Biteko atoa angalizo viongozi kutoheshimu mihimili iliyopo

By Elizabeth John ,, Ibrahim Joseph , Nipashe
Published at 08:40 AM May 27 2024
Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko, amewataka viongozi kuheshimu utaratibu wa mihimili iliyowekwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Dk. Biteko alielekeza hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Mji Njombe.

Alisema nchi inaongozwa na Katiba, muhimili mmoja hauruhisiwi kuingilia majukumu ya muhimili mwingine badala yake yote inafanya kazi kwa nia moja ya kuleta ustawi wa wananchi.

"Tuheshimu vyombo vyetu vya sheria, tufuate sheria kwenye maisha yetu. Nchi hii inaongozwa na Katiba na tumegawanya majukumu. Serikali ina majukumu yake, mahakama ina majukumu yake na Bunge lina majumuku yake, isitokee muhimili mmoja ukataka kuingilia majukumu ya muhimili mwingine," alionya.

Dk. Biteko alielekeza kuwa viongozi waliopo waheshimu utaratibu wa mihimili iliyopo na waache kuingilia vyombo vingine vya uamuzi kwa kutoa matamko kwa wananchi.

Pia alitaka wananchi kuacha misimamo iliyopitiliza wakati timu ya mawakili itakapokuwa inawasikiliza na badala yake wafuate ukweli.

"Maandiko yanasema ukijua kweli itakuweka huru, nawe utakuwa huru kwelikweli na mawakili simamieni ukweli mtapokuwa mnasikiliza watu hawa watakaokuja kwenu," alisema Dk. Biteko.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ya Haki Jinai ambayo lengo lake ni kuboresha mfumo wa upatikanaji haki kwa umma nchini.

"Tume ile ilikuja na mapendekezo, iliona mambo mengi ndani ya jamii ambayo migogoro mingi imo kwenye jamii, miongoni mwa migogoro hiyo ni ya ardhi, masuala ya mirathi na utawala bora, maana yake sisi viongozi tumekuwa sehemu ya migogoro hiyo," alisema Dk. Biteko.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alisema kuwa kupitia kampeni mbalimbali, jamii imeendelea kuelimika na kuhamasika.

Dk. Dorothy aliwataka wanaume kujitokeza kutoa kero zao ili kupata elimu itakayowasaidia kutotenda matukio ya kikatili.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Pindi Chana, alisema tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, mikoa saba imefikiwa. Hiyo ni Ruvuma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Manyara, Dodoma na sasa Mkoa wa Njombe.

Alisema katika mikoa sita, migogoro 516 imetatuliwa kati ya 4,942 na kufikia wananchi 4,15,000, akiwaomba wananchi wa Njombe kujitokeza kwa wingi ili kupata fursa ya msaada wa kisheri kupitia kampeni hiyo itakayofanyika kwa siku 10.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, alisema mkoa huo umejiwekea utaratibu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kampeni hiyo imekuja wakati mwafaka kwa kuwa itaongeza thamani kwa viongozi.