Musoma vimebaki vijiji 27 ambavyo havina zahanati

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:21 AM May 28 2024
Baadhi ya wakazi  wa kijiji hicho wakichangia nguvukazi zao kwenye ufyatuaji wa matofali ya ujenzi wa zahanati ya kijiji chao.
Picha: Mpigapicha Wetu
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakichangia nguvukazi zao kwenye ufyatuaji wa matofali ya ujenzi wa zahanati ya kijiji chao.

WAKAZI wa Musoma Vijijini mkoani Mara, wapo katika uboreshaji wa huduma za afya kwa kushiriki ujenzi wa zahanati na sasa vimebaki vijiji 27 kati ya 68 ambavyo havina zahanati.

Katika ujenzi huo, wanachangia nguvukazi, fedha taslimu na vifaa vya ujenzi kwenye miradi yao ya maendeleo inayobuniwa na kuanza kutekelezwa na wao, ikiwamo ya ujenzi huo wa zahanati na shule mpya.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amesema, jimbo hilo lina kata 21, vijiji 68 na vitongoji  374 huku kukiwa na zanahati 29 zinazotoa huku 25 kati ya hizo zikiwa ni za serikali.

"Wanavijiji wako katika ujenzi wa zahanati mpya 16 kwa kutumia michango ya fedha na vifaa vya ujenzi kutoka katika kaya na pia michango mingine kutoka kwangu mbuge," amesema Prof Muhongo.

Amefafanua kuwa michango mingine ni kutoka kwa madiwani na viongozi wengine wa vijiji na kata zenye miradi ya ujenzi, baadhi ya  wazaliwa wa vijiji na kata zenye miradi ya ujenzi, huku  serikali kuu nayo ikichangia ukamilishaji wa zahanati hizo.

"Miongoni mwa zahati zinazojengwa ni ya Kijiji cha Kaburabura. Nilifanya harambe kwa ajili ya fedha na vifaa vya ujenzi wa zahanati hiyo, Taarifa ya matokeo ya harambee hiyo ilishatolewa, na inapatikana kwenye Tovuti ya Jimbo la Musoma Vijijini," amasema.

Amesema, wadau wa maendeleo wanakaribishwa kuchangia ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Kaburabura, na kwamba wanaweza kiutuma fedha za mchango kwenye aaunti ya Kijiji katika Benki ya NMB Na: 30302300684. Jina la Akaunti: Kijiji cha Kaburabura.