Bashungwa awatoa hofu wananchi wanaotumia vivuko vya Kigamboni- Kigogo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:18 PM May 28 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewatoa hofu Wananchi wa mkoa wa Dar es salaam wanaotumia usafiri wa vivuko eneo la Kigamboni -Magogoni juu ya taharuki kuhusu huduma inayotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.

Akizungumza leo jijini hapa, Waziri Bashungwa amesema "Niwatoe wasiwasi Wananchi wa Dar es Salaam pamoja na kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa hakukuwa na sababu ya kutengenezwa. Lakini sisi tunaofahamu yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki."

Ameeleza kuwa sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwa ajili yakupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, Bashungwa amesema kuwa tayari ameikutanisha TEMESA na Kampuni ya AZAM Marine na kujadili namna bora yakushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni - Kigamboni.