Bustani ya JKT Ruvu kuongeza wanyama akiwemo simba

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:41 PM May 20 2024
Simba.
Picha: Maktaba
Simba.

KIKOSI cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu, kinatarajia kuongeza wanyama akiwemo simba katika bustani yake ambayo wameifungua eneo la Ruvu Kibaha mkoani Pwani.

Bustani hiyo ya wanyama ipo katika eneo la ekari 70 zilizotengwa na kikosi hicho, kuwarahisishia wananchi kuona wanyama wa aina mbalimbali na kupiga nao picha.

Kamanda wa kikosi cha JKT Ruvu, Kanali Peter Mnyani amebainisha hayo wakati wa uzinduzi wa bustani hiyo ambayo amesema kwa sasa imeanza na wanyama wachache akiwemo Pundamilia, swali, mbuni, twiga ambao ni katika awamu ya kwanza.

Kanali Mnyani amesema mwezi Juni awamu ya pili ya wanyama wataletwa katika bustani hiyo ambao ni pamoja na Simba na kabla ya kuwekwa kwenye bustani hiyo watapatiwa mafunzo ambayo yatamuwezesha yeyote kupiga nao picha bila kudhuriwa.

Kamanda huyo amesema kuanzishwa kwa bustani hiyo itasaidia kukuza uchumi kwa kuongeza pato litakalosaidia kuhudumia vijana wanapofika kupata mafunzo katika kikosi hicho.

Akifungua bustani hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John amesema amempongeza Kanal Mnyani kwa kusimamia uanzishwaji wa bustani hiyo ambayo ambayo ni kubwa na itakayorahisisha wananchi wa mkoa huo kufika kwa urahisi na kuona wanyama.

Nickson amesema uanzishwaji wa bustani hiyo ni muendelezo wa kutangaza utalii kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo shughuli za kiuchumi katika eneo hilo pia zitakuwa na kuongeza pato katika kikosi hicho na wananchi wa jirani.

Athumani Mbega ni mmoja wa wakazi wa Mlandizi ambaye alifika katika bustani hiyo na kuongeza uanzishwaji wake unaokwenda kuwarahisiahia kuona wanyama karibu na kuokoa gharama za kwenda kwenye mbuga ambazo zipo mbali.

Katika bustani hiyo Mwananchi anapata fursa ya kulisha wanyama na kupiga nao picha bila kupata madhara kutokana na mafunzo wanayopewa wanyama hao kabla ya kuletwa kwenye bustani hiyo.