MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kuanzisha operesheni Maalum ya kuwasaka waganga wote wa kienyeji ambao wanajihusha na vitendo vinavyochangia kuwapo mauaji ya watu wenye ulemavu.
Chalamila ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika ambayo kimkoa yalifanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam jana.
Amesema, maadhimisho hayo yaliandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, huku Chalamila akiwa mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri Dk.Dotothy Gwajima.
Amesema, ataandaa utaratibu maalum wa kufanya operesheni hiyo baada ya kukutana na viongozi wenzake.
Mkuu huyo wa mkoa amesema, kama waganga wa aina hiyo wapo mkoani mwake, wajiandae kuhamia kwingine, kwa kuwa hawataki mkoani mwake.
"Wanashawishi watu kuua wenye ulemavu wa ngozi, lakini pia wanaweza kusema wanatamka watu wafupi, wenye vipara au vyovyote vile. Sasa natangaza kuanza msako," alisema Chalamila.
Aidha, amekemea watu kushabikia vitendo vya udhaliliaji wa watoto na utu wao, wazazi kuwa na matendo mema ambayo watoto wanaweza kujifunza kwao.
"Tusilalamikie teknolojia kuwa inamomonyoa maadili, wawawekee watoto wao kiwango ya kutumia teknolojia badala yake tunawasaidie kujua umuhimu wake na jinsi ya kutumia," amesema..
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk. Amon Mapanju, amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu haina budi kuzingatiwa na wazazi na walezi.
Ameitaja kaulimbiu hiyo kuwa ni; "Elimu Jumuishi kwa Watoto Kuzingatie Ujuzi, Maadili na Stadi za Kazi; Wajibu wa Wazazi na Jamii Katika Kumsaidia Mtoto katika Kufikia Malengo yake kwa Maendeleo ya Baadaye".
"Lengo la kaulimniu hii inakumbusha kupaza sauti kwa watoto na kuhakikisha wanapata elimu inayoendana na sayansi na teknlojia itakayowawezesha kwenda sambamba na soko la ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri na kutumia vifaa vya teknolojia ikiwamo kompyuta, hivyo ni muhimu wazazi na walezi kuharakisha watoto wao wanapata elimu," amesema Dk. Mapanju.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED