ACT yatishia kuiburuza TAMISEMI kortini

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:32 AM Jun 13 2024
 Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kinakusudia kuishtaki Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) mahakamani ili kuzuia hatua za maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea sasa.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Novemba, mwaka huu, na utahusisha kuchagua wenyeviti wa vitongoji, vijiji, mitaa na wajumbe wake, ikiwa ni mwaka mmoja kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao husimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema sheria mpya za uchaguzi zimetoa mamlaka kwa INEC kusimamia uchaguzi huo lakini wanashangaa TAMISEMI kutaka kufanya kazi hiyo. 

"Kwa mujibu wa kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024, tume imepewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji. 

“Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024 inasema: ”Kwa kuzingatia matakwa ya ibara 74 (6) na 75 na 78 za Katiba, Tume itakuwa na majukumu: (C) kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika sheria itakayotungwa na bunge,” alisema. 

Kwa  mujibu wa katibu mkuu huyo, kitendo inachotaka kufanya TAMISEMI hakikubaliki kwa sababu ni batili na kinavunja sheria za nchi. 

"Jana (juzi) tumepata barua kutoka TAMISEMI ya kutualika kuhudhuria kikao cha kutoa maoni ya rasimu ya kanuni zitakazosimamia uchaguzi huo wa serikali za mitaa. Tutakwenda  kwenye kikao hicho lakini si kwa ajili ya kwenda kutoa maoni bali kwenda kuiambia isimamishe mara moja mchakato unaoendelea nao wa maandalizi ya uchaguzi huo kwa sababu ni batili na unavunja sheria za nchi," alisema Shaibu. 

"Hatua hii ya TAMISEMI kupora madaraka ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ni kinyume cha sheria za uchaguzi. Inatia  doa kubwa falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan na inapaswa kulindwa na wadau wote wa demokrasia nchini," alisisitiza.  

Alisema tayari wamezungumza na asasi za kiraia kuhusu kusudio hilo la kuishtaki TAMISEMI kwa kuingilia kazi ya INEC. 

"Na kama tunaona asasi hizo zinachelewa, tumejipanga wenyewe kwenda Mahakama Kuu na tayari chama kimeshaanza kujipanga kwa ajili ya hili," alisema Shaibu. 

Pia alisema kwenye kusudio lao hilo la kuishtaki TAMISEMI, chama hicho kitaandaa kikao maalum na kuvialika vyama vingine vya siasa kuweka msimamo wa pamoja juu ya kuzuia ofisi hiyo kusimamia uchaguzi huo wa serikali za mitaa. 

"Kutokana na hali inayoendelea na kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, chama chetu kitaandaa kikao maalum na kuvialika vyama vingine vya siasa kuweka msimamo wa pamoja juu ya kuzuia TAMISEMI kusimamia uchaguzi huu,"alisema Shaibu. 

Aidha, Shaibu alisema chama hicho kinataka wajumbe wote wa zamani wa iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuondolewa ili kupisha wajumbe wengine wapya watakaopatikana kulingana na matakwa ya sheria mpya za uchaguzi. 

Alisema wajumbe walioko katika tume hiyo hawatokani na mabadiliko yaliyofanyika ya sheria za uchaguzi, hivyo wanatakiwa kuondoka ili wateuliwe wajumbe wengine wapya.