Askofu anayedaiwa kujinyonga kuzikwa kwa taratibu za kikanisa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:00 AM May 20 2024
Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Joseph Bundala.
Picha: Maktaba
Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Joseph Bundala.

MWILI wa Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist Tanzania (MCT), Joseph Bundala, anayedaiwa kujinyoga hadi kufa katika ofisi yake ndogo iliyopo kwenye kanisa hilo, Ipagala jijini hapo, unatarajiwa kuzikwa leo kama taratibu za uchunguzi wa kifo chake uliombwa na familia zitakamilika.

Aidha, Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Samwel Nyanza, ametangaza kufungwa kwa kanisa la MCT, Ipangala kwa siku 40, ambako tukio hilo lilitokea. 

Akizungumza kwenye ibada maalumu iliyofanyika kwenye Kanisa la MCT Ihumwa, Makamu Askofu Mkuu Nyanza, alisema kanisa linatarajia kumzika kiongozi huyo kwa taratibu za kikanisa.

“Tangu jana yameibuka mambo mengi sana watu wanahoji kwa hili lililotokea sisi tunafanyaje na tunafahamu kuwa kuua na kujiua ni dhambi, lakini jana (juzi) tumejadiliana sana na tumeona tutamzika kwa mujibu wa taratibu zote za kanisa hayo mengine tunamwachia yeye na Mungu wake,” alisema Askofu Nyanza.

Askofu huyo aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wanachopitia kwa kuwa kila jambo linalotokea ni mpango wa Mungu.

“Huu unaweza kuwa ni mpango wa Mungu anataka kutukumbusha kuna mahali tumekosea hivyo kifo hiki kiwe sehemu ya sisi kulijenga kanisa upya, lakini kama kanisa inatupasa tuingie kwenye toba tumwombe sana Mungu atusimamie.

“Na kama tutashikana basi katika hili tutatoboa, lakini kama tutazubaa tutashindwa moja kwa moja na nimekuwa nikipokea ujumbe wa simu kutoka sehemu mbalimbali kuna ambao wanatupa pole, lakini wapo ambao hawatutakii mema hivyo tunapaswa kuwa imara zaidi ya wakati mwingine ili kulijenga kanisa letu,” alisema.

Kadhalika, aliwataka waumi kuwaombea viongozi wao wa dini ili kuondokana na tatizo la afya ya akili ambalo kwa kiasi kikubwa ndilo linachangia watu kufikia uamuzi mbaya kama huo.

“Afya ya akili ndiyo inaweza kufanya hiki kutokana na mizigo ya mambo ambayo viongozi wa dini wamebeba kutoka kwa waumini wao unakuta watu wana ugomvi unaletwa kanisani, mtu ana njaa linaletwa kanisani na mambo mengine kama hayo,” alisema.

Kuhusu kufungwa kwa kanisa la Ipagala, alisema waumini wataendelea kusali, lakini watafanya ibada zao nje hadi siku 40 zitakapoisha ndipo wataliweka wakfu na kuanza kutumika tena.

Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Allen Sisso, alisema ratiba ya mazishi itatolewa baada ya taratibu za kitabibu ambazo zinaendelea kufanywa na familia kuhusu uchunguzi wa nini hasa kimemuua kiongozi huyo wa kiroho.

“Watu wanaongea mambo mengi sana lakini sisi kama kanisa bado hatujatoa kauli yetu, tunasubiri uchunguzi ambao unafanywa na familia majibu ya kitabibu yatakayotoka ndipo na sisi tutatoa tamko letu kuhusu kifo cha Askofu wetu mkuu,” alisema Askofu Sisso.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Alchelaus Mutalemwa, akizungumzia tukio hilo Mei 17, mwaka huu, alisema Jeshi la Polisi linachunguza tukio hilo la Askofu huyo ambaye ni mkazi wa Ihumwa jijini hapa.

“Tukio hilo liligundulika Mei 16, 2024 majira ya saa moja usiku katika mtaa wa Meriwa, Dodoma ndani ya ofisi yake iliyopo katika kanisa hilo.”

Alisema uchunguzi wa awali katika eneo la tukio, umekutwa ujumbe unaoeleza sababu za kujinyonga ni madeni na mgogoro uliopo katika uendeshaji wa shule binafsi.

Aidha, dada wa marehemu, Veronica Alexandra alisema wanataka uchunguzi wa tukio hilo kwa kuwa Mei 16, aliwasiliana na kaka yake na kumwambia anapokea simu za vitisho na kwamba akili yake imefika mwisho na baadaye jioni alipokea taarifa za kifo chake.