Bil. 12/- kukijanisha Jiji Dodoma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:38 AM Jun 12 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza katika kikao cha pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo pamoja na Viongizi waandamizi wa Wizara hizo (hawapo pichani) kujadili mradi wa kukijanisha Jiji.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza katika kikao cha pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo pamoja na Viongizi waandamizi wa Wizara hizo (hawapo pichani) kujadili mradi wa kukijanisha Jiji.

SERIKALI imesema Sh. bilioni 12 zitatumika katika utekelezaji wa mradi wa kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kijani.

Kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kupanda miti na maua katika hifadhi za barabara ili kutunza mazingira na kupendezesha mandhari ya jiji hilo.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alisema hayo jaja jijini hapo katika kikao cha pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Selemani Jafo. 

Mradi huo wa Green Solution Project (GSP) unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambayo inafadhili mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa Jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 112.3. 

“Naamini timu za wataalamu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Ujenzi na taasisi zake zikishirikiana na kujadili suala la utunzaji wa mazingira hususan katika Jiji la Dodoma, zitakuja na mikakati bora ya utekelezaji wa mradi  huu,” alisema.

 Bashungwa alisema kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo katika jiji la Dodoma utafungua mawanda mapana kwa serikali kutafuta wadau wa maendeleo watakaoshirikiana nayo kukijanisha maeneo mbalimbali nchini.  

Aidha, Bashungwa alimwagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kusimamia Wakala wa Barabara (TANROADS) kuandaa usanifu na upembuzi yakinifu ambao hautaathiriwa na mabadiliko na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ikiwamo upanuzi wa barabara ambao umekuwa ukisababisha ukataji wa miti ambayo imepandwa  hivi karibuni. 

Naye Waziri Jafo aliipongeza Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS kwa upandaji miti na kuitunza hususan katika barabara Chimwaga - Ihumwa Junction jijini Dodoma.

Dk. Jafo alisema serikali ina mpango wa kukutana na wamiliki na wawekezaji wa maeneo yaliyo pembezoni mwa barabara ili kuweka mkakati wa pamoja wa upandaji miti na bustani za maua ili kuendelea kukijanisha nchi.  

Ofisa Mazingira Mwandamizi kutoka TANROADS, Julius Luhuro, alisema taasisi hiyo itaendelea kukijanisha hifadhi za barabara kwa barabara zilizopo na zinazojengwa katika maeneo mengi nchini hususan Dodoma na kusisitiza kuwa mkakati huo ni endelevu wenye lengo la kuhifadhi mazingira.