ACT-Wazalendo bado walia na Sheria ya Uchaguzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:14 AM May 20 2024
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman.
Picha: Maktaba
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman.

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema Sheria ya Uchaguzi ya Kupiga Kura ya Mapema inapaswa kuondolewa kwa sababu ndiyo chanzo cha vurugu na mauaji katika Uchaguzi wa Zanzibar.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa mikoa miwili ya kichama Kaskazini A na B Unguja wa chama hicho, katika mkutano wa kukamilisha ziara, kuwashukuru wanachama kumaliza uchaguzi mkuu wa viongozi.

Amesema Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuweka utaratibu wa askari wa ulinzi na usalama kupiga kura siku moja kabla ya uchaguzi mkuu ni sheria ambayo imeleta matatizo makubwa katika kufikia misingi ya uchaguzi huru na haki visiwani Zanzibar.

“Katika maridhiano ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa mambo mawili tumesema hayana mjadala la kwanza ni kura ya siku mbili hili lazima liondoke. Tulisema hatuwezi kupoteza muda kuja mezani kujadili iwepo au isiwepo kwa sababu imeletwa kwa nia ya kufanya dhuluma, kudanganya na kuiba uchaguzi,” amesema.

Ameongeza: “Leo hatuwezi kujadili kwamba wizi huu uendelee au usiendelee na hili kama halijatekelezwa hatutokubali na ndiyo chanzo cha vurugu na kuua watu.”  

Amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kama sheria hiyo haitoondolewa, chama hicho hakitokubali kwa sababu imetungwa kwa misingi ya kuvuruga haki ya demokrasia na inaruhusu udanganyifu kufanyika katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Aidha, amesema kabla ya ACT kukubali kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuna mambo ya msingi walikubaliana ikiwamo serikali kuhakikisha inafanya mabadiliko makubwa katika muundo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ikiwamo mfumo wa upatikanaji wa makamishna na sekretarieti ya tume hiyo.

Amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 lazima kila mwananchi mwenye haki apewe cheti cha kuzaliwa na gharama za kupata cheti hicho ziondelewe, ili kila mwananchi aweze kupata haki yake ikiwamo kitambulisho cha mzanzibari mkaazi, ambacho ndiyo msingi wa kuandikishwa katika daftari la wapigakura la Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Amesema mambo hayo ni haki kwa kila mwananchi na kwa mujibu wa makubaliano, yanapaswa kutekelezwa kwa muda mfupi ili kila mwananchi kupata fursa ya kuchagua au kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Othman amesema kama hayo hayatatekelezwa, hawatokuwa na sababu ya kubaki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu dunia na taasisi za kimataifa itawashangaa kuendelea kuwamo katika serikali hiyo ambayo imeshindwa kuweka misingi ya haki na demokrasia.

Hata hivyo, amesema kamati ya uongozi ya ACT Wazalendo imeshawasilisha msimamo wake kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya  Muungano juu ya mambo ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya ACT Wazalendo kuamua kuwamo au kujitoa katika SUK.

Amesema kutokana na kuendelea kusuasua kwa utekelezaji wa mambo waliyokubaliana kamati ya uongozi wa chama hicho unatarajiwa kukutana mwezi huu, kufanya tathmini kabla ya kutoa uamuzi wa kuendelea kuwemo katika serikali hiyo au kujiondoa.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Ismail Jussa, amesema chama kimeandaa mkakati wa kuhakiki wanachama na wafuasi nyumba kwa nyumba ili kujua idadi yao, ikiwemo walioandikishwa na ambao bado ili kuweka kumbukumbu sahihi kabla ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, alisema mchakato huo utafanyika mwaka huu.