CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimetoa msaada wa Sh. Milioni 10 kwa waathirika wa maporomoko ya tope lililofunika nyumba 20 na shule moja katika Kata ya Itezi jijini Mbeya.
Msaada umetolewa leo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi alipowatembelea waathirika hao ambao wanaishi kwenye kambi iliyowekwa katika Shule ya Msingi Tambuka Reli.
Akizungumza na waathirika hao, Dk. Nchimbi amewataka kufuata maelekezo ya serikali ikiwa ni pamoja na kutorejea kwenye makazi yao ambayo yalikumbwa na maporomoko.
“Sisi kama chama tunawapa pole sana waathirika wote wa maporomoko hayo, lakini tunawasihi sana msirejee kwenye yale maeneo mpaka wataalamu watakapofanya utafiti, pia muepuke kujenga makazi kwenye maeneo yote hatarishi,” amesema Dk. Nchimbi.
Akitoa taarifa ya tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema waathirika wanaoishi kwenye kambi hiyo wapo 51 na kwamba wanaendelea kuhudumiwa na serikali pamoja na wadau.
Malisa, amesema wataalamu mbalimbali wakiwamo wa miamba wanaendelea na uchunguzi kwenye eneo yalikotokea maporomoko hayo ili kubaini chanzo cha tukio hilo.
Hata hivyo amesema taarifa za awali zinaonyesha eneo hilo bado ni hatarishi na hivyo wananchi wamezuiliwa wasiende kwenye makazi yao mpaka majibu ya utafiti yatakapotoka.
“Baada ya tukio lile Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilifika kwa ajili ya kuangalia kilichotokea na iliagiza waathirika wakae hapa shuleni kwa muda wakati wanasubiri taratibu zingine, kwahiyo hapa wanapata huduma mbalimbali za kibinadamu,” amesema Malisa.
Amesema waathirika hao wamepata huduma mbalimbali ikiwamo huduma za afya, ushauri nasaha kutokana na baadhi yao kuathirika kisaikolojia, chakula, vifaa vya kulalia.
Akizungumza kwa niaba ya waathirika hao, Diwani wa Kata ya Itezi, Sambue Shitambala ameishukuru serikali na wadau mbalimbali kwa kuendelea kuwasaidia waathirika hao tangu siku ya kwanza huku akiwaomba na wadau wengine kuendelea kuwaunga mkono.
Kimahesabu ni kwamba Sh. Milioni 10 iliyotolewa na CCM, ikigawanywa sawa kwa waathirika wote 51 kila mmoja atapata Sh. 197,000.
Maporomoko hayo yalitokea Aprili 14 asubuhi ambapo baadhi ya wananchi walikuwa wanajiandaa kwenda kanisani na wengine walikuwa wameshaondoka hali ambayo inadaiwa kuwa chanzo cha maisha yao kunusurika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED