BRELA: Kupata usajili,leseni ya biashara ni saa 72

By Restuta James , Nipashe
Published at 04:27 PM Jun 19 2024
 Mkurugenzi wa Leseni BRELA, Andrew Mkapa.
Picha: Restuta James
Mkurugenzi wa Leseni BRELA, Andrew Mkapa.

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umesema matumizi ya teknlojia katika kupata huduma zinazotolewa na taasisi hiyo, yameondoa urasimu na kuwawezesha wananchi kupata leseni katika kipindi cha siku moja hadi tatu za kazi.

Akizungumza kwenye mafunzo ya waandishi wa habari mjini hapa leo Juni 19, 2024; Mkurugenzi wa Leseni BRELA, Andrew Mkapa, amesema maboresho ya wakala huo ambayo yamewaruhudu wafanyabiashara kujisajili kwa mfumo wa mtandao (Online), yanalenga kupunguza muda wa kupata huduma hadi siku moja.

“Tunataka kama mfanyabiashara atakuwa amekamilisha vielelezo vyote muhimu kama namba ya mtambulisho wa mlipa kodi, kitambulisho cha taifa, vibali vya udhibiti, hati za usajili, vibali vya uhamiaji (kwa wageni) na uthibitisho wa mahali pa kufanyia biashara…akiwa na hivi vyote tunataka ahudumiwe hata ndani ya siku moja,” amesema.

Amesema BRELA inatoa leseni za biashara za kundi A kwa kampuni, viwanda na biashara zenye sura ya kitaifa na kimataifa, zikiwamo zinazoagiza au kuuza bidhaa nje ya nchi na mikoa mbalimbali.

“Huhitaji kwenda ofisi za BRELA kujisajili. Na sasa tumeboresha kiasi kwamba mfanyabiashara anaweza kuhuisha leseni yake kwa kulipia kila mwaka au kwa miaka mitatu mfululizo,” amefafanua.

Mkapa amesema BRELA inafanya mageuzi hayo chini ya programu maalumu ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI), unaolenga kurahisisha utaratibu wa uanzishaji wa biashara, kwa kuwapunguzia wafanyabiashara muda na gharama.