hicho wameteuliwa kushika nafasi hiyo, lakini hakuna aliyedumu. Kiti hicho kwa sasa kiko wazi baada ya Paul Makonda kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa katika mabadiliko yaliyotangazwa usiku wa manane kuamkia Jumapili ya Pasaka.

Ni mabadiliko yaliyoibua hisia tofauti huku kukiwa na minong’ono kwa wanaotajwa kushika nafasi hiyo. Wakuu wa Mikoa waliotenguliwa usiku wa kuamkia Pasaka, John Mongella na Amos Makalla pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya wanatajwa kuwa na nafasi ya kukalia kiti cha Katibu wa Uenezi CCM.

Rais Samia aliapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha Rais wa Tano, Dk. John Magufuli kilichotangazwa Machi 17, 2021. Mnamo Aprili 30, 2021, Halmashauri Kuu ya CCM katika kikao maalum ilipitisha kwa kauli moja Rais Samia kuwa mgombea pekee wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Wakati huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humprey Polepole ndiye aliyeujulisha umma juu ya uamuzi huo, na Mkutano Mkuu Maalum ulipitisha Samia kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, akichukua nafasi ya Hayati Dk. Magufuli.

Mara baada ya kuingia madarakani, mwenyekiti huyo alianza kuisuka safu ya uongozi ndani ya chama hicho, kwa kumteua Daniel Chongolo ambaye kabla alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano chini ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ikiwa chini ya Nape Nnauye, akitokea kwenye nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Halmashauri Kuu pia ilimteua Christina Mndeme kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara huku Abdalah Juma Sadala akiendelea kuhudumu nafasi hiyo upande wa Zanzibar.

Pia nafasi ya Polepole aliyoitumikia tangu Desemba 13, 2016  akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Nape, ilikabidhiwa kwa Shaka Hamdu Shaka huku Katibu wa Uchumi na Fedha akiwa Frank Hawasi.

Ikumbukwe kuwa Polepole aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge Novemba 29, 2020. Aprili 14, 2022, Rais Samia alimteua Polepole kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi na mwaka uliofuata, alimhamishia Cuba ambako yuko hadi sasa akihudumu katika nafasi hiyo.

Shaka alidumu kwenye nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi minane na siku 13, hadi Januari 14, 2023, Halmashauri Kuu ya CCM ilipomteua Sophia Mjema kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, huku Rais Samia akimteua Shaka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ambako anahudumu hadi sasa.

Mjema alidumu kwenye nafasi hiyo kwa miezi tisa na siku nane, kisha Paul Makonda kuteuliwa na Halmashauri Kuu kushika wadhifa huo aliodumu nao kwa siku 162, akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Chongolo, akiwa ni Katibu Mkuu wa CCM wa 11 alijiuzulu nafasi hiyo baada ya kashfa mbalimbali alizohusishwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Machi 9, mwaka huu aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Chongolo alidumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka miwili miezi minane na siku 15, kisha Halmashauri Kuu baada ya kuridhia barua ya kujiuzulu ya Chongolo ilimteua Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kushika wadhifa huo anaoendelea nao hadi sasa.

Katika kipindi hicho, Sekretarieti ya CCM imekuwa inapitia mabadiliko mbalimbali ambapo hivi karibuni, Rais Samia alimteua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Anamringi Macha, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Kati ya waenezi waliopita chini ya uenyekiti wa Rais Samia, Makonda ndiye aliyedumu kwa muda mfupi zaidi, huku kukiwa na mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuwa kupewa kwake nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ni kupanda ngazi au kushuka ngazi huku kukiwa na maswali mengi ya kilichosababisha kuondolewa katika Sekretarieti ya CCM licha ya kuonekana kufanya vizuri kwenye ziara zake mikoani kuimarisha chama.

Katiba mabadiliko ya juzi, mbali na Makonda, Rais alimteua Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Fakii Lulandala kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, huku Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Gilbert Kalima akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga.

WANAOTAJWA

Kwenye makundi sogozi ya WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii, majina ya viongozi watatu yameonekana kutawala mijadala ya wanaotajwa kuwa na nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Makonda ndani ya Sekretarieti ya CCM.

Katika mjadala huo, taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunusi, inarejewa kwa kuangalia majina ya viongozi ambao uteuzi wao umetenguliwa, lakini kukawa na maelezo kwamba watapangiwa majukumu mengine.

Katika taarifa hiyo wapo ambao wameelezwa uteuzi wao umetenguliwa, lakini aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mongella na yule wa Mwanza, Makalla ilielezwa watapangiwa kazi nyingine.

AMOS MAKALLA

Ana mambo yanayoshabihiana na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kuanzia uswahiba wa masomoni IDM Mzumbe, wana umri unaofanana, miaka 52 na kihistoria ni makada kindakindaki waliokulia kwenye chama, hata wakawa vigogo wa UVCCM wakiwa na nyendo za kisiasa pamoja.

Walitumikia pamoja kwenye uongozi wa UVCCM chini ya Mwenyekiti Nchimbi kisha baadaye walipokomaa kisiasa na umri, wakapitia vyeo tofauti, Makalla wakati fulani akirejeshwa kwenye Sekretarieti ya CCM, akiwa kwenye Idara ya Fedha, kama alivyotumikia UVCCM.

Mwenzake Nchimbi akazungukia kwenye utendaji wa kiserikali zaidi, akianzia Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) iliyokuwa ajira yake ya kwanza, hata akakwea kwenye ukuu wa wilaya, ubunge uliompa uwaziri na baadaye akiibukia balozi katika nchi kadhaa kabla ya kurejea tena katika chama.

Mizunguko kama hiyo ilikuwa kwa Makalla, kuna wakati hakuonekana katika nafasi hizo, ubunge na kisha Naibu Waziri (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, pia Maji na Umwagiliaji) kabla ya kurejea tena kwenye ukuu wa mkoa na sasa rasmi kuna tetesi za kurejea tena sebuleni katika chama wakiwa makada walioiva kama ilivyomtokea swahiba wake Nchimbi.

Hata kitaaluma, wana-Mzumbe hao, Balozi Nchimbi ambaye ngazi yake ya kwanza kitaaluma ni utawala wa umma, Makalla amezama kwenye uhasibu, lakini kwa pamoja waliporejea shuleni, shahada zao za pili ni za usimamizi wa biashara, unasaba wao na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia, naye ni mwana-Mzumbe wa darasa moja na Balozi Nchimbi, lakini kamtangulia kwa miaka mingi.

OLE SABAYA

Mbali na Makalla na Mongella, orodha ya wanaotajwa kurithi mikoba ya Makonda pia ina jina la Ole Sabaya, mzaliwa wa Sambasha, Arumeru, mkoani Arusha mwaka 1986, ambaye anatoka familia ya kifugaji ya Loy Thomas Sabaya ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.

Kabla ya kushinda kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Sabaya aliwahi kuwa mkuu wa wilaya kama ilivyokuja kuwa kwa mwanawe Lengai baadaye.

Jina la Lengai Ole Sabaya limeibua mjadala zaidi kutokana na historia yake; ana Shahada ya Sayansi katika Hisabati. Katika siasa amewahi kuwa diwani pekee wa CCM mwaka 2015 katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, kipindi hicho upinzani uliiangusha CCM. Zilikuwa enzi za "mafuriko ya Edward Lowassa".

Mwaka 2017, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha na mwaka mmoja baadaye akateuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani kilimanjaro.

Uteuzi huo ulifanya Ole Sabaya kuwa mkuu wa wilaya mdogo zaidi miongoni mwa walioteuliwa, akipangiwa kituo cha kazi cha Hai, eneo ambako ndiko jimbo lililokuwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.

Ole Sabaya alianza kulalamikiwa hadharani na Mbowe mwaka 2019 kwa madai ya kuwarubuni wenyeviti 20 wa serikali za vijiji waliohamia CCM ghafla wakitokea CHADEMA.

Baada ya hapo, Ole Sabaya alianza kuandamwa na tuhuma mbalimbali, hasa za kundi la wafanyabiashara na baadhi ya watu waliodai anakandamiza upinzani ili kumdhibiti Mbowe.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai alipotangaza Mbowe kuangushwa katika kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 2020, Mbowe na CHADEMA walimlalamikia hadharani Ole Sabaya wakieleza kupanga matokeo kabla ya kura kupigwa.

Ole Sabaya pia alifanya matukio mbalimbali yaliyoibua hisia za kitaifa, ikiwamo kukamata fedha bandia Sh. milioni 800 pamoja na tukio na kuvunja kampuni ya upatu ya Qnet iliyolalamikiwa kutapeli walimu na wastaafu.

Mei 13, 2021, Rais Samia alimsimamisha kazi Ole Sabaya kama mkuu wa wilaya kupisha uchunguzi na tarehe 4 mwezi Juni mwaka huo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kujibu mashtaka mbalimbali.

Tarehe 15 mwezi Oktoba mwaka 2021, Ole Sabaya alihukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu, kwa kosa la kuiba fedha taslimu 390,000 toka kwa Diwani wa Sombeni, Bakari Msangi.

Miezi saba baadaye, Mahakama Kuu ilifutilia mbali hukumu hiyo kwa kile ilichokieleza kwamba ushahidi wa mashahidi ulipishana sana kuhusu kiini cha tukio.

Mwezi mmoja baadaye Sabaya alishinda kesi nyingine ya uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mfawidhi Patricia Kisinda iliyofunguliwa wakati anakamatwa.

Sabaya alihamishiwa Moshi kukabiliana na mashtaka mengine ambayo baadaye yaliondolewa mahakamani.

Tarehe 5 mwezi wa nne mwaka 2023 baada ya kukaa jela kwa siku 672, Ole Sabaya aliachiwa huru na toka wakati huo ameonekana hadharani mara moja mnamo tarehe terehe 4, 2024 katika Kanisa la Ebeneza Restoration, akimshukuru Mungu.

Katika mjadala wa warithi wa Makonda CCM, Ole Sabaya anatajwa kama kijana mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja, kusimamia anachokiamini na kutokuwa na sifa ya ndumila kuwili, tabia ambayo wanasiasa wengi wanatajwa kuwa nayo.

Kuna wanaokwenda mbali zaidi na kudai kuwa kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kitakutana Aprili 4, mwaka huu, kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi na walioteuliwa kwenda kwenye majukumu serikalini.

Inadaiwa kuwa kwa sasa Rais Samia anasuka safu ya kumsaidia na kukisaidia chama kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Oktoba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2025, ikiwa ni uchaguzi wake wa kwanza akiwa Rais.

Wakati Polepole ndiye Katibu Mwenezi aliyempokea Rais Samia ambaye baadaye akawa Mwenyekiti wa CCM Aprili, 2021, baadhi ya watangulizi wa nafasi hiyo kihistoria ni: Kingunge Ngombale-Mwiru, Omari Ramadhani Mapuri, John Mgesa, Jackson Msome, John Chiligati, Aggrey Mwanri, Christoper Ole Sendeka na Nape.