Aliyesababisha ajali ya Katibu Tawala K’njaro asakwa

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:18 AM Jun 20 2024
Ajali ya Katibu Tawala K’njaro iliyotokea jana na kusababisha kifo chake pamoja na dereva wake.
Picha: Mtandao
Ajali ya Katibu Tawala K’njaro iliyotokea jana na kusababisha kifo chake pamoja na dereva wake.

MAKACHERO wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro wanamsaka Godlisten Kileo, dereva wa lori la kusafirisha nishati safi ya gesi, aliyesababisha ajali iliyoua watu wawili, akiwamo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Dk. Tixon Nzunda (56).

Kileo, aliyekuwa akiendesha lori aina ya scania, lenye namba za usajili T 655 ABY alitoroka Juni 18 mwaka huu, baada ya kusababisha ajali hiyo katika eneo la Mjohoroni-Palestina, Kata ya KIA, Wilaya ya Hai, wakati kiongozi huyo akiwahi msafara wa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango na ujumbe wake.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi, mkoani humo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Simon Maigwa, licha ya chanzo cha ajali hiyo kuendelea kuchunguzwa, polisi imeanzisha msako wa kutamfuta dereva huyo aliyetoroka baada ya ajali.

Alisema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa gari namba T 655 ABY aina ya scania, mali ya kampuni ya Orange Gas, kushindwa kulimudu gari lake na kwenda kugonga gari lingine.

Ajali hiyo iliyohusisha lori aina ya scania na toyota landcruiser V8 (GXR), lenye namba za usajili STM 7476, ilisababisha vifo viwili, cha Dk. Nzunda na dereva wake, Alphonce Edson (54).

Marehemu Dk. Nzunda, alikuwa akielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kumpokea Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango na ujumbe wake.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akitangaza taarifa za kifo cha Dk. Nzunda, alisema Dk. Nzunda na dereva wake walipoteza maisha, majira ya saa 8:30 mchana katika eneo la Mjohoroni (Palestina), Wilaya ya Hai.

Dk. Nzunda wakati wa uhai wake, aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Machi 16, 2023.

Vilevile, Februari 28, 2021, Hayati Dk. John Magufuli aliyekuwa Rais, alimteua Dk. Nzunda kuwa Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI.