‘CCM haitashika dola kwa mabavu wala kwa bunduki’

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:15 AM Apr 17 2024
Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Oganaizesheni, Issa Haji Gavu.
PICHA: CCM
Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Oganaizesheni, Issa Haji Gavu.

KATIBU Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Oganaizesheni, Issa Haji Gavu, amesema kamwe chama hicho hakitashika dola kwa mabavu wala kutumia bunduki bali kidemokrasia.

Gavu ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano uliokutanisha viongozi wa chama, serikali, taasisi ziziso za kiserikali, viongozi wa dini, wazee na machifu katika Kata ya Mlowo, Mbozi mkoani Songwe ukiwa mwendelezo wa ziara za chama hicho

"Hatutashika dola kwa mabavu wala bunduki bali tutashika dola kwa njia za kidemokrasia. Msingi wa demokrasia ni kupiga kura na ili mwanadamu ashawishike basi una wajibu wa kumshawishi kabla ya kupiga kura", amesema.

"Tuhakikishe tunaendelea kuhamasisha na kuchapa kazi kwa kuwa ndicho kitu pekee kitakachoendelea kutupa thamani kwa wananchi kuendelea kutuamini," ameongeza.

Wakati huo huo, katika mkutano wa hadhara mkoani hapa, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema ‘atamkaba shingo’ Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha mradi wa maji mkoani Songwe unakamilika kwa wakati hyuku akisistiza kuwa lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwatua kinamama ndoo kichwani.

Pia amewataka watumishi wa halmashauri kutatua migogoro ya ardhi na kutenda haki, huku akimwagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kutoa kibali kwa wakulima na wafanyabiashara ili kuuza mazao nje ya nchi.

"Tuendelee kufanya kazi kwa juhudi. Ninatoa aelekezo kwa serikali inapaswa isimamie haki za raia watumishi wa halmashauri kuhakikisha wanatatua migogoro ya ardhi wasiruhusu wananchi wadhurumiwe ninawaomba sana sana.

"Habari ya maji Rais ametoa Sh. bilioni 100 ninaomba zisimamiwe vizuri nitambana  Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuhakikisha zinafika kwa wakati na zifanye kazi lengwa," ameahidi Dk. Nchimbi.

Kadhalika, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi kistaarabu kwa kuzingatia weledi na haki na kwamba CCM haitaki kuona mfanyabiashara anaonewa.

"Niwatake wananchi kuweka bajeti ya chakula pembezoni ya nchi kuna hali mbaya msikimbilie kuuza tu chakula kumbukeni na kuweka bajeti, Ili muweze kujiepusha na janga la njaa," amesema Dk. Nchimbi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amesema ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia mkoa umepata maendeleo makubwa ikiwamo kujengewa shule za kisasa, umeme na maji.